MAOMBI YA KUZIAMURU BARAKA ZAKO ZIKUFUATE.
Na Peter M Mabula. Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU. |
Bwana YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze.
Leo omba ukiamuru baraka zako zikufuate.
Jambo muhimu kabla ya yote hakikisha uhusiano wako na Bwana YESU ni mzuri ndipo uombe.
Wakati mwingine baraka fulani haijaja kwako kwa sababu hujaiamuru ije kwako kwa njia ya maombi au maombi ya kufunga.
Kumb 28:8 '' BWANA ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako. ''
MUNGU huiamuru baraka ije kwako kwa kukufungulia mlango wa baraka hiyo kupita na kuja kwako.
Ona Mfano hapa ambapo MUNGU aliamuru baraka ya chakula cha mbinguni ishuke kwa wana wa Israeli. Biblia inasema
Zaburi 78:23-25 '' Lakini aliyaamuru mawingu juu; Akaifungua milango ya mbinguni; Akawanyeshea mana ili wale; Akawapa nafaka ya mbinguni. Mwanadamu akala chakula cha mashujaa; Aliwapelekea chakula cha kuwashibisha.''
Lakini ni muhimu kujua kwamba kama uhusiano wako na MUNGU uko vibaya hakika MUNGU hataiamuru baraka yako ije kwako kupitia maombi yako.
Biblia inasema '' Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.Kwa maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu, na vidole vyenu vimetiwa unajisi kwa uovu; midomo yenu imenena uongo, ndimi zenu zimenong'ona ubaya. Hapana adaiye kwa haki, wala hapana atetaye kwa kweli; hutumainia ubatili, hunena uongo; hupata mimba ya madhara, na kuzaa uovu.-Isaya 59"1-4''
Mkono wa MUNGU wa baraka haukupungua hata usiweze kukubariki ila maovu yako ndio yamekufarakanisha wewe na Muumba wako hata hukupokea baraka zako..
Ni muhimu sana kutengeneza na MUNGU ndipo uzihitaji baraka zake.
Bwana YESU alitupa kanuni ya kupokea kutoka ulimwengu wa roho.
Mathayo 7:7-8 '' Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.''
Kwa maana nyingine unaweza kusema hivi ombeni nanyi mtapokea ila msipoomba hamtapokea maana hamukuomba.
Baraka zako ni zipi hata usipokee?
Ndugu leo omba ukiziamuru baraka zako zikufuate na utazipokea kwa jina la YESU KRISTO.
Ngoja nikupe ushuhuda kidogo.
Mtumishi wa MUNGU mmoja ambaye ni rafiki yangu siku moja alikuwa anatufundisha na kusema kwmba; Alipotaka kuoa ilimsumbua sana maana mabinti wote walikuwa wanamkataa kwa sababu walimuona mkali sana na alikuwa na sura ya ukali sana. Kila akitaka kumchumbia binti alikataa na kusema kwamba huyo hafai maana ni mkali sana. Baadae yule mtumishi aliamua kusema kwamba ''Baraka yangu ya mke mwema niamuru inifuatena jambo hili sitaliombea tena na sitamwambia binti yeyote tena duniani ili anikubali kumchumbia kisha tufunge ndoa''
Yule mtumishi baada ya hapo alianza tu kumtumikia MUNGU kwa uaminifu na hadi watu wakawa wanamshangaa, hata mwaka na nusu haukufika, Binti mmoja ambaye alikuwa mkoa jirani alionyeshwa na MUNGU yuu ya mume wake na akaelekezwa mahali anaposali huyo kijana. Yule Bibti alisafiri kutoka mkoa huo kuja Dar es salaam na kwenda pale Kanini na kumwambia Mchungaji. Baadae huyu kijana mtumishi alipokuwa anatoka Ibadani aliitwa na viongozi wake wa kanisa na kumwambia yule binti alikuwa pamoja na wale vingozi wa kanisa. Yule Binti akasema ''Hakika ni huyo ambaye nimemuona kwenye maono na nikaelekezwa kuja hapa'' Yule kijana baada ya kuelezwa alilia na MUNGU akamsemesha kwa sauti kwamba yule ndiye. Baada ya hapo walifunga ndoa na hadi sasa wana zaidi ya miaka 12 katika ndoa, huku wakiwa na watoto watatu na ndoa ni paradiso ndogo kwao.
Umejifunza nini?
Ndugu wakati mwingine unatakiwa kuiamuru baraka yako ikufuate.
Kuna watu ni kama Pesa inawafuata maana Baada ya maombi wakianzisha mradi fulani hufanikiwa sana lakini wengine wakianzisha mradi kama huo huo tena katika eneo zuri zaidi bado wao hawafanikiwi.
Leo ndugu iamuru baraka yako iliyo haki yako ikufuate.
Kuna mabinti anaweza akafanya kila mbinu ili kumpata kijana fulani lakini hafanikiwi lakini wengine hata hawaombi sana ila wanafanya kazi ya MUNGU kwa juhudi lakini hao hao bila kutumia nguvu hata kidogo huchumbiwa na kuolewa huku wengine wakiwa bado.
Leo iamuru baraka yako ikufuate kwa jina la YESU KRISTO.
Iamuru furaha ya ndoa yako irudi.
Iamuru akili yako ya kufaulu masomo irudi.
Iamuru amani na upendo katika familia yenu au ukoo wenu irudi.
Amuru kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Chochote ukitakacho kutoka kwa MUNGU kiamuru leo kikufuate.
Wewe mteule wa MUNGU unayo mamlaka ya kuomba katika jina la YESU KRISTO na baraka ikakufuata.
Kumbuka baraka ya MUNGU ni muhimu sana kwako na baraka hiyo ni tofauti na baraka za kipepo.
Mithali 10:22 '' Baraka ya BWANA hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni nayo.''
Iamuru leo baraka ya MUNGU ikufuate.
Hakikisha tu una uhusiano mzuri na MUNGU.
Hakikika unaishi maisha matakatafu na hakikisha wewe ni mtii kwa MUNGU katika utoaji wa fungu la kumi na sadaka.
Kama ni hivyo basi iamuru baraka yako uitakayo kutoka kwa MUNGU ikufuate.
Inawezekana
Maombi yako ya leo ni muhimu sana.
Isaya 45:2-3 '' Nitakwenda mbele yako, na kupasawazisha mahali palipoparuza; nitavunja vipande vipande milango ya shaba, na kukata-kata mapingo ya chuma; nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni BWANA, nikuitaye kwa jina lako, naam, MUNGU wa Israeli.''
MUNGU naweza kukupa hazina za gizani ambazo wabaya wako walificha ili usipate.
Leo amuru baraka zako zikufuate.
Kupitia maombi yako hakika baraka yako itakufuata kwa jina la YESU KRISTO.
Amuru uponyaji wa mwili wako ukufuate.
Amuru kuwa mzima.
Zaburi 103:3-6 '' Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote, Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema, Aushibisha mema uzee wako, Ujana wako ukarejezwa kama tai; BWANA ndiye afanyaye mambo ya haki, Na hukumu kwa wote wanaoonewa.''
Leo hakikisha unaziandika baraka zako kisha tubu kwa Bwana YESU na anza kuiamuru baraka moja baada ya nyingine ikufuate.
MUNGU akubariki sana sana na pia ukipenda kunisapoti katika huduma yangu nakukaribisha sana kunitumia sadaka yako ya hiari kwa namba yangu ambayo huwa ipo chini ya kila somo lanfu yaani 0714252292, Tuma kutokea Mtandao wowote na itanifikia.
Kwa ushauri na maombezi kwa njia ya siku niandikie sms kwa namba 0714252292 nitakuombea kisha nitakupangia siku ya kukuombea kwa simu na utapata ushindi mkuu wa BWANA YESU. Kama uko nje ya nchi na unatamani kunisapoti katika huduma yangu wasiliana nami kwa namba hiyo au kwa email yangu ambayo nayo huwa ipo chini ya kila somo langu.
MUNGU wa mbinguni akubariki sana na aziamuru baraka zako zote zikufuate leo.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.
0 Comments