KUMFANYIA SHINGO NGUMU NA KUMPINGA ROHO MTAKATIFU.




Bibilia inatuambia sisi watu ambao tumeamua kumpokea na kumwamini Yesu na kumfanya Bwana na Mwokozi wa maisha yetu:

“Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;” (YN. 1:12 SUV).

Kwa hiyo kila mmoja wetu aliyempokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yake amepewa uwezo wa kufanyika mtoto wa Mungu.
Huu uwezo unajidhihirisha katika huduma na kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha ya mwamini.

Moja ya majina ambayo Roho Mtakatifu anaitwa kwayo ni "ROHO WA KUTIFANYA WANA."

Maandiko yanasema:

“Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba.” (RUM. 8:15 SUV).
Huyu Roho wa kufanywa wana anayetajwa katika huu mstari ni Roho Mtakatifu.
Kwa kadiri mimi na wewe tunavyoitikia huduma na kazi ya Roho Mtakatifu maishani mwetu tunaudhihirisha uwana katika maisha yetu.
Ndo maana maandiko yanasema:
“Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu.” (RUM. 8:14 SUV).
Kwa hiyo uwana wetu unadhihirishwa pale tunapokubali na kuitikia uongozi wa Roho Mtakatifu katika maisha yetu.

Maandiko pia yanasema:
“Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda" (EZE. 36:27 SUV).
Katika hili andiko Roho Mtakatifu anafananishwa na dereva anayeyaendesha maisha yetu na anayaendesha maisha yetu katika sheria za Mungu ili kuzishika na kuzitenda.

Kimsingi Roho Mtakatifu ameachiliwa maishani mwetu ili atusaidie kutembea katika njia za Mungu au kwa maneno mengine kuyaishi maisha ya Ukristo.

Yesu alipokuwa anamtambulisha Roho Mtakatifu kwetu alisema:

“Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.” (YN. 14:26 SUV).

Yesu alisema Roho Mtakatifu atakapokuja atatufundisha mambo yote na kutukumbusha yote ambayo Yesu ametuambia.

Kwa hiyo ikitokea tunataka kwenda nje ya njia au nje ya utaratibu, Roho Mtakatifu atatukumbusha ni neno gani tunakaribia kulikiuka ili kutusaidia tusitoke nje ya njia.

Hilo neno inawezekana tumelisoma wenyewe au tumewahi kulifundishwa mahali.

Huduma ya Roho Mtakatifu kwa sehemu kubwa ni kutukumbusha yale tuliyoambiwa au kufundishwa lakini pia ni kutufundisha kwa kutufanya tuelewe neno tunalolisoma na jinsi ya kuliishi kiuhalisia maishani mwetu ya kila siku.

Lakini pia Yesu alifundisha kuhusu Roho Mtakatifu:

“Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.” (YN. 16:13 SUV).

Roho Mtakatifu anatuongoza na kututia kwenye Kweli yote.

Yaani anahakikisha maisha yetu yanatembea na kuishi katika kweli yote ya neno la Mungu.

Hata Paulo alipokuwa akiwaandikia Wagalatia na kuwaonya kuhusu matendo ya mwili aliwaambia:

“Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.” (GAL. 5:16-17 SUV).

Laiti tungeenenda kwa Roho wala kamwe tusingetimiza tamaa ya mwili.

Tunaishi kwa kufuata matendo ya mwili kwa sababu hatukubali kuenenda kwa Roho.

Katika lugha ya asili hilo neno "enendeni" linatupa maneno matatu katika lugha yetu ya kiswahili:

(i). Kumwitikia.

(ii). Kuendeshwa.

(iii). Kuongozwa.

Kwa hiyo ili tusitimize tamaa za mwili maishani mwetu inatupasa kukubali kumwitikia Roho Mtakatifu pale anapotusemesha au kutubonyeza kitu.

Ili kutotimiza tamaa za mwili tunatakiwa tuwe tayari kuendeshwa Naye.

Ili tuishi maisha ya kutotimiza tamaa za mwili inabidi tuwe tayari kuongozwa Naye.

Katika maisha ya mwamini kutakuwa na mashindano makubwa sana kati ya Roho Mtakatifu na miili yetu yaani kile Roho Mtakatifu anataka kwa ajili yetu na kile miili yetu inataka.

Haya mashindano yanapelekea sisi kutofanya yale tunayotaka kutegemeana ni nani tunamwitikia yaani Roho wa Mungu au miili yetu.

Mtu ambaye kila wakati anauitikia mwili wake hawezi kuishi maisha ya rohoni ya kumpendeza Mungu na yule anayemwitikia, kuendeshwa na kuongozwa na Roho Mtakatifu hawezi hata siku moja kuishi kwa kufuata tamaa za mwili.

Kimsingi maisha ya Ukristo au maisha yetu kama watoto wa Mungu ni maisha ya kumwitikia, kuendeshwa na kuongozwa na Roho wa Mungu.

Kama tukitaka kuishi maisha ya ushindi hatuna budi kukubali kumwitikia, kuendeshwa na kuongozwa na Roho Mtakatifu maishani mwetu.

Kwa kadiri tunavyoyafungua maisha yetu kwa neno la Mungu kwa njia ya kulisoma na kufundishwa na kuhubiriwa, tunazidi kurahisisha hii kazi na huduma ya Roho Mtakatifu maishani mwetu.

Maandiko yanasema:

“Kwa kuwa nimejaa maneno; Roho iliyo ndani yangu hunihimiza.” (AYU. 32:18 SUV).

Kwa hiyo kwa kadiri tunavyoyajaza maisha yetu na neno la Mungu kwa njia ya kulisoma sisi wenyewe na kufundishwa na kuhubiriwa neno, inatoa uwepesi kwa sisi kusikia na kuitikia mhimizo wa Roho Mtakatifu kwetu.

Roho Mtakatifu atatuhimiza katika yale ambayo tumeyasoma na kufundishwa na kuhubiriwa.

Kila tunapokuwa mahali pa maamuzi au tunataka kufanya jambo, kwa lile neno ambalo lipo ndani yetu, Roho Mtakatifu atatuhimiza ama tufanye au tusifanye ili kutusaidia kuishi kwa kuiheshimu kweli maishani mwetu.

Ndiyo maana ni muhimu sana kwa mwamini kulijaza neno la Mungu maishani mwake kwa njia ya kulisoma na kufundishwa na kuhubiriwa.

“Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu.” (KOL. 3:16 SUV).

Wajibu wa kulijaza neno maishani mwetu ni lako na langu kwa njia ya kuishi maisha ya nidhamu ya kulisoma neno la Mungu na kulifundishwa na kuhubiriwa maishani mwetu.

Roho Mtakatifu anaweza tu akatuhimiza kwa kadiri ya neno lililo ndani yetu.

Kumbuka kuwa moja ya kazi za Roho Mtakatifu ni kutukumbusha na anatukumbusha lile ambalo tumewahi kusoma au kulisikia.

Tunapokuwa tunayafunga maisha yetu kwa neno la Mungu kwa kutolisoma, kutolifundishwa na kutolihubiriwa, tunaondoa uwezekano wa Roho Mtakatifu kutuhimiza.

Maandiko yanasema:

“Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.” (RUM. 10:17 SUV).

Unaona hiyo sehemu ya pili ya mstari ambao tumetoka kuunukuu?

"kusikia huja kwa neno la Kristo."

Usomaji wa neno la Kristo au neno la Mungu maishani mwako unakupa uwezo wa kuisikia sauti ya Roho Mtakatifu anapokuhimiza maana atakuhimiza sawa na neno la Mungu maishani mwako kwa kuthibitisha au kupinga yale ambayo unataka kufanya au unafanya.

Pia maandiko yanasema:

“Na ingawa Bwana atawapeni chakula cha shida na maji ya msiba, lakini waalimu wako hawatafichwa tena, ila macho yako yatawaona waalimu wako; na masikio yako yatasikia neno nyuma yako, likisema, Njia ni hii, ifuateni; mgeukapo kwenda mkono wa kulia, na mgeukapo kwenda mkono wa kushoto.” (ISA. 30:20-21 SUV).

Nataka tuone pale anaposema "waalimu wako hawatafichwa, ila macho yako yatawaona waalimu wako."

Ina maana ni mapenzi ya Mungu kutuongoza kwa watu ambao watafanyika waalimu kwetu na kutufundisha na huko kufundishwa kutatupelekea kusikia sauti nyuma yetu ikituambia njia ni hii tugeukapo kutaka kwenda mkono wa kushoto au wa kulia.

Sauti hiyo tunayoisikia ni ya Roho Mtakatifu ila kinachotuwezesha kuisikia ni pale tunapoyafungua maisha yetu kwa mafundisho sahihi ya neno la Mungu na hii sauti inakuja kwetu tunapotaka kugeuka au kwa maneno mengine tunapotaka kufanya maamuzi mbali mbali maishani mwetu.

Mara nyingi Roho Mtakatifu anatuhimiza kwa kushuhudia pamoja na roho zetu au kusema huku ndani na roho zetu.

“Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;” (RUM. 8:16 SUV).

Roho Mtakatifu akikushuhudia ghafla tu huku ndani unajikuta unajua kuwa jambo fulani ni sahihi au sio sahihi.

Ghafla unajua kuwa hii njia ni sahihi au siyo sahihi.

Labda tu wewe mwenyewe uamue kufanya shingo yako ngumu na uwe mkaidi.

Sasa kazi na huduma hii ya Roho Mtakatifu katika maisha ya mwamini inaweza kukutana na upinzani kutoka kwa huyo mwamini, kwa huyo mwamini kuwa na shingo ngumu au kwa maneno mengine kuwa mgumu kugeuka anaposemeshwa na Roho Mtakatifu.

Kwa njia hiyo akajikuta anampinga Roho Mtakatifu.

“Enyi wenye shingo ngumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo.” (MDO 7:51 SUV).

Mimi na wewe tunampinga Roho Mtakatifu kwa kuzifanya shingo zetu ngumu au kuwa wagumu kugeuka pale anapotusemesha.

Mioyo isiyotahiriwa ni mioyo ambayo ipo kama haielewi neno la Mungu au maneno au mhimizo wa Roho Mtakatifu.

Masikio ambayo hayajatahiriwa vivyo hivyo.

Yanakuwa magumu kusikia sauti ya Roho Mtakatifu.

Tunakuwa wagumu kumwitikia, kuendeshwa na kuongozwa Naye.

Roho Mtakatifu anategemea pale anapotusemesha kwa kutushuhudia ndani ya roho zetu tutaitikia mara moja lakini shida yetu au tunakuwa wazito kuitikia au tunapotezea kabisa ule ushuhuda wa Roho Mtakatifu ndani yetu.

Maandiko yanasema:

“Geukeni kwa ajili ya maonyo yangu; Tazama, nitawamwagia roho yangu, Na kuwajulisheni maneno yangu.” (MIT. 1:23 SUV).

Huu mstari ni kama umeandikwa mbele nyuma.

Ili kuweza kuelewa maana yake inabidi usome sehemu ya pili ndipo usome ya kwanza yaani "Tazama nitawamwagia Roho Wangu na kuwajulisheni maneno yangu. Geukeni kwa sababu ya maonyo yangu."

Roho Mtakatifu anapomwagwa maishani mwetu, anatujulisha maneno ya Mungu.

Sasa pale anapotujulisha hayo maneno ya Mungu, tunatakiwa sisi, mimi na wewe, tugeuke na kwenda sawa na hayo maneno anayotujulisha.

Shida yetu kubwa ni kumfanyia jeuri Roho wa Bwana.

“Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?” (EBR. 10:29 SUV).

Ujeuri ni kutokubali maelekezo.

Tunaelekezwa na Roho Mtakatifu lakini sisi ni wabishi.

Ukitaka kujua kuwa huwa sisi tunafanyaga dhambi makusudi ni pale ambapo unatukuta tunajificha ili kufanya dhambi.

Ile kujificha ni ushahidi kuwa tunajua kuwa tunachofanya sio sawa.

Tatizo la kutotaka kuelekezwa inaweza kupelekea kuvunjika kwa hizo shingo ambazo tunazishupaza kwa Roho Mtakatifu.

“Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, Atavunjika ghafula, wala hapati dawa.” (MIT. 29:1 SUV).

Roho Mtakatifu atakuwa mwaminifu kukuonya mara kwa mara kuhusu jambo fulani au mambo fulani maishani mwako.

Ukishupaza shingo au ukigoma kugeuka, shingo (uwezo wa kugeuka) itavunjika ghafla pasipo dawa.

Kwa maneno mengine upo muda ambao ni rahisi kumwitikia Roho Mtakatifu na kutoka katika shida au changamoto hasa ya kitabia na ya kimwenendo ambayo tumo.

Lakini hiyo itategemea mwitikio wetu wa haraka kwa maonyo, uongozi, kuendeshwa na kuongozwa na Roho Mtakatifu.

Tukishupaa na njia zetu tunaweza kupoteza uwezo wa kugeuka ghafla pasipo dawa na ikatutumbukiza kwenye vifungo ambavyo sasa hatujui tufanyaje na hata tungejua cha kufanya hatuna uwezo wa kufanya.

Ninaamini kuna kitu umekipata katika shule hii.

Mungu atusaidie tuzidi kukua katika kushirikiana na, na kuitikia kazi ya Roho Mtakatifu maishani mwetu.

Mungu akatusamehe pale tulipofanya shingo zetu ngumu na kumpinga Roho Mtakatifu maishani mwetu.

Mungu akatusamehe kila tulipomfanyia jeuri Roho wa Neema katika maisha yetu.

Mungu asituondolee Roho Wake Mtakatifu maishani mwetu.

Mungu atuhurumie na kuturehemu na akairejeshe huduma na kazi ya Roho Mtakatifu maishani mwetu.

Tukapewe sasa uwezo wa kumwitikia, kuendeshwa, na kuongozwa Naye katika Jina la Yesu.

Kama baada ya kusoma somo hili unahisi umekuwa ukimpinga Roho Mtakatifu maishani mwako na kumfanyia jeuri, ongea Naye kama mtu ambaye unamwona, mwombe msamaha na mwombe arejeshe tena kazi na huduma Yake maishani mwako mana bila Roho Mtakatifu inaweza kuwa ngumu sana maishani mwako.

Ubarikiwe sana.

Nakupenda sana.

Nakuombea sana.

Ndiyo maana Mungu ananipa hizi shule nikugawie na wewe.

UMEBARIKIWA.

MCHUNGAJI NA MWALIMU

CARLOS RICKY WILSON KIRIMBAI.

WHATSAPP #:+255786312131.

Post a Comment

0 Comments