AINA/HATUA TATU ZA MAJARIBU UTAKAYOKUTANA NAYO KATIKA MAISHA. MATHAYO 4:1-11..




 AINA/HATUA TATU ZA MAJARIBU UTAKAYOKUTANA NAYO KATIKA MAISHA. MATHAYO 4:1-11..

."Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani,ili ajaribiwe na IBILISI.Akafunga siku arobaini mchana na usiku,mwisho akaona njaa.Mjaribu akamjia akamwambia,Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu,amuru kwamba mawe haya yawe mkate.Naye akajibu akasema,Imeandikw,Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo kinywani mwa Mungu.Kisha ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu ,akamweka juu ya kinara cha hekalu,akamwambia,Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake;Na mikononi mwao watakuchukua;Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.Yesu akamwambia,Tena imeandikwa,Usimjaribu Bwana Mungu wako.Kisha ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno,akamwonyesha milki zote za ulimwengu,na fahari yake,akamwambia, Haya yote nitakupa,ukianguka kunisujudia.Ndipo Yesu alipomwambia,Nenda zako,shetani;kwa maana imeandikwa,Msujudie Bwana Mungu wako,umwabudu yeye peke yake.Kisha ibilisi akamwacha;na tazama,wakaja malaika wakamtumikia. Ndugu zangu ni vema mkajua kuwa,kabla shetani hajakuacha uendelee na maisha yako kuikaribia ndoto na hatima ya maisha yako,uwe na uhakika kwanza atakujaribu katika hatua hizi tatu..Ikiwa unapitia katika jaribu fulani wakati huu,chunguza lipo katika kundi lipi kati ya haya kisha utambue ni majaribu ya kundi lipi kati haya yamesalia ili uje wakati wa kuachwa na shetani ijapokuwa yaweza kuwa kwa muda tu. Umewahi kujiuliza ni kwanini kuna jaribu ni rahisi kulishinda kwa kutumia neno la Mungu na lingine linaonyesha kana kwamba lina asili ya neno la Mungu na kila wakati unapotumia neno kupambana nalo kunakuwepo hali ya mgongano baina ya neno moja na lingine na unabaki kwenye mkanganyo.Kuna ahadi moja inagongana na nyingine,wazo moja linagongana na lingine,neno linagongana na lingine,ufunuo mmoja unagongana na mwingine..ghafla unajikuta ni vigumu kulishinda jaribu hilo kwa kutumia mstari wabiblia. YESU alijikuta katika mazingira ambayo alilazimika kukabiliana na majaribu ya aina tatu katika mazingira yale yale na kwa hakika haikuwa kazi rahisi kama wengi wetu tunavyozani.Shetanj,katika kumjaribu mtu,huleta majaribu katika hatua zifuatazo;

Hatua ya kwanza, JARIBU KWA MUJIBU WA TAMAA YA MTU.

Hii ni hatua ya awali kabisa ya majaribu.Ni aina za majaribu ambayo huwapata watu ambao ni wachanga bado katika imani.Ni majaribu ambayo shetani huyatumia kupima umakini wetu juu ya imani na neno la Mungu.Kabla ya majaribu mengi yote shetani huanza na ya asili hii.Yesu alikuwa pia mtahiniwa katika hili(MATHAYO 4:2-4).. ...mjaribu anamwambia,UKIWA NDIYE MWANA WA MUNGU....GEUZA JIWE KUWA MKATE... Mstari wa pili unasema ....akafunga siku arobaini...MWISHO AKAONA NJAA..
Kulikuwa na uhusiano wa karibu kati ya TAMAA ya Yesu na kile ambacho shetani alimjaribu kwacho yaani njaa.Majaribu haya,shetani huwa anajaribu kuitambua "status" yako kisha kuitumia kukupa ushauri wa kutimiza haja yako.Majaribu haya huwa yanakuwa na namna hii; "Nakujua wewe ni nani lakini pia naijua shida yako" ...Nakujua wewe ni mwana wa Mungu lakini najua pia unanjaa;Nakujua wewe ni mwana wa Mungu lakini najua unashida ya pesa; Nakujua wewe ni mwana wa Mungu lakini huna na unahitaji mke au mume;Nakujua wewe ni mwana wa Mungu lakini unahitaji kazi,nk... Ni majaribu ambayo shida yako inakinzana na identity yako..unajikuta katika mazingira ambayo utii wako juu ya uovu ndio njia pekee ya kutatua tatizo lako ama unashurutishwa kuitumia karama na kipawa alichokupa Mungu kutimiza matakwa yako. Majaribu jinsi hii ni ngumu sana kushinda kwa kutumia utashi na hekima ya kawaida isipokuwa neno la Mungu.Ukikumbuka tu neno sahihi kwa wakati huo unaweza kulikabili jaribu la jinsi hii;Ndio maana awali nilisema kuwa shetani huyatumia majaribu ya aina hii kupima tu umakini wetu juu ya neno la Mungu.Yesu alikabili kwa jibu fupi tu..."IMEANDIKWA....MTU HATAISHI KWA MKATE"... aliposhinda hili kwa neno la Mungu,shetani akamjia na hatua ya pili ya jaribu akiwa na vifungu vya biblia. Hatua ya pili, 

JARIBU KWA MUJIBU WA NENO LA MUNGU. 

Pindi anapoona umakini wako juu ya neno kwa majaribu ya aina hiyo ya awali,shetani huchukua biblia na kuanza kuunda jaribu kwa mujibu wa maandiko.Majaribu ya jinsi hii huwapata watu ambao kwa sehemu wamefanikiwa kuzikabiri tamaa zao kwa ajili ya Kristo.Watu wenye mitazamo ya "kwa ajili ya Yesu nipo tayari kwa lolote" ama "ni heri nife lakini niingie mbinguni" ama "hata nikiwa maskini,mgonjwa,njaa au nimeshiba,katika dhiki na taabu,katika mauti au uzima;Yesu ni yeye yule Jana Leo na milele".Ndugu yangu,kama umefikia hatua ya imani(ya kujikana kwaajili ya Bwana) basi we ni mtahiniwa wa majaribu ya jinsi hii. Ni majaribu ambayo Shetanj naye anakuja na mistari ya biblia kukabiliana na ile uliyonayo moyoni ikupayo imani kwa Mungu..Yesu alikuwa mtahiniwa katika hili(MATHAYO 4:5-7)..IBILISI AKAMCHUKUA MPAKA MJI MTAKATIFU..JUU YA KINARA CHA HEKALU....akamwambia UKIWA NDIWE MWANA WA MUNGU......KWA MAANA IMEANDIKWA... Wakati jaribu la awali likuwa "fanya kwa kuwa unashida", hili la sasa "fanya kwa sababu imeandikwa". Je! Unaweza kugundua tofauti baina yake?..hapa Shetani huwa anachana kabisa na swala,la tamaa zako ni kukujia na maandiko..Majaribu haya yana asili hii... "Ninakujua wewe ni mwana wa Mungu lakini imeandikwa" ...Ninakujua wewe ni mwana wa Mungu lakini imeandikwa utakula mema ya nchi,utakuwa kichwa,akuponya magonjwa yako yote,hakuna tasa katika Israel,mke mwema atoka kwa BWANA;ghafla unajikuta kile unachokijua kwa habari ya Mungu na hali halisi vinakinzana.Kila unapotumia mstari 

mmoja kulikabili jaribu shetani anakuletea mstari mwingine unakuondolea uthabiti wa moyo juu ya ule ulonao.. ...Imeandikwa nitakuwa kichwa na nimefeli,nimeponywa magonjwa na ninaumwa,nitakula mema ya nchi na nimaskini,Bwana kasema nami kuwa ndiye mke wangu na amenikataa,nk.... Katika hili Yesu hakutumia mistari ya kujitetea kama mwanzo ila alimpa shetani tu ukweli kwamba ninajua unanijaribu ili hali unajua kuwa mimi ni nani hivyo basi nakwambia wewe kama walivyoambiwa wenzako...USIMJARIBU BWANA MUNGU WAKO..Majaribu haya unaweza kushinda pale tu utakapopata mstari ambapo unagonga shetani moja kwa moja.Katika haya usiendelee kulumbana na shetani kuhusu ahadi za Mungu.Mtakesha.

Hatua ya tatu, JARIBU KWA MUJIBU WA OFA YA SHETANI KWAKO.

Baada ya kushinda hatua hizo mbili,shetani atakuja kukupa ofa.Hii si kwa habari ya tamaa au neno linavyosema ila zawadi yake kwako ikiwa utafanya matakwa yake.Haya ni majaribu yanayowapata watu waliofanikiwa zaidi kiimani,kihuduma,kiuchumi au kimaisha kwa ujumla.Kimsingi,ni watu wachache sana huwa wanafikia hatua ya kujaribiwa na majaribu ya namna hii kwa kuwa haya ni maalumu kwa ajili ya '"profit maximazation". Ni majaribu ambayo huyatumia shetani kuwaondoa watu katika kusudi la Mungu katika majira ya kulitimiza kusudi.Inahitaji kustahimili mengi kabla ya kufikia hapa.Katika hili shetani huja na mpango wa kukuinua na kukufanikisha zaidi.Si kwa sababu ya tamaa yako au neno linavyosema ila tu kukupa zaidi ya pale ilipofikia.Yesu alikuwa mtahiniwa wa hili(MATHAYO 4:8-10)....IBILISI AKAMCHUKUA...AKAMWONYESHA MILKI ZOTE ZA ULIMWENGU NA FAHARI YAKE...akamwambia,HAYA YOTE NITAKUPA...Utagundua kuwa majaribu haya huwapata watu ambao tayari WAMESHATEMBEA na kuona fahari ya mambo mengi. Wakati jaribu la awali lilikuwa "fanya kwa kuwa unashida", la pili"fanya kwa sababu imeandikwa",hili la sasa "fanya ili nikupe"..naamini unaendelea kuona tofauti ya aina/hatua hizi tatu za majaribu.Katika hili,tamaa zako haziusiki wala neno la Mungu halihusiki.Fanya nikupe ndo habari ya mjini katika hili.Katika hili shetani kisha jua kuwa wewe ni mwana wa Mungu na hana haja ya kutaka umthibitishie.Majaribu haya yana asili hii; "Ukifanya hivi utakuwa zaidi ya ulivyo sasa" ...Ukifanya hivi utaongeza washirika,upako na miujiza katika huduma yako,ukifanya hivi utaongezewa cheo,biashara yako itafanikiwa,utakuwa maarufu zaidi...katika hili si kwamba huna kitu ila kuna ahadi ya kuwa zaidi ya vile ulivyo.Ukishindwa kupambanua roho hii ndo hukawii kujikuta kuzimu kutafuta upako zaidi au kuwa na miujiza feki au kifanya biashara za magendo na rushwa,ufisadi na usaliti huzaliwa katika hili pia.
Kulishinda jaribu hili,ijapokuwa unampaswa bado kuwa na mstari wa kujibu lakini Yesu alichukua hatua ya ziada ya ...NENDA ZAKO SHETANI...kumfukuza shetani.Hata hivyo majibu matatu ya Yesu yalikuwa na Siri fulani. 

1.Mtu hataishi kwa mkate...lilikuwa ni jibu juu ya hoja ya haja au uhitaji wa Yesu(njaa). 

2.Usimjaribu Bwana Mungu...lilikuwa ni kumtiisha shetani juu ya mpango wake. 

3.Msujudie Bwana Mungu wako...lilikuwa ni jibu juu ya hoja ya haja au uhitaji wa shetani(kusujudiwa) 

 Ikiwa unapitia katika jaribu lolote unaweza kujichunguza ili kujua ni aina/hatua gani ya jaribu unapitia ili ikusaidie kujua shetani anatumia hila gani na wewe unaweza kutumia hekima gani ili kushinda.Katika kila jambo kumbuka kamwe hatujaribiwi kupita uwezo wetu na Mungu ni mwaminifu hata kufanya mlango wa kutokea..usisahau KUOMBA NA KUMTEGEMEA MUNGU kwani hata katika maarifa haya niliyokupatia bado neema ya Mungu ni kitu bora zaidi kukupa wokovu.
Neema ya Kristo iwe pamoja nawe.Amen

Post a Comment

0 Comments