Na Peter M Mabula. Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU. |
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kanisa ni jumuia ya Wakristo.
Kanisa ni watu walioitwa na kutengwa na mambo ya dhambi.
1 Kor 6:17-18 '' Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema BWANA, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa BABA kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,''
Maandiko hayo ni sehemu tu ndogo ya maandiko yanayolitambulisha Kanisa la KRISTO duniani.
Kanisa hai wametengwa na uovu wa dhambi na wametengwa na mambo ya kidunia yaliyo machukizo(Machafu).
Ndio maana huwezi kumuona Askofu akiwa disko akicheza.
Huwezi kumuona Mkristo aliyeokoka akiwa kwa mganga wa kienyeji.
Huwezi kumuona Mchungaji anatoa talaka.
Huwezi kumuona Mteule wa MUNGU akivuta sigara wala bangi na tena huwezi kumuona mteule wa KRISTO akitumia madawa ya kulevya.
Huwezi kuona kanisa wakichukua mapanga na mikuki wakienda kulipiza kisasi kwa maadui zao.
Kanisa ndilo pekee linalosababisha amani Duniani.
Kanisa ni la muhimu sana duniani.
Siku Kanisa la MUNGU likiondolewa duniani ndipo neema itatoweka.
Kibiblia katika migao saba ya nyakati huu ni wakati wa Kanisa au wakati wa Neema.
Kanisa la KRISTO ndilo pekee linalomwabudu MUNGU aliye hai na wa kweli.
Kama kuna kanisa halijafikia hali hiyo basi hilo sio kanisa la KRISTO ila ni kanisa la kibinadamu tu.
Katika Kanisa MUNGU ameweka viongozi na wasimamizi ili kazi ya MUNGU itendeke vizuri.
Matendo 20:28 '' Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi(Kanisa) lote nalo, ambalo ROHO MTAKATIFU amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake MUNGU, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.''
Kanisa ni la Muhimu sana ndio maana shetani huliwinda kanisa kuliko kitu chochote. Lakini kanisa linamshinda shetani kwa damu ya YESU KRISTO na kwa Neno la ushuhuda na kwa kuvumilia katika MUNGU aliye hai.
Ufunuo 12:11 ''Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.''
Kwa sababu kanisa ndicho kitu pekee ambacho shetani hakitaki basi amejribu mara kadhaa kuleta makanisa feki yanayomtukuza yeye na mengine yanamwabudu yeye, lakini hiyo haina maana kwamba kanisa la kweli halipo bali lipo na linazidi kuchanua.
shetani amejaribu kubuni dini nyingi sana lakini Kanisa la MUNGU lipo na litaendelea kuwepo na litaendelea kushinda na zaidi ya kushinda maana kanisa la KRISTO ndilo lililolibeba kusudi la MUNGU.
Madhehebu sio kanisa ila ni ni sehemu tu ambapo kanisa(Wakristo) wanakutana na kumwabudu MUNGU. Ndio maana wakati mwingine dhehebu moja linaweza kuhama kutoka kwa KRISTO kwa sababu ya viongozi wao waliojikinai lakini Kanisa la kweli la KRISTO bado lipo na linaendelea. Hatuendi mbinguni kama dhehebu bali tutaenda mbinguni kama kanisa la KRISTO lililoshinda duniani.
Kiongozi wa Kanisa akinaswa na shetani hakika kondoo kutawanywa kiroho itakuwa rahisi sana.
Mara nyingine tumesikia baadhi ya viongozi wa kanisa la kweli wakivamiwa na shetani na kuondoka katika kusudi la MUNGU.
Hapa nimekuandalia mambo saba ambayo mimi Peter Mabula ninaona kama ndiyo yanayoweza kulitafuna kanisa la kweli.
1.Dhambi kwa viongozi wa kanisa.
Hosea 4:6 '' Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako.''
Madhara makubwa zaidi yanayoweza kuliathiri kanisa ni dhambi kwa viongozi wa kanisa. Watu wa kanisani wanaweza wakaangamizwa sawasawa na watu wa mataifa kwa sababu ya viongozi wa kanisa. Kiongozi wa kanisa akiisahau sheria(Neno la MUNGU lote) anaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiroho kwa kanisa.
Kiongozi akiwa mdhambi itakuwa vigumu sana yeye kukemea dhambi katika kanisa na kwa njia hiyo watu wa MUNGU watakuwa wanaangamiza kwa kukosa maarifa.
Kama mchungaji ni mzinzi ni vigumu sana yeye kukemea uzinzi.
Kama Mchungaji ni mwizi ni vigumu sana kukemea wizi.
Kama Askofu ni muongo ni vigumu sana kukemea uongo kanisani.
2.Viongozi wa kanisa kutendea kazi kila neno wanaloambiwa na waumini au jirani wa waumini.
1 Timotheo 5:19-22 ''Usikubali mashitaka juu ya mzee, ila kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu. Wale wadumuo kutenda dhambi uwakemee mbele ya wote, ili na wengine waogope. Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, na mbele za malaika wateule, uyatende hayo pasipo kuhukumu kwa haraka; usifanye neno lo lote kwa upendeleo. Usimwekee mtu mikono kwa haraka, wala usizishiriki dhambi za watu wengine. Ujilinde nafsi yako uwe safi.''
Katika maandiko haya tunaweza kujifunza mambo mengi sana lakini kulingana na somo langu katika kipengele hiki cha pili, kunahitajika umakini sana kwa viongozi wa kanisa katika vile wanavyoambiwa na waumini au majirani wa baadhi ya waumini.
Kwanza kiongozi anapoambiwa jambo na mmoja wa waumini wake ambalo linamweka hatiani mtu mwingine haitakiwi kiongozi huyo kumwita haraka haraka tu mtuhumiwa na kumuonya au kumtenga, mambo hayo yanalitafuna sana kanisa leo.
Haina maana kwamba usifanyie kazi unayoambiwa na waumini wako au majirani wa waumini wako lakini hakikisha unafanya uchunguzi wa kina wewe mwenyewe ili pasitokee uonevu. Kama kuna mtu umemuonea wewe mchungaji hakika mtu huyo hata kama atakuwa anakuja kanisani lakini hatakusikiliza na hatazingatia Neno la MUNGU unalomfundisha, hadi uweke mambo sawa.
Mara nyingine watu wenye makosa ndio huwa wa kwanza kukimbilia kwa Mchungaji ili kuwasema wengine kama njia ya kujisafisha na kuonekana wema.
Inawezekama mmoja wa wana kanisa anatuhumiwa na mtu mwingine wa kanisani kwamba ni mzinzi kwa sababu tu alionekana akitembea barabarani saa saba usiku. Mchungaji kama atamwita mtuhumiwa haraka tu na kumfukuza kanisani au kumsema hadharani kanisani, na kama jambo hilo amesingiziwa hakika hapo kanisa litakuwa limetafunwa sana maana huyo naye anaweza akaanza kuitafuta haki yake kwa nguvu, anaweza akaacha kwenda kanisani na kujiangamiza kabisa, anaweza akarudi nyuma kiroho.
Kama amekosea inabidi kiongozi ajilidhishe kwanza ndipo atoe hukumu. Namna nzuri ya kujilidhisha ni kupata ushahidi kutoka kwa watu wawili au watatu ndivyo Biblia inashauri hapo juu.
Dhambi lazima zikemewe kanisani lakini iwe ni kweli dhambi imetendeka, sio kusingiziwa.
Biblia inakushauri kiongozi wa kanisa kwamba usihukumu kwa haraka ila thibitisha kwanza. Usipendee mtu, lakini kama utaamua haraka haraka tu mambo yanayowahusu waumini hakika unaweza kujikuta umependelea pasipo sababu.
3.Kuwepo wakala wa shetani katikati ya kanisa.
1 Yohana 4:1-3 ''Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na MUNGU; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani. Katika hili mwamjua ROHO wa MUNGU; kila roho ikiriyo kwamba YESU KRISTO amekuja katika mwili yatokana na MUNGU. Na kila roho isiyomkiri YESU haitokani na MUNGU. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani.''
Shetani hutaka sana kuingia kanisani ili aharibu utakatifu wa kanisa.
Kanisa ni lazima lisimame katika kweli ya Neno la MUNGU.
Viongozi wa kanisa ni lazima sana walisimamie kusudi la MUNGU kwa kulitii sana Neno la MUNGU.
Kwa tamaa za pesa le kuna baadhi ya watumishi hutunga vitu vya uongo ili tu kujipatia waumini au kupata pesa.
Sio kila miujiza ni ya MUNGU na sio kila anyehubiri watu ni anataka watu hao waende uzima wa milele. Kila mtu anaweza kuwa mchungaji akiamua lakini kama huyo hamtii KRISTO hakika huyo ni wakala wa shetani kanisani.
roho ya mpinga Kristo ipo na kazi yake ni kuaondoa watu kwa KRISTO.
Hatuhitaji kumwabudu MUNGU kupitia sanamu au maji ya baraka, hatutakiwi kumwabudu MUNGU kupitia watu wanaojiita MUNGU.
Tunatakiwa kumwabudu MUNGU kupitia YESU KRISTO na sio vinginevyo.
4. Kanisa kuacha maombi.
1 Thesalonike 5:17 '' ombeni bila kukoma; ''
Maombi ni maisha hivyo hayatakiwi kuwa ya msimu tu bali ya siku zote.
Kanisa likisahau maombi kuna madhara yatatokea maana kuona rohoni kutapungua, hamu ya kuendelea na wokovu itapungua.
Kanisa lisipokuwa na maombi ni rahisi shetani kupanda magugu ndani ya kanisa na kuyang'oa magugu hayo ikawa ni vigumu.
Kanisa halitakuwa kuwa na maombi tu bali pia ni lazima kanisa liwe na maombi ya kufunga kila mara.
Kanisa kama mtu binafsi wa kanisani lazima afundishwa kuomba na kufunga na awe anafunga ili kunoa makali yake ya kiroho na ili aweze kujibiwa mahitaji yake anayakayo.
Kuna mengine hayawezi kuondoka katika kanisa hadi kanisa lifunge na kuomba.
Mathayo 17:21 ''Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.''
5. Kanisa kutembea katika maono ya uongo yanayoambatana na ujanja ujanja wa watumishi.
Mathayo 15:8-9 ''Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.''
Kama kanisa litamwacha KRISTO na Neno lake hakika shetani atachukua nafasi tu na jambo hilo kupelekea uongo kuanza kuliendesha kanisa.
shetani akitawala kanisa ni lazima waumini wawekewe mipaka na kufundishwa kujiona kwamba wao tu ndio kanisa na kwingine kote ni kwa shetani. Biblia ndio inatakiwa iwe ushahidi na sio watumishi kuwadanganya watu.
Sio kila mchungaji au Askofu ameitwa na MUNGU, Wengine wamejita na wengine wameitwa na shetani.
Shetani ni baba wa uongo hivyo na watumishi wake lazima wabuni vitu vya uongo na lazima kanisa litembee katika maono ya uongo, mambo haya yanalitafuna kanisa sana.
Leo kuna wachungaji hawamhubiri KRISTO tena bali wanajihubiri wenyewe na kudanganya watu. Kanuni ya Biblia pia inatafasiriwa vibaya na baadhi ya watu. Ngoja nikuambie; Japokuwa Ibrahimu Ni Baba Wa Imani Lakini Hiyo Haina Maana Kwamba Sara Ni Mama Wa Imani. . Mambo Ya Kiroho Huwa Tofauti Na Mambo Ya Kibinadamu. Tukiruhusu Kanisa Liifuate Dunia Basi Ipo Siku Tutasikia Kwamba Stephano Au Ayubu Ni Babu Wa Imani. Dunia Leo Imeingia Kanisani Ndio Maana Kuna Mawakala Wa shetani Hujipachika Katika Baadhi Ya Maandiko Na Kudai Maandiko Hayo Yaliwatabiri Wao. Kuna Watu Hudai Wao Ni Eliya Amerudi Duniani, Kuna Watu Hujiita Kristo, Kuna Watu Hujiita Henoko Aliyerudi Duniani, Wengine Hudhani Kuna Mtu Anaitwa Mama Wa Mungu leo. Kuna Watu Hujiita Mungu Muumbaji Aliyekuja Kuishi Na Wanadamu Na Kuna Waongo Original Hudai Biblia Iliondolewa Zamani Na Kuja Kitabu Kingine. Kanuni Ya Biblia Iko Tofauti Sana Na Kanuni Za Kibinadamu Au Kanuni Za Kimwili. Ukitaka Biblia Ikufuate Utaishia Pabaya. Wewe Mwanadamu Ndio Unatakiwa Uifuate Biblia. Biblia Haiwezi Kubadilishwa Na Mazingira Wala Haiwezi Kubadilishwa Na Wanadamu. Kataa Kuokoka Harafu Utarajie Mbingu, hakika hakuna mbingu kwa wanaokataa kuokolewa na BWANA YESU(Yohana 3:16-21). Mkatae YESU Ukidhani Utafika Mbinguni, hakika huwezi kufika(Matendo 4:12)
6. Kanisa kukosa upendo.
1 Petro 1:22-23 ''Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo. Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele. ''
Upendo wa KiMUNGU ni hali ya kumpenda mtu bila kujali mtu huyo alivyo au ana sifa gani.
Lazima kanisa liwe na upendo. Kanisa lazima limpende mchungaji wao na sio kumsema vibaya. Kumbuka kuwa mkimsema vibaya mchungaji wenu hakuna atakayemsema vizuri huko nje, hakuna atakayekuja kuokoka maana atadhani kanisa halifai kumbe ni kukosekana kwa upendo.
Lazima kanisa wapendane wote bila kujali cheo cha mtu au hadhi ya mtu. Ukikosekana upendo wa kiMUNGU kanisani hakika jambo hilo litalitafuna sana kanisa na kanisa halitastawi kamwe.
''Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.-1 Kor 13:4-7 ''
7. Kutokubali kukosolewa au kusahihishwa.
1 Kor 8:2 ''Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua.''
Hakuna mwanadamu anayejua yote na hakuna mwanadamu anayeweza yote.
Katika kanisa wote tunategemeana. Hata Mchungaji kuna baadhi ya mambo hajui na anahitaji kusaidiwa, Hata mama mchungaji sio kwamba anajua yote kuliko wanawake wote kanisani. Sio kwamba wazee wa kanisa hawana la kusaidiwa bali yapo tena mengi.
Sio kwamba matumizi ya kanisa yakienda vibaya basi wanaotaka kushauri wafukuzwe kanisani.
Vitu vya kanisa ni vya kanisa na sio mali ya kiongozi wa kanisa hivyo kuna wengine akitaka kusaidiwa tu kwa upole anaanza kuhubiri kwamba roho ya uasi na kukosa heshima imeingia kanisani.
Kama Mchungaji angekuwa anajua yote ana anaweza yote basi kusingekuwepo kiongozi wa ibada kanisani, kusingekuwepo mashemasi kanisani, kusingekuwepo wapiga vyombo na kusingekuwepo waimbaji. Lakini kwa sababu kila mtu kanisani ni muhimu basi ni muhimu sana kusaidiana ili kuondoa lawama zisizokuwa na sababu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili
0 Comments