KIPIMO KIKUBWA CHA MTU MKAMILIFU NA ASKOFU KAKOBE





NENO LA MSINGI:

YAKOBO 3:2:

“Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. MTU ASIYEJIKWAA KATIKA KUNENA, HUYO NI MTU MKAMILIFU, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu.”

Viko vipimo kadhaa katika Biblia ambavyo tunaweza kujipima ukamilifu wetu, huku tukijilinganisha na mfano wa mtu mkamilifu, Yesu Kristo [ZABURI 37:37]. Kipimo kikubwa kimojawapo cha ukamilifu ni mtu kuweza kuuzuia na kuutawala ulimi; na kuufanya useme yale tu ambayo Yesu mwenyewe angeweza kuyasema. Biblia inasema kwamba, ulimi wa mtu asiye mkamilifu ni ULIMI MOTO NA ULIMWENGU WA UOVU; nao ndio uutiao mwili wote unajisi, na kuuwasha moto mfulizo wa maumbile [YAKOBO 3:6]. Ikiwa watu wengi katika Kanisa la Nyumbani au Kanisa Kuu, ndimi zao ni moto na ulimwengu wa uovu; basi mwili wote yaani Kanisa lote litatiwa unajisi na kuwashwa moto kwa sababu yao. Moto wa ulimi unaweza kuligawanya Kanisa, na kuleta makundi makundi kuondoa upendo kati yetu na kumfanya Roho Mtakatifu awe mbali nasi. Biblia inasema “Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo[YAKOBO 3:10]. Biblia inazidi kutueleza kwamba, mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, dini yake mtu huyo haifai na anajidanganya moyo wake kwamba ni mkristo [YAKOBO 1:26]. Ikiwa tunataka kufahamika kwamba ni wakristo, basi inatubidi tuwe na ndimi zilizo baridi, zinazotoa baraka wakati wote katika Kanisa, na mataifa wanaotuzunguka.

Kwa sababu hiyo, leo katika Kanisa la Nyumbani, tunapenda kujifunza tabia za ulimi moto, ambao ni ulimwengu wa uovu. Kwa kuzifahamu tabia hizi za ulimi moto, utaweza kujua ikiwa ulimi wako ni moto au la! Ikiwa ulimi wako ni moto, basi hujakuwa mtu mkamilifu na Biblia inasema dini yako haifai kitu na unajidanganya moyo wako. Inafaa basi, umwendee leo Yesu Kristo, na kumwomba neema nyingi iliyoko katika damu yake iliyomwagika msalabani; ili uweze kuuzuia ulimi wako kwa hatamu na kuufanya usiwe moto tena, bali uwe baridi utoao baraka. Watu wote katika Kanisa la Nyumbani na Kanisa Kuu, tukiwa na ndimi baridi zinazotoa baraka; tutakuwa ni baraka kwa Kanisa lote la Mungu na Taifa lote, na Utatu wa Mungu utafanya makao kwetu na kujidhihirisha kwetu kwa namna nyingi.

TABIA KUMI ZA ULIMI MOTO, ULIMWENGU WA UOVU:

1. HUSEMA UONGO NA KUSINGIZIA


Ikiwa tunataka kufanya maskani yetu pamoja na BWANA, kusema uongo na kusingizia; hakupaswi KAMWE kuonekana katika ndimi zetu [ZABURI 15:1-3a; MITHALI 25:23; ZABURI 101:5a; ZABURI 101:6-7; MITHALI 19:5,9,22; MITHALI 20:17; WAKOLOSAI 3:9; WAEFESO 4:25]. Ahadi zetu zinazotoka katika ndimi zetu lazima ziwe kweli na amini. Tukimwambia mtu tutakwenda kwake Jumatatu saa 10 jioni lazima iwe kweli hivyo hivyo, isipokuwa tunapokuwa tumepata mambo mazito labda ugonjwa n.k. na hata hapo tutatoa taarifa kabla za kuomba msamaha na kukiri kumkosea mtu yule. Ndiyo yetu lazima iwe ni ndiyo na siyo yetu siyo. Kuvunja ahadi ni kutokumjua Mungu [SOMA HOSEA 4:1-2; 2 WAKORINTHO 1:17-19]. Tunapotoa ahadi na baadaye tunapogundua kuwa ahadi hiyo ni kwa hasara yetu, hata hapo hatupaswi kuyabadili maneno yetu [ZABURI 15:1-2, 4]. Ikiwa hatuna uhakika wa kufanya jambo, basi tusitoe ahadi. Sema kwa mfano “Nitakuja kwako kesho kama nikiweza kumaliza shughuli zangu mapema. Hii ni ahadi yenye masharti ya kutekelezwa kwanza. Ndugu asipokuona, basi atajua kuwa masharti hayo hayakutekelezwa na hutakuwa umesema uongo. Mtu asemaye uongo na kusingizia, mtu huyu ulimi wake ni moto.

2. HUFANYA MIZAHA AU UTANI

Katika Ukristo, hakuna utani au mizaha. Hakuna watani katika wokovu. Utani wa namna yoyote ni kinyume na Ukristo! Mtu wa kabila fulani utamsikia akisema kuwa watu wa kabila fulani ni watani zake na utamsikia akiwatania katika misiba na popote pale. Haya ni mambo ya mataifa au watu ambao hawajaokoka. Ukristo hauna sehemu kabisa ya mizaha na utani. Ulimi unaopenda mizaha au utani, ni ulimi moto, ulimwengu wa uovu [SOMA ZABURI 1:1; MITHALI 26:18-19].

3. HUSENGENYA

Kusengenya ni kumsema mtu vibaya kwa lengo la kumharibia sifa na kutaka aonekane mbaya, hafai na wa kudharauliwa. Kusengenya hufanywa mtu akitajwa wakati yeye hayupo katika mazungumzo hayo. Kusengenyana katika Biblia ndiko kunakotajwa kwamba ni KUUMANA NA KULANA KUNAKOSABABISHA MAANGAMIZO [SOMA WAGALATIA 5:15]. Kusengenyana huangamiza umoja na upendo katika Kanisa na kusababisha makundi makundi. Mtu mwenye ulimi moto ndiye ambaye hupenda kuwasengenya wenzie. Yeye ambaye anayemsengenya jirani yake, hatakwenda kufanya maskani pamoja na Mungu [SOMA ZABURI 15:1, 3; ZABURI 50:19-20, 22]. Wako wengine ambao hawasengenyi, lakini hupenda kuyasikia masengenyo na kuyafurahia. Hawa pia hushiriki dhambi hiyo sawa na wasengenyaji hao. Kusengenya lazima kuwe na sehemu mbili. Anayesengenya na anayepokea masengenyo kwa kuyaruhusu masikio yake kuyasikia na kuyafurahia. Kama hakuna wanaoyapokea masengenyo, basi wasengenyaji watatoweshwa. Ni sawa na mtoa rushwa na mpokea rushwa. Wote hatia yao ni ile ile. Mtu akizungumza na wewe na kumtaja mwingine kwa sifa mbaya, mwambie pale pale mfanye maombi kwa ajili ya ndugu anayetajwa, na mwambie aliyesema sifa hizo aombe mwenyewe.

4. HUSEMA MANENO YA DHARAU

Hatupaswi kudharauliana sisi kwa sisi au kuwadharau mataifa. Yesu angetudharau (maana tulikuwa wachafu na wasiofaa lolote), je, tungekuwa wapi leo? Mtu mwenye ulimi moto, hujaa maneno ya dharau kwa wenzake. Amdharauye mwenzake afanya dhambi [SOMA MITHALI 14:21a].

5. HUSEMA MANENO YA UKAIDI



Huutumia ulimi wake kuwaambia wenzake kwamba hamjali Kiongozi, na kuwashawishi wenzie wamuone Kiongozi wao mbaya na hafai. Huutumia ulimi wake kusema hawezi kufuata maneno ya Mungu katika jambo fulani, na kuwashawishi wengine kuasi. Mtu mwenye ulimi wa ukaidi kwa kiongozi wake wa Kanisa, mume wake, boss wake kazini n.k. huyu ana ulimi moto. Ukaidi ni chukizo kubwa kwa BWANA na ni ulimwengu wa uovu [SOMA MITHALI 3:32].

6. HUKASIRIKA NA KUTOA MANENO YA HASIRA


Mtu mwenye ulimi moto, hukasirishwa na mambo madogo madogo tu na kuzira kila kitu. Mtu wa jinsi hii hawezi kukaa na watu kwa amani. Wakati wote yeye ni kununa tu na kutafuta ugomvi. Hasira ya namna hii siyo sehemu ya ukristo. Hasira ya jinsi hii huzaa ugomvi na dhambi nyingi. Hatupaswi kuiruhusu hasira kuutawala ulimi [MHUBIRI 7:9; MITHALI 22:24-25; WAKOLOSAI 3:7-8; YAKOBO 1:19-20]. Tunapaswa kumkasirikia shetani tu anayewatesa na kuwatumikisha ndugu zetu katika dhambi, na hasira yetu katika hilo, itatusukuma kuomba zaidi, kutoa mali zetu zaidi na kuhubiri Injili zaidi kuikemea dhambi. Huku ndiko kuwa na hasira bila kutenda dhambi [WAEFESO 4:26].

7. HUSEMA MANENO MENGI WAKATI WOTE

Mkristo hazungumzi ili kuhakikisha ukimya unatoweka pale alipo! Kabla ya mkristo kuzungumza, anayaangalia maneno atakayoyasema kwamba yatakuwa ya kuwapa neema na kuwafaa wale watakaoyasikia [WAEFESO 4:29; WAKOLOSAI 4:6]. Mtu mwenye maneno mengi wakati wote, LAZIMA atakuwa ANAISHI KATIKA DHAMBI. [SOMA MITHALI 10:19]. Katika maneno mengi wakati wote, kunakuwa na kuongeza chumvi na kupamba ripoti au taarifa ili watu wafurahi au wacheke, Kuongeza chumvi huku, ni kusema uongo na ni dhambi iliyo mtego mkubwa kwa watu wengi wanaosema “Bwana Asifiwe”. Mtu mwenye maneno mengi, wakati wote anapenda azungumze yeye tu, tena kwa sauti kubwa ili asikiwe mbali, ulimi wake ni moto na ulimwengu wa uovu.

8. HUSEMA MANENO YA KIBURI NA MAJIVUNO

Mtu mwenye ulimi moto, husema maneno ya kiburi na majivuno. “Pasipo mimi kwaya haiwezi kuimba, lazima mnijali sana au siyo sitaimba”. “Kanisa zima hakuna mwalimu kama mimi au anayeijua Biblia kama mimi”. “Kanisa zima mimi ndiye msichana mzuri ninayeangaliwa na kutamaniwa na kila mvulana”. “Nyumba yangu ni nzuri kuliko zote za kwenu”. “Nimesoma kuliko kila mtu hapa”. “Hakuna mfanyakazi kama mimi kati yenu”. “Hakuna mwombaji kama mimi, ninyi wote ni wavivu tu”. Maneno yoyote ya kiburi na majivuno yanayofanana na haya siyo sehemu ya ukristo. Ulimo moto hujivuna na kunena kwa kiburi. Kumcha BWANA, NI KUCHUKIA KIBURI NA MAJIVUNO [SOMA MITHALI 8:13].

9. HUSEMA MANENO YA FITINA, UCHONGEZI, WIVU NA KUTETA KWA LUGHA YA KABILA WASIOIELEWA WANAOSIKIA

Ulimi moto, hujaa wivu, fitina na uchongezi. Mtu mmoja mwenye ulimi moto anapoutumia kunena maneno ya wivu, fitina na uchongezi, huweza kuliwasha moto Kanisa la Nyumbani na hata Kanisa Kuu lote [SOMA 2 WAKORINTHO 12:20] Mkiwa wawili au watatu wa kabila fulani katikati ya wengine wa kabila jingine, haiwapasi kutumia lugha ya kabila lenu kuzungumza na kuwaacha wengineo hawaelewi lolote. Ni ulimi moto unaotenda hayo. Ulimi baridi hujenga, kufariji, na kuwatia moyo watu wote, mahali pote; na kuwafaa wahitaji wote. Siyo vibaya kusema lugha ya kabila lenu, mnapokuwa ni ninyi peke yenu. Anapokuwepo asiye wa kabila lenu, semeni Kiswahili ili yeye naye ajengwe.

10. HUHESABU MABAYA TU

Ulimi baridi, wakati wote huhesabu mema ya mwenzie na kuyataja hayo wakati wote. Ulimi baridi huyapuuza na kutokuyahesabu matendo mabaya aliyoyatenda mtu ambaye alikwisha omba msamaha. Mtu mwenye ulimi moto, humsema mwenzie na kumhesabia mabaya tu wakati wote kana kwamba hafanyi jema hata moja. Mtu mwenye ulimi moto hamsifu mwenzake katika lolote wala kutafakari mema aliyoyafanya, bali huorodhesha mabaya aliyoyafanya mwenzie moja baada ya jingine. Ulimi wa upendo hauhesabu mabaya [1 WAKORINTHO 13:56]. Mtu mwenye ulimi baridi, anapowazungumza wenzie wakati wote huyataja yale waliyoyafanya yenye sifa njema, yenye staha, yenye wema, yenye sifa nzuri, yaliyo safi na ya haki na kuyatafakari hayo [SOMA WAFILIPI 4:8].

Hizi ndizo tabia kumi za ulimi moto, ulimwengu wa uovu. Itakuwa ni baraka ya ajabu Kanisa lote likiwa na watu wenye ulimi baridi. Anza leo kuuzuia ulimi wako kwa hatamu katika Jina la Yesu na kuufanya baridi. Ukimwomba Mungu, na kuchukua hatua, hakuna lisilowezekana kwa Mungu. Atakubadilisha leo na utakuwa na ndimi wenye baraka na siyo ule unaolaani [SOMA YAKOBO 3:10-12]. Ukikizuia kinywa chako na ulimi wako hivyo, utajilinda nafsi yako na taabu [SOMA MITHALI 21:23].

Post a Comment

0 Comments