MAMBO YA MSINGI KUJUA KUHUSU IMANI



Na: Patrick Sanga

Waraka wa Juni

Katika Waebrania 11:1   Biblia inasema “Basi imani ni kuwa na hakika na mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana”.

Katika somo hili mpenzi msomaji nataka kukuonyesha mambo kadhaa ya msingi unayopaswa kujua kuhusu imani, ili imani yako iweze kuongezeka na kuwa imara. Katika kukuonyesha mambo haya ya msingi nitakupitisha katika habari ambayo Yesu pamoja na wanafunzi wake walikuwa wakivuka bahari na safari ikiwa inaendelea dhoruba ikajitokeza. Habari hii imeandikwa katika Injili za  Mathayo, Marko na Luka pia. Mimi nitanukuu yale ya Mathayo kama mwongozo kwa somo hili.
Biblia inasema “Akapanda chomboni wanafunzi wake wakamfuata. Kukawa msukomsuko mkuu baharini, hata chombo kikafunikizwa na mawimbi; naye alikuwa amelala usingizi. Wanafunzi wake wakamwendea wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunangamia. Akawaambia mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu, Wale watu wakamaka wakisema, Huyu mtu ni wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?” (Mathayo 8:23-27).

 Jambo la kwanza; Imani ipo katika viwango mbalimbali vinavyopimika.

Mfano huu wa Yesu unatusaidia kujua kwamba kumbe imani ipo katika viwango mbalimbali, mfano imani ndogo na kubwa. Ni wazi kwamba imani ndogo/haba haiwezi kutengeneza jibu la mahitaji yako.
Katika habari hii usalama wale wanafunzi ulitegemea kiwango cha imani yao. Yesu akijua hilo ndio maana aliwauliza mbona mmekuwa waoga enyi wenye imani haba? Ile kusema imani haba ina maana kiwango cha ile imani yao kisingeweza kuleta matokeo yaliyokusudiwa, kwa kuwa kilikuwa kidogo. Na hivyo tunajua kwamba kumbe imani inaweza kuongezeka au kupungua.

Jambo la pili; Unaweza ukawa na Yesu na usiamini kwamba anaweza kukusaidia.

Ukweli huu tunaupata baada ya kusoma habari hii kama ilivyoandikwa katika Marko 4:36-41. Ule mstari wa arobaini unasema ‘Akawaambia, mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?
Ni imani yangu kwamba Yesu aliwauliza swali hili huku ndani yake akijaribu kufikiri sababu ya wanafunzi kushindwa kunyamazisha ile dhoruba. Si kana kwamba wanafunzi wa Yesu hawakumuamini yeye kabisa. La hasha, walimwamini ndio maana waliacha kazi zao na familia zao kumfuata Yesu.
Imani ambayo wanafunzi waliikosa ni ile ya Yesu kuweza kuwaokoa na dhoruba iliyokuwa inawakabili. Ndivyo ilivyo hata leo, licha ya maelfu ya watu kumwamini Yesu kama Bwana na mwokozi wao, wengi hawana imani naye kwamba anaweza kuwaponya magonjwa yao, ndoa zao, familia zao, nchi zao nk au jaribu lolote mfano wa hili la wanafunzi.

Jambo la tatu; Unaweza kuwa na imani lakini ipo pengine na si kwa Yesu.

Naam ukweli huu unathibitika baada ya kusoma habari hii katika kitabu cha Luka 8:22-25. Ule mstari wa ishirini na tano unasema ‘Akawaambia, imani yenu iko wapi? Wakaogopa, wakamaka, wakisema wao kwa wao, Ni nani huyu basi hata anamuru pepo na maji, navyo vyamtii?
Kwa mujibu wa Luka, Yesu alitambua kwamba imani ya wanafunzi wake haikuwa kwake bali mahali pengine. Na ndiyo maana aliwauliza iko wapi imani yenu? Kwa lugha nyingine aliwaambia najua imani mnayo, lakini haipo kwangu.
Imani ya wale wanafunzi ilikuwa katika uzoefu na akili zao katika kuendesha zile mashua. Wao walifikiri kupitia uzoefu na ujanja wao wangeshinda. Kwa hiyo waliamini katika uweza wao binafsi, naam imani ambayo haikuwasaidia pia.

 Jambo la nne; Imani inaweza kuhamishika tegemeana na nini unasikia

Kwa mujibu wa Warumi 10:17, chanzo cha imani ni kusikia. Imani katika Kristo inakuja kwa kusikia habari za Kristo, imani kwa Shetani inakuja kwa kusikia habari za Shetani nk. Kwa hiyo mtu mwenye imani katika Kristo imani yake inaweza kuhama kutoka kwa Yesu kwenda kwa Shetani tegemeana na ameruhusu nafsi yake kusikia na kutafakari vitu gani. Jambo hili ndilo lililowatokea Adam na Hawa katika bustani ya Edeni (Mwanzo 3:1-8).
Ili imani yako isihamishike jenga mazingira ya kusikia na kusoma neno la Mungu ukitafakari kila iitwapo leo. Naam kwa mapato yako yote jipatie ufahamu wa neno la Kristo. Hakikisha unaongeza imani yako katika kila eneo ambalo unajua imani yako imepungua au ipo kwa kiwango kidogo.

Mambo zaidi ya kujifunza;
  • Hofu/mashaka/woga/kusitasita ndio maadui za imani. Usiruhusu mambo haya yakazuia jibu la maombi yako (Waebrania 10:38, Marko 11:22). Kumbuka Mungu si mwanadamu hata aseme uongo, maadam ameahidi katika neno lake atatenda tu.
  • Unapokuwa katika jaribu/changamoto haupaswi kuutazama ukubwa wa jaribu bali udumu ukiamini kile ambacho Mungu amesema kwa habari ya eneo ambalo unalipitia (Yohana 3;14, Hesabu 21:4-9).
  • Jizoeze kufanya tathmini ya kiwango cha imani yako kwa kuangalia kama kinatosheleza kutatua changamoto (jaribu) unazozipitia au la. Angalia imani yako ipo wapi na kwa nani?. Ukigundua imepungua (Mathayo17:20) basi ongeza, kama ipo pahala pengine nje ya Yesu irejeshe kwa Yesu na si mwandamu au uwezo na nguvu zako. Maandiko yako wazi kabisa ,kwamba, sisi hatuwezi kufanya neno/jambo lolote bila Yesu (Yohana 15:5).
 Utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili Bwana kuaminiwa na utadumu kuaminiwa.
Mungu awabariki

Post a Comment

0 Comments