AINA ZA UPENDO.
1. UPENDO AGAPE - UPENDO WA MUNGU. (Godly Love)
Agape ni aina ya upendo wa ki-Mungu, utendao kazi
ndani ya mtu pasipo masharti yoyote au sababu yoyote. Ni upendo usioangalia
hali ya nje ya mtu. Ni nguvu au uwezo wa
mvuto wa Ki-Mungu utendao kazi ndani ya mtu, kumwonyesha mtu mwingine wema wa
Mungu bila kujali hali yake yoyote. Ni upendo usio na sababu yoyote; unampenda
mtu kwasababu tu unatakiwa kumpenda, nukta. Hakuna sababu nyingine. Kwa
kingereza wanasema unconditional love.
Aina hii ya upendo; agape, ni kama ule
aliotuonyesha Mungu kwa kuupenda. Neno la Mungu linasema ‘Mungu alitupenda
tungali wenye dhambi’ (Rum 5:8) ili atuokoe na mauti itokanayo na uasi kwa
Mungu. Imeandikwa katika biblia kwamba Mungu aliupenda ulimwengu wenye kila
aina ya uovu, uasi na uchafu (Yoh 3:16, Rum 1:28-32) na akamtoka Kristo afe kwa
ajili yetu, ili tuokolewe. Kwahiyo, alitupenda bila kujali uchafu na uasi
tuliokuwa nao. Huo ndio upendo wa agape.
Mfano; Upendo wa Msamaria mwema. (Luka 10:29-37)
Msamaria mmoja alimkuta mtu mmoja asiyemfahamu,
ameanguka barabarani kwasababu amepigwa ma majambazi. Huyu Msamaria aliamua
kumsaidia huyu mhanga kwa kumsafisha vidonda vyake na kuchukua katika punda
wake na kumpeleka katika nyumba ya wagonjwa na sii hivyo tu, bali alijitolea
hata kumlipia gharama za matibabu, huu mtu asiyemjua kabisa. Huu ndio upendo wa
ki-Mumgu ndani ya mtu. Hauangalii hali ya nje wala hauna masharti; bali mtu
huamua kuuachilia tu kwa mtu, kawasababu Mungu ameumimina ndani yake kwa ajili
ya mtu/watu wengine.
Lakini tunasoma kuwa, kabla ya huyu Msamaria kupita
pale njiani na kumwuoka huyu mhanga, walipita watu wengine wawili ambao
wanaaminika kuwa ni watumishi wa Mungu. Kwanza alipita kuhani wa Mungu, lakini
hakutaka kumsaidia, labda kwasababu hamjui. Neno linasema, alijipitisha kando
akaenda zak bila kumsaidia. Kisha akapita Mlawi, amabye pia ni mtumishi wa
Mungu, lakini naye pia alijipitisha kando kabisa, akaenda zake bila kutoa
msaada kwa huyu mtu, kwasababu tu ni mtu asiyemfahamu. Pamoja na udini
waliokuwa nao, tunasoma kuwa, hawakuweza kumsaidia huyu mtu aliyejeruhiwa
vibaya na majambazi. Ni aidha, hawakuwa kabisa na upendo agape ndani yao, au hawakuuachilia upendo agape utoke, uhudumie mtu.
Lakini cha kushangaza, akaja Msamaria (amabye ni
mtu wa kabila lisilohesabika kuwa la wacha Mungu) ndiye aliyeweza kuuruhusu
upendo wa Mungu wa agape umhudumie
yule mhanga wa ujambazi japo hamjui kabisa. Akamsafisha viWale watumishi wa
Mungu walishindwa kuuruhusu upendo agape
kutoka ndani yao, kumhudumia huyu mhanga. Hawa watumishi wa Mungu tuliowasoma,
walitawaliwa na upendo wenye masharti na unaoangalia kwanza hali ya nje ya mtu.
Upendo agape hautakiwii kuangalia
hali ya nje ya mtu, wala hautakiwi kuwa na masharti yoyote. Ni upendo wa Mungu
mwenyewe alitumiminia mioyoni mwetu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu (Rum 5:8)
Sifa kuu tatu (3) za Upendo wa ki-Mungu (Agape).
i.
Hauangalii hali ya mtu
ya nje.
ii.
Hauna masharti yoyote
ya kupenda.
iii.
Hauna kipimo au
kiwango cha kupenda.
iv.
Hauna mwisho au kikomo
cha kupenda.
2. UPENDO PHILEO – UPENDO WA KIRAFIKI. (Friendship
Love)
Phileo ni upendo wa kirafiki. Huu ni pendo tofauti kidogo
na upendo wa agape. Phileo ni upendo
wenye sababu. Kiingereza wanasema ‘congitional
love’. Ni upendo wenye sababu. Huu ndio upendo unaokuwepo kati ya marafiki.
Phileo ni upendo unaoshikiliwa na
kishikizo/kifungo cha ‘masharti’ fulani au ‘sababu’ fulani. Mtu huwa rafiki wa mtu fulani ‘kwasababu’
fulani. Kuna mazingra yamewafanya watu fulani kuwa marafiki. Mazingira hayo au
mashrti fulani yakivunjika kati yao, basi upendo ulio kati yao huyeyuka na
urafiki wao huvunjika.
Aina hii ya upendo wa phileo ni kama ile ambayo Yesu anaisema katika kitabu cha Yohana
14:21,23. Anasema kwamba ‘mtu akinipenda,
Baba atampenda, nami na Baba tutakuja kufanya makoa ndani yake’. Huu ni upendo
tofauti na ule unaotajwa katika Yohana 3:16 na Warumi 5:8 ambao unasema Mungu alitupenda tungali wenye dhambi pasipo
masharti yoyote. Yaani, kwa upendo agape,
Mungu hakujali hali zetu za nje wala masharti yoyote. Lakini kwa upendo phileo, Mungu anaangalia kwanza kama
mtu atatimiza masharti aliyoyaweka, kisha ndipo na yeye Mungu anaachilia upendo phileo kwa mtu huyo, anakuwa rafiki yake.
Mahali pengine Yesu alisema kwa wanafunzi wake kuwa
‘siwaiti ninyi tena watumwa bali
marafiki.’ Hilo neno ‘tena’
linamaanisha kwamba, baada ya kukaa na wanafunzi wake kwa muda fulani, waliweza
kufikia kiwango Fulani cha mashati
alichokitaka Bwana, hata sasa wamefika katika ngazi wa kuwa marafiki wa Yesu na
sio watumwa tena. Ndio maana imeandikwa pia katika kitabu cha Mithali 8:17
kuwa, ‘ninawapenda wale wanipendao …’ Hivyo phileo
ni upendo wenye masharti na sababu.
Rafiki wa mtu husema ‘nampenda mtu Fulani, rafiki yangu kwasababu …’
Labda kwasababu wanasoma wote au kwasababu alimsaidia katika eneo fulani au
kwasababu anatabia fulani au kwasababu wanatoka kijiji kimoja, n.k.
Mfano; Urafiki wa Jonathan na Daudi. (1Samweli
18:1-4)
Tunaona Jonathan anampenda sana Daudi baada ya
kugundua vipawa vilivyo ndani ya Daudi. Tunasoma kwamba Daudi alikuwa anajua
sana kupiga muziki (zeze) na kuimba zaburi kwa Mungu, kitu kilichofanya Daudi
awe karibu sana na Mungu na kufunikwa na utukufu wa Mungu (upako). Hivyo
Jonathan alimpenda sana Daudi kwasababu
Daudi ana upako, uliomsaidia babake (mfalme) Sauli kufunguka kutoka katika
nguvu za giza mara kwa mara. Hivyo Daudi akawa mtu wa msaada sana kwa familia
ya Mfalme na katika serikali yake. Pasipo Daudi kuwepo karibu, mambo yote ya
ofisi ya Mfalme na nyumba yake yanaharibika. Hicho kilimfanya Jonathan kumpenda
sana sana Daudi. Na Daudi naye akampenda sana Jonathan kwasababu Jonathan
alimpenda yeye kwanza, na pia kwasababu Jonathan alikuwa motto wa mkuu wan
nchi, mtoto wa Mfalme. Kukajengeka upendo mkubwa sana wa kirafiki kati ya Daudi
na Jonathan, upendo Phileo. Hivyo, Phileo ni upendo wenye sababu au
masharti.
Mfano Mwingine; Urafiki wa Yesu na Lazaro, Mariam
na Martha. (Yohana 11:5, 35-36)
Japo biblia haielezi wazi wazi sababu za urafiki wao, lakini maandiko yanaonyesha wazi kuwa, uhusiano
wa Yesu na kina Lazaro, Martha na Mariam, ulikuwa wa karibu sana ingawa
hawakuwa ndugu zake wala wanatimu wake, bali marafiki zake. Angalia
inavyoelezwa katika msatri wa 5; Neno la Mungu linasema, 5Naye Yesu
alimpenda Martha na umbu lake (dada yake, ambaye ni Mariam) na Lazaro (kaka
yao). Hebu jiulize, kwanini Roho Mtakatifu alimwongoza Yohana kutanguliza
kumuandika Martha kwanza, kabla ya Lazaro au Mariam? Hii ni wazi kwamba, Yesu
alikuwa na uhusiano wa kirafiki, tena wa karibu sana na hii familia, na hasa
Martha (nionavyo mimi, kulingana na maandiko). Tuangalie zaidi mazingira haya
kama ilivyoandikwa.
Yohana 11:20; Martha aliposikia kwamba hatimaye
Yesu amefika msibani japo kwa kuchelewa, alikwenda kumlaki (kumpokea) lakini
Mariam hakutoka, alibaki ndani. Unadhani kwanini? Baada ya kuongea na Yesu kwa
muda Fulani, ndipo tunamona Mariam akiamua kwenda kmwuita na Mariam, atoke
ndani kwenda kumsalimia Yesu (mstari wa 28-32) Hii inaonyesha ukaribu
uliokuwepo kati ya Yesu na Martha. Walikuwa na upendo mkubwa sana wa kirafiki, Phileo. Wasomaji wa Biblia nakumbuka
hata wakati Yesu alipotembelea familia yao siku moja, ni Martha aliyeonyesha
kumjali Yesu sana hata kujituma jikoni ili kumuandalia chakula, wakati Mariam
hakuwa hata na pressure, bali
alijiketisha miguuni pa Yesu kusikiliza Neno la Mungu. Japo badaye Martha
alishushuliwa na Yesu, lakini ndiye aliyeonyesha kumjali (kum-care) Yesu zaidi, ndiye aliyeonyesha
kusumbuka kwa ajili ya Yesu zaidi kuliko Mariam. Soma hii katika kitabu cha
Luka 10:38-42.
Mimi naamini urafiki wa Martha kwa Yesu alijengeka
katika mazingira ya Martha kuthamini wema na baraka alizotendewa na Yesu,
kwasababu utakumbuka kwamba, Martha ndiye yule mwanamke kahaba, ambaye siku
moja alisikia injili katika mkutano ambao Yesu alikuwa anahubiri na akatubu
dhambi zake, akatua mzigo wake na Yesu akamsamehewa kabisa uovu wake wote. Kwa
furaha aliyokuwa nayo, akaenda nyumbani kwake, akachukua chupa ya perfume (marhamu) safi tena ya bei
kubwa, akaja mahali ambapo Yesu alialikwa chakulani nyumbani kwa Farisayo
aitwaye Simon.
Kwa utaratibu wa kiyahudi, ni mwiko kabisa mwanamke
kuingia katika kikao cha wanaume wala kumgusa mwanaume bila utaratibu. Lakini
kwa jinsi alivyokuwa na msukumo mkubwa moyoni, alishindwa kujizuia, akapenya
mpaka mahali walipokuwa wamekaa chakulani, akasimama nyuma ya Yesu, akadondosha
machozi katika miguu ya Yesu (kwasababu wayahudi hukaa chini kwenye zulia, na
hii ina maana kwamba, Yesu alikuwa amekunja miguu kwa nyuma, ndio maana machozi
yakamwangukia miguuni). Ndipo alipoinama
na kuvunja ile ya marhamu safi, nyumba yote ikajaa harufu nzuri. Martha
akaipaka miguu ya Yesu mafuta yale mazuri, akachukua nywele zake ndefu na
kuipangusa vizuuuri miguu ya Yesu. Mwisho akamalizia kwa kuibusu sana miguu ya
Yesu mpaka mafarisayo wakakwazika na kunung’unika; lakini Yesu akamtetea Martha
na kusema ‘mwacheni! Huyu amesamehewa dhambi nyingi kuliko ninyi, ndio maana amenipenda zaidi sana kuliko ninyi wote.
Kwa habari kamili, soma Luka 7:36-50.
Pengine kwa sababu ya unyenyekevu wa Martha, ndipo
upendo wa kirafiki (phileo) ulipozaliwa
kati ya Yesu na Martha. Tunasoma hatimaye siku nyingine, Martha akamualika Yesu
chakulani nyumbani kwao (Luka 10:38-42). Kitendo hicho kilimtabulisha Yesu kwa
familia ya Lazaro. Biblia inasema Yesu akawapenda sana Martha, Mariam na Lazaro
kirafiki - phileo (Yoh 11:1-5). Baada
ya hapo, ndipo Lazaro alipougua sana hata Martha akatuma watu kwa Yesu kumwomba
aje kumponya kaka yao ambaye pia ni rafiki sana wa Yesu. Mpaka Lazaro anakufa,
Yesu alikuwa hajatokea.
Siku Yesu anafika, walikuwa wameshamzika Lazaro
siku nne zilizopita, tayari ananuka, ameharibika. Habari ziliposikika kwamba
Yesu amefika msibani, ni Martha peke yake aliyetoka kwenda kumlaki Yesu. Baada
ya muda Martha kuongea na Yesu kwa muda, ndipo akrudi ndani kwenda kumwita
Mariam atoke kwenda kumsalimia Yesu kule nje. Mariam akatoka, naye alipomwona
Yesu, alilia kwa uchungu sana na kujibwaga miguu pa yesu na kulalama ‘Yesu kama
ungeuja mapema, kaka yetu asingekufa, ungemponya’. Yesu alipomwona Mariam
analia, na wayahudi waliofuatana naye wanalia, Yesu akaugua sana moyoni,
akafadhaika, na mstari wa 35 unasema “Yesu akalia machozi”. Hata wayahudi
walipomuona Yesu analia, waksema, “angalia jinsi alivyompenda (Lazaro)”. Hii
inaonyesha kwamba, kulikuwa na upendo mkubwa sana wa kirafiki kati ya Yesu na
Lazaro na dada zake. Baada ya hayo, tunasoma Yesu akaenda kumfufua rafiki yake
Lazaro kutoka mautini.
Ndipo katika sura inayofuata (Yoh 12:1-8) baada ya
wakati fulani kupita tangu Yesu amfufue Lazaro, tunaona familia ya Lazaro
wanamwandalia Yesu karamu (sherehe au party), pengine ilikuwa ni ibada ya
shukurani ya kufufuka kwa Lazaro. Siku hiyo, Martha akaanda chakula kizuri,
halafu wote wakiwa wameketi chakulani, Martha akarudia tena kumvunjia Yesu
kibweta cha marashi safi, kumbuka hii ni mara ya pili anamfanyia Yesu tendo
hili la upendo. Martha akamvunjia
Yesu kibweta kingine cha marashi (perfume) safi ya bei kubwa; akampaka tena
Yesu marhamu safi kwa nywele zake. Ilikuwa ni ratili ya mafuta safi ya marhamu
yenye thamani nyingi. Safari hii Yuda ndiye aliyekwazika (soma mwenyewe utajua
sababu). Lakini tunamwona Yesu akimtetea tena Martha na kusema ‘mwacheni, kwa
kitendo hiki, ananiandaa kwa maziko yangu’. Hii inatuonyesha jinsi Yesu
alivyokuwa na urafiki wa Karibu sana na Martha. Martha alimpenda sana Yesu kwa
wema usioelezeka, ambao Yesu alimtendea yeye na familia yake. Upendo uliokuwa
katika yao ni upendo phileo, Upendo
wa kirafiki, upendo wenye sababu.
Sifa kuu tatu (3) za Upendo wa kirafiki (Phileo).
i.
Unaangalii hali ya mtu
ya nje.
ii.
Una masharti yoyote ya
kupenda.
iii.
Una kiwango au kipimo
cha kupenda.
iv.
Una mwisho au kikomo
cha kupenda.
3.
UPENDO EROS – UPENDO
WA KIMAPENZI AU MAHABA. (Romantic/Sexual
Love)
Eros ni upendo wa kimapenzi au kimahaba unaokuwa kati ya
watu fulani kusababisha watu hao kuwa na uhusiano wa kimapenzi (mahaba) kati
yao. Kwa utaratibu wa Mungu na jamii zilizo ‘sawa sawa’, Eros ni aina ya upendo unaotakiwa kuwa kati ya watu wenye
uhusiano wa ki-ndoa, yaani mtu mke na mume au kati ya watu wanaoelekea katika
uhusiano wa ki-ndoa wa mume na mke. Aina zote za upendo zinahusisha moyo
(nafsi) wa mtu, lakini Eros huwa na
sifa ya kuwa na hisia zenye nguvu zaidi toka moyoni kuliko aina zingine zote za
upendo. Eros ni aina ya upendo wenye nguvu kali sana ya
hisia za binadamu.
Tunaona Neno la Mungu (katika kitabu chake maalum
kinachohusu mahaba ya wapenzi wawili)
kitabu cha Wimbo Ulio Bora 8:6, Neno
la Mungu linasema kwamba Upendo (Eros) huwa na nguvu sana, kama mauti. Nguvu hiyo ya upendo
huunganisha nafsi (fikra,hisia na maamuzi) za wapenzi wawili kuwa kitu kimoja
katika fikra, hisia na maamuzi yao kwasababu ni upendo uliolenga kujenga ndoa
nzuri na familia bora.
Mfano; Upendo wa Yakobo kwa Raheli. (Mwanzo
29:10-30)
Yakobo alipomkimbia kaka yake Esau, alikimbilia
nchi ya mbali, nchi ya mama yake, kwa mjoba wake Labani. Labani alikuwa na
binti wawili, mkubwa aliitwa Lea na mdogo waliitwa Raheli. Biblia inasema Lea
alikuwa na macho mazito, yaani ukimwangalia, utadhani amelala, kumbe ndio
anakuona. Na Raheli alikuwa na umbo zuri la mwili na sura nzuri ya usoni. Na
Biblia inasema kwamba, Yakobo alimpenda Raheli. (Mwa 29:16-20). Labani
akamwabia Yakobo atumike kuchunga wanyama wake kwa miaka saba (kama mahari),
ndipo atampa Raheli kuwa mke wake. Yakobo akapendezwa na hilo, na akakubali
kutumika na kuchapa kazi za Labani kwa miaka saba ili ampate Raheli. Na Neno la
Mungu linasema, kwa jinsi Yakobo alivyompenda Raheli (kwa Eros - kimapenzi kuwa mke wake), alichapa kazi sana na kwa bidii
kiasi kwamba, ile miaka saba ilionekana michache sana.
Hiyo ni nguvu ya upendo Eros. Yakobo alikamatwa katika upendo eros kwa Raheli. Ilikuwa kali sana. Nakwambia eros ina uwezo wa kumfanya mtu asione ugumu wa kazi, asione
machungu, asione umbali wa mwendo, asione ukali wa jua, asione aibu wala woga mbele
za watu wengine; Eros ina nguvu sana
juu ya mtu mwenye nayo, hata kuwatala utu wake wote. Eros ina nguvu ya fikra, hata kutawala mawazo ya mtu; eros ina nguvu ya hisia, hata kutawala
kuhisi/kujisikia kwa mtu; eros ina
nguvu ya maamuzi, hata kutawala matendo ya mtu kabisa. Unaweza ukamkuta kijana
sik hizi ni msaaaafi kuliko tunavyomjua, kumbe ni kwasababu tayari amekamatwa
kwa mwanamwali binti ‘Labani’ kama Yakobo aliyodakwa. Wee acha bwana!
Tehetehetehetehe (kicheko).
Yakobo alijaa Raheli katika mawazo yake yote! Kila saa alibaki kumuwaza Raheli kwa muda mrefu;
Yakobo alijaa Raheli katika hisia
zake kiasi cha kutousikia machungu ya ile kazi na hata akaona miaka saba kwa si
kitu kikubwa; Yakobo alijaa Raheli katika maamuzi
yake hata kumfanya afanye kazi kwa nguvu kama trekta au katapila, ili tu
kumpata Raheli. Raheli ndiye aliyekuwa nguvu na hamasa ya Yakobo kudamka
alfajiri na mapema kwenda kulisha mifugo ya mjomba wake Labani.Upendo Eros una nguvu kama mauti aisee. Wee
acha tu.
Upendo wa kimapenzi au mahaba - Eros. (Romantic Love or Sexual Love)
Upendo wa kimapenzi huwa kati ya watu wawili
wanaoelekea katika uhusiano wa kudumu wa mume na mke. Mungu hakukusudia upendo
huu wa kimapenzi uwe wa kujaribu na kuacha, kwasababu eros ni upendo wenye nguvu sana ya hisia (nafsi), hivyo huathiri
sana moyo, ufahamu, hisia za mtu na pengine hata afya ya mwili wa mtu kabisa,
kama hatajua namna ya kuutawala ipasavyo. Hivyo Eros si upendo wa kuingia na kutoka utakavyo, kama mtu abadilishaye
nguo (labda kama kuna cha kujifunza; nitaeleza baadaye maana yah ii sentensi),
bali eros ni upendo uliokusudiwa
kukaa kati ya watu wawili tu, kwa maisha yao yote yaliyobaki hapa duniani
(permanently for life), sio kuingia na kutoka, kwasababu una uwez wa kujeruhi
sana myo wa mtu na kumwachia vidonda na makovu ya moyoni. Tena nasisitiza, eros ni kwa ajili ya watu wawili tu, na
sio watatu au zaidi, laa sivyo huo hautakuwa upendo, bali tamaa (lust and not
love). Na tena eros, ni upendo kwa
ajili ya watu wawili wa jinsia tofauti tu, na sio jinsia moja.
Mfano; Upendo wa Isaka kwa mkewe Rebecca. (Mwa
26:1-11)
Isaka alikuwa akiishi katika nchi ya Wafilisti.
Watu wale wakamwona Rebeka, wakavutiwa na uzuri wake, hata wakamtamani.
Wakamuuliza Isaka, ‘ee bwana ee, huyu msichana tunayemwona katika boma lako na
wakati mwingine unaambatana naye, ni nani kwako? Isaka akaogopa kusema ni mke
wake, kwa maana wangeweza kumuua ili wamchukue Rebeka, kwa jinsi alivyokuwa
mzuri wa kuvutia. Isaka akasema ‘ni dada yangu’. Basi wakamwacha. Lakini kumbe
wale watu walitumwa na Mfalme Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, ili kupeleleza na
kujua uhusiano wao, kwasababu Mfalme alivutiwa sana na uzuri wa Rebeka, akataka
kumuao.
Siku moja, Mfalme Abimeleki alipokuwa akipta pita
mitaani, akakatiza mtaa ambao nyumba ya Isaka ilikuwepo. Biblia inasema “8Abimeleki Mfalme akachungulia
dirishani, akawona Isaka akicheza-cheza na Rebeka mkewe”
(kimahaba/romantically). Mfalme Abimeleki akamwita Isaka, akamwambia, kwa jinsi
nilivyowaona mnchezeana vile, haaaaata! lazima huyu ni mkeo, huwezi
kucheza-cheza vile na dadako, sasaaaa, mbona uliniambia kuwa huyu ni ndugu yako
(dadako)? Isaka akajibu ‘niliogopa nisije nikauwawa kwa ajili yake’. Basi
Abimeleki akamlaumu Isaka, kwa kusema, mtu mmoja wetu angelala na Rebeka bila
kufikiri ni mkeo, kwasababu ulisema mwenyewe ni dadako. Ndipo Mfalme akaamuru
watu wote wasimguse Isaka wala mkewe Rebeka; akasema “11amgusaye mtu
huyu au mkewe, lazima atauawa”.
Baadhi ya Dalili na Sifa za Upendo wa Kimapenzi
(mahaba) - Eros (Romantic Love).
1) Mvuto kwa Haiba yake na kuchukuliana nayo.
(Mwonekano na tabia).
2) Kukaa mawazoni kwa mtu anayependa. (Kujaa moyoni)
3) Shauku kubwa ya kuwa pamoja kila wakati.
(Kuambatana)
4) Heshima kubwa kwa mtu apendwae (Utii na Uaminifu)
5) Kumjali na kumtanguliza mtu apendwae. (Kipaumbele)
6) Zawadi na gharama kwa mtu apemdwae.
(Kujitoa/Sacrifice)
7) Furaha na Amani kutawala moyoni. (Kuridhika)
Baadhi ya maandiko yanayotaja upendo eros. (Upendo wa kimapenzi)
(Waefeso 5:25.) Enyi waume, wapendeni wake zenu kama Kristo alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa
ajili yake. (Mhubiri 9:8-9.) 8Mavazi yako yawe meupe siku zote; wala
kichwa chako kisikose marhamu. 9Uishi kwa furaha pamoja na mke
umpendaye, siku zote za maisha yako ya ubatili uliyopewa chini ya jua. (Wimbo
Ulio Bora 7:1-10) 10Mimi ni wake mpendwa
(mpenzi) wangu na shauku yake ni juu yangu. (Wimbo Ulio Bora 4:1-7) 1Tazama,
u mzuri mpenzi wangu, u mzuri, macho yako…nywele zako… 7Mpenzi wangu
u mzuri pia, wala ndani yako hamna hila.
4.
UPENDO STORGE – UPENDO
WA KIFAMILIA. (Family Love)
Upendo storge
ni upendo wa kifamilia, ni upendo unaotokana na damu moja ya undugu. Ndugu wa
damu moja hata kama hawapatani au wemegombana, bado ndani yao kuna upendo wa
kindugu. Fikiria; mtu na mdogo wake wakiwa wamegombana sana na kutupiana mito
ya makochi na vitabu vyote vya kwenye shelfu za kabati, baadaye, mmoja akimkuta
ndugu yake anaonewa au anagombana au anapigwa na muuza machungwa wa mtaani,
huyu ndugu yake kwa vyovyote ataguswa tu, ataonyesha kujali tu au anaweza hata
kuweka tofauti zao pembeni na kuingilia kumsaidia. Msukumo huo au mvuto huo, ni
mvuto unaotokana na viini vya upendo wa kifamilia unaowafungamanisha watu wa
damu ya familia moja au ukoo mmoja.
Mfano; Upendo wa Musa kwa Mwebrania mwenzake. (Kutoka
2:11-12)
Musa aliona mwebrania mwenzake akipigwa na mmrisri.
Kwasababu na yeye alikuwa mwembrania, ndani yake kukachemka mvuto wa kindugu,
kuliwaka moto wa upendo wa kifamilia. Akainuka na kwenda kumpigania. Musa
akamuua yule mmisri na akamwokoa yule mwebrania. Japo hawajazaliwa tumbo moja,
lakini waote wana damu za kiebrania, na viini vile vya asili yao,
viliwafungamanisha katika pendo la kindugu (kifamilia) hata wakasaidiana.
Upendo huo ulimnyima Musa kujikausha wakati ndugu yake anaonewa, anapigwa na
anataka kuuwawa. Si ajabu wakati anayatazama yale maonezi kwa mbali, hata
alipojidai kuondoka bila kumsaidia, yamkini miguu yake ilishindwa kutembea,
nafsi yake ikakamatwa kurudi kumsaidia ndugu yake. Hiyo ni nguvu ya upendo
storge, upendo wa kindugu.
Mfano; Upendo wa Baba kwa Mwana mpotevu. (Luka
15:11-32)
Tunasoma jinsi mwana huyu mdogo wa baba tajiri
alivyoomba sehemu ya urithi wake na kutokomea nchi za mbali kwenda kutafuta
maisha. Lakini maandiko yanaeleza jinsi alivyovutwa na dunia na kuharibu mtaji
wake wote wa mali alizopewa na babaye.neno la Mungu linasema, kijana huyu
alijiingiza katika anasa za dunia na mwishowe alifilisika kabisa. Baada ya muda
wa mahangaiko alipata kibarua cha kulisha nguruwe wa mtu mmoja. Hali yake ya
kimaisha ilikuwa mbaya sana hata akatamani kula chakula cha nguruwe. Lakini
akili zikamrudia na akaona anateseka bure wakati kule kwao, baba yake ana
watumishi wanaokula vizuri kuliko yeye. Ndipo alipoamua kurudi nyumbani kwa
toba. Kwa hali ya mzazi wa kawaida, huyu kijana angepewa adhabu kali sana;
lakini kinyume chake, baba yake mzazi alimpokea kwa shangwe na furaha. Akamvika
na mavazi mazuri, akamchinjia na ng’ombe mnono na kumfanyia sherehe kuuuubwa ya
kufana. Hiyo ni nguvu ya upendo wa kindugu. Japo alichofanya si cha kupendeza,
lakini nguvu ya upendo wa kindugu unaweza kufunika uovu wooooote uliotendwa na
ndugu yenu. Watu wanaweza kuamua kusamehe au kufumbia macho makosa yaliyotendwa
na ndugu yao kwasababu ya nguvu ya upendo wa kindugu, unaitwa kwa kiebraia storge.
Upendo wa kindugu, storge unafanana kwa sehemu
na ule upendo wa ki-Mungu wa agape.
i.
Hauangalii hali ya nje
ya mtu.
ii.
Hauna masharti ya
kupendwa.
iii.
Hauna kikomo au mwisho
wa kupendwa.
Tofauti yake moja kubwa na upendo wa agape ni kwamba, upendo wa kindugu una kiwango au kipimo cho
kupenda. Ndugu wanapendana lakini kwa viwango tofauti; upendo wao haulingani.
Tofauti ningine kubwa ni kwamba, kwasababu huu upendo wa kindugu unatokana na binadamu, basi ni lazima hautakosa madhaifu
mengi. Ingawa ndugu wanaweza kuwekeana masharti fulani fulani ya kitabia ili
kuweka uelewano kati yao, hata masharti hayo yakivunjwa, na baadhi ya ndugu
wakasema wamefika mwisho, hawataki tena kumsaidia, lakini mwishoni, baada ya
hasira kutulia na muda kupita, utaona ndugu wanainuka, wanajikongoja, kwenda
kumsaidia tu ndugu yao. Hiyo ndiyo nguvu ya upendo wa kindugu au kifamilia.
NAMNA YA KUPATA MWENZI MZURI WA MAISHA.
(HOW TO FIND/GET A GOOD MARRIAGE PARTNER)
*Mithali 19:14, 21
1. Mweleze Mungu vizuri, zile haja za moyo wako. (*Fil
4:6-7)
Mungu ameahidi kuwa atakupa mtu wa kufanana na wewe
(Mwa 2:18). Kwa hiyo ni muhmusana ujijue wewe ukoje, kisha ndipo utaweza
kumweleza Mungu na kumwomba akupe mtu wa haja ya moyo wako. Hivyo ni muhiu sana
kujijua, kujitambua na kujielewa kwa jinsi ulivyo na ni aina gain ya watu ambao
wewe unaendana nao (mnaiva). Hii ni kwasababu, watu tuko tofauti. Unaweza
kuishi na mtu yoyote duniani, lakini hutaweza kuishi vizuri na kila mtu. Maisha mazuri yanakuja kwa kukutana na mtu ambaye mnaelewana na
mnaendana. Ndio maana Mungu alimwambia Adam kwamba, mwenzi wako wa maisha,
atafanana na wewe.
Usimfiche Mungu moyo wako. Kumbuka, yeye ni Baba
yetu na sisi tu watoto wake vipenzi. Hivyo Mungu anaheshimu sana haja za moo
wako ambazo zitakupa wewe furaha ya maisha. Mathayo 7:7-11 inasema, Ombeni
nanyi mtapewa. Mwana akiomba mkate, hapewi jiwe, akiomba samaki, hapewi nyoka.
Anapewa alichoomba. Lakini pia ni muhimu ujue kwamba, mwana akiomba mkate,
hapewi jiwe, lakini pia hapewi keki hata kama ndani ya nyumba kuna keki. Mwana
akiomba samaki, hapewi nyoka, lakini pia hapewi kuku, hata kama ndani ya nyumba
kuna kuku wengi. Hii ni kwasababu, Mungu anaheshimu sana matakwa na mahitaji ya
watoto wake, maana anapenda kuiona furaha ya watoto wake. Soma Zab 145:17-18 na
Isa 45:11 uone. Pia 1Kor 7:39.
Maombi yako ya bidii yatampa Mungu kumchonga,
kumuandaa. Kila mtu huumbwa na Mungu vizuri, lakini Neno linasema kwamba,
dhambi iliharibu utaratibu mwingi sana wa Mungu duniani. Soma Mwa 6:5-8 na Rum
1:28-32. Dhambi imevuruga mambo mengi sana, nafsi za watu wengi ziko corrupted
(zimeharibiwa na kuvurugwa) na dhambi. kwahiyo, maombi yako yatamfanya Mungu
kuanza kumshughulikia na kumtengeneza huyo mwenzi wako, popote alipo duniani.
Na Biblia inasema kwamba, maombi ya mwenye haki yanafaa sana, mt akiomba kwa
bidii. Soma Yak :16, Luk 18:1,
Kol 4:2.
2. Mwombe Mungu akuonyeshe au akukutanishe na mwenzi
wako. (*Yer 33:3)
Kila mmoja wetu ambaye Mungu amempangia kuwa na
mwenzi, ana mwenzi huyo mahali Fulani hapa duniani. Pointi ya kwanza inahusu
kufanya maombi ya kumwmba Mungu kumchonga na kumfinyanga huyo mwenzi wako
popote alipo. Point hii ya pili inahusu kumwomba Mungu kusababisha mazingira
ambayo yatawakutanisha na mtatambuana baada ya kupata ufahamu wa Mungu kwamba ‘you
belong together’ yaani mnaendana, mnafanana, mnafaana na hivyo mnaweza kuishi
pamoja vizuri. Hiyo ndiyo maana halisi ya kufunuliwa au kuonyeshwa. Japo Mungu
anaweza kukupa maono katika ndoto au katika maombi, lakini si lazima iwe hivyo.
Si kila mtu anaweza kupata maono kuhusu mwenzi wake. Soma Efe 1:15-19, Zab
32:8, Isa 43:26, Isa 45:11
3. Tengeneza marafiki. (*Mith 18:24, Mith 17:17)
Watu weng humwomba Mungu kwa uaminifu sana ili
wapate mwenzi wa maisha. Lakini wanfanya makosa ya kujifungia katika kisiwa cha
upekee. Ni ngumu sana kuonekana na kujulikana tabia na utu wako wa ndani kama
hutachangamana na jumuiya za marafiki. Mungu ndiye chanzo cha urafiki. Hat Yesu
alikuwa na marafiki wa kiume na waki kike pia. (Yoh 11:5). Jithidi kufanya marafiki mvalimbali ila
mwombe Mungu akupe marafiki wazuri.
Kuna aina nyingi za marafiki; Kuna arafiki wa mbali
(peer friends), marafiki wa kawaida (casual friends), marafiki wa karibu (close
friends or best friends) na marafiki wa moyoni (intimate friends). Unaweza ukawa
na marafiki wa kawaida wengi uwezavyo, haina shida. Lakini unahitaji marafiki
wa karibu wachache (Mith 18:24). Katika wingu kubwa la marafiki zako, Mungu
ataanza kukuongoza nawe utawachuja na kuwaweka katika ngazi hizo mbalimbali.
Katika hali ya kawaida, Mungu atakukutanisha na mwenzi wako wa maisha kati ya
marafiki zako na watu unaofahamiana nao. Kwa maombi unayofanya, Mungu
atasababisha mkutane, mfahamiane, mtambuane na mptane.
4. Thibitisha moyo wako kwamba unampenda kikweli. (*Mhubiri 9:8-9a)
Kadri unavyoendelea na maisha ya uaminifu katika
wokovu, maombi, kujifunza neno la Mungu na kumtumikia Mungu kwa namna
mbalimbali, Mungu atasababisha ukutane na mtu anayefanana sana na haja za moyo
wako kuhusu mwenzi wa maisha. Utahitaji usikivu mkubwa wa rohoni ili kuambua ni
aina gani ya upendo unaingia moyoni mwako kuelekea kwake (kwasababu kuna aina
nne za upendo). Upendo wa Mungu, Upendo wa Kindugu, Upendo wa Kirafiki, Upendo
wa Kimapenzi (mahaba).
Katika ya watu unaofahmiana nao, yupo mmoja ambaye
atakuwa wa tofauti sana ndani yako. Mungu atampa kuonekana watofauti sana
kuliko wengine wote wanaokuzunguka. Hivyo kabla ya kwenda kusema naye na
kumshirikisha uonavyo wewe moyoni mwako, thibitisha kimaombi tena na tena kwamba ndani yako kuna upendo wa kweli kwa
ajli yake. Mk 5:25 – (30) – 34; inasema,
wengi walimgusa Yesu na kumsukuma-sukuma, lakini ni mmoja tu ambaye atakuwa na
mguso wa tofauti katika moyo wako.
ISHARA
ZA KUTAMBUA (UPENDO WA) PENZI LA KWELI.
1.
Mtu huyo atakamata umakini wako na atakuvutia (attention).
2.
Atajaa moyoni na mwazoni mwako kuliko kawaida na
wengine.
3.
Utatamani sana uwepo wake wakati wote (kuwa
naye).
4.
Utapenda kuwasiliana naye mara kwa mara (kama
hamko wote).
5.
Utakuwa na moyo wa kumjali, wema, zawadi na
kujitoa sana kwa ajili yake.
6.
Utakuwa na heshima ya juu sana, adabu, utii na
uaminifu sana kwake.
7.
Utakuwa na maneno mazuri, maneno laini, na maneno
ya upendo kwake.
8.
Utakuwa na moyo/uwezo wa kumvumilia au
kuchukuliana naye vile alivyo.
9.
Utakuwa na hamu ya kumgusa au kumshika kwa upendo
(si tamaa).
10.
Utakuwa na moyo na utayari wa kumlinda na
kumhifadhi.
11.
Uhusiano wenu
utapendeza mbele za watu wengi (si lazima wote)
12.
Utakuwa na amani na furaha ya ajabu moyoni
mwako/mwenu.
Mungu alisema kwa mkono wa Mtume Paulo kuuelezea
Upendo kwa namna hii;
1 Cor 13 : 4-8(a)
*
Upendo
huvumilia/subira (Love is patient)
*
Upendo
hufadhili/hufanya wema (Love is kind)
*
Upendo hauna husuda
(Love doesn’t Envy)
*
Upendo haujivuni (Love
is not proud)
*
Upendo haukosi adabu
(Love is not rude)
*
Upendo hauna ubinafsi
(Love is not selfish)
*
Upendo hauna uchungu
(Love is not easily angered)
*
Upendo hauhesabu
mabaya (Love doesn’t count wrongs)
*
Upendo haufurahii uovu
(Love doesn’t rejoice with evil)
*
Upendo hufurahia
ukweli (Love rejoices in truth)
*
Upendo unalinda (love
always protects)
*
Upendo huamini yote
(Love always trusts)
*
Upendo hutumaini (Love
always hopes)
*
Upendo hustahimili
(Love always perseveres)
5. Omba
ushauri kwa watu wanaokujua/wanaomjua huyo umpendaye.
2Kor 13:1; Zab 73:24; Mith 15:22
Ushauri kutoka kwa watu werevu wanaomjua Mungu na
wanaowajua ninyi wawili utakuhibitishia kwamba ulichsikia mooni juu ya huyo mtu
ni sahihi. Wakati mwingi (si wakati wote) watu wa pembeni huwa na uwezo wa
kuona vizuri zaidi mambo kuliko watu mlio ndani. Wanaweza kuona vitu ambavyo
ninyi mlio ndani ya urafiki hamuoni bado.washauri wanaweza kutumiwa na Mungu
kuthibitisha mawazo uliyo nayo na mipango uliyonayo. Mashauri ya watu yanaweza
kukusaidia kufanya maamuzi magumu nay a muhimu. (Math 18:16; 1Tim 5:19;
Ebr 10:28)
Mwombe Mungu akuongoze kwa watu wazuri wenye hekina
watakaokushauri. Lakini la muhimu kuliko vyote ni wewe mhusika kubaki na uamuzi
wa mwisho. Washauri wabaki washauri na sii waamuzi; wewe ndiwe uwe mwamuzi wa
mwisho. Ni muhimu kupima ushauri wote unaopewa kwa maombi na uongozi wa Mungu.
Wakati mwingine, Mungu anaweza kukuongoza kitu ambacho hakuna mtu mwingine
anakiona ukionavyo wewe. Neno la Mungu linasema, amani ya Kristo itakusaidia
kufanya maamuzi mazuri.
Soma; Fil 4:6-7, Kol 3:15 na Isa 55:12
6. Mwendee
na Useme naye kwa hekima. (*Wimbo
3:1-4)
Baada ya maombi na subira, Mungu akuongoze kusema
naye kwa wakati utakaoongozwa na Mungu. Uwe jasiri na muwazi. Lakini usemi wako
uwe wa kawaida (simple). Usichague maneno magumu wala misamiati wala mafumbo.
Uwe wazi na wa kawaida. Usitumie maneno ya kiroho saaaaana ili kumtisha au
kumfunga mtoto wa watu. Kwa mfano; usitumie maneno kama, ‘Mungu ameniambia’ au
‘Asema Bwana wa majeshi’ maneno kama haya, yanamfunga mtu kusema “ndiyo” (kama
atashitushwa nayo na kuogopa) lakini kama ni mtu jasiri na
hajakupenda/hajakukubali, mtapambana. Huo sasa si mwelekeo mzuri.
Kijana mmoja alipoataliwa, akaanza kuporomosha
maneno makali mfano ‘nakuzungushia ukuta wa moto, hutaolewa na mtu mwingine ila
mimi, na ukikataa, Bwana atakutandika’. Hii si hekima ya Mungu. Mungu hatumii
nguvu bwana. Ikiwa kwenda mbinguni tuu, Mungu halazimishi watu, Je itakuwa
ndoa? Wewe ukishasema mameno rahisi; Kwa mfano; ‘nimeomba kwa muda, na hivi
ndivyo ninavyosikia moyoni mwangu kwamba, nakupenda sana, na ikiwa itampendeza
Mungu na wewe pia, basi uwe mwenzi wangu wamaisha’. Ukishamwambia maneno hayo
rahisi (au yanayofanana na hayo) amini kwamba kama ni mpango wa Mungu muwe wote
maishani, maombi yako na neema ya Mungu vitamsaidia kufanya uamuzi mzuri kwa
ajili yenu wawili. Unaweza kupata jibu la ‘ndiyo’ au ‘hapana’ au ‘subiri’. Mtu
wa Mungu huongozwa na Mungu, halazimishi wala hakasiriki ovyo kwa kitu kama
hiki. Maana yangu ni kwamba, hauhitaji kutumia nguu ya mwili wala akili (kuwaza
sana). Baada ya kuongea na kutua mzigo wako kwake, pumzika naumwachie Mungu
kumalizia kazi.
Mkumbuke Mariam mama wa Yesu, japo alijua ana
mchumba, lakini malaika aliposema naye kuhusu kupata ujauzito kabla ya ndoa,
hakukurupuka mbio kwenda kwa Yusufu na kuanza kumwelesha, bali alimwachia Mungu
kuongea na Yusufu. Mimi binafsi naamini Mariam alimwombea sana Yusufu. Lakini
kwasababu ulikiwa mpango wa Mungu wa kuwa pamoja maishani, Mungu hakuongea na
Mariam peke yake; aliongea na Yusifu pia. Mungu ni Mungu wa utaratibu,
usimfundishe kazi. Jifunze kupumzika ndani ya Mungu na kutokuwa na wasiwasi.
Huko ndiko kukua kiroho. Amani ya Kristo ikuhifadhi.
7.
Thibitisha uhusiano wako/wenu (kiofisi).
(*Wimbo 3:4)
Baada ya kuongea na kulitafakari pamoja kwa muda
mtakaoona unatosha au unafaa, ni muhimu sana sasa mpelekane mbele, katika
mamlaka zenu za kifamilia na kikanisa. Uhusiano mzuri usiwe wa mafichoni.
Tunaona huyu mpenzi katika kitabu cha Wimbo anasema, anataka kumtafuta mpenzi
wake, amshike mkono, wapelekane kwa wazazi. Huo ndio utaratibu mzuri kibiblia.
Familia na kanisa watawasaidia kufuata taratibu za kiutamaduni na kiroho ili
mhalalishwe kuwa mume na mke. Ndipo ndugu na marafiki mtawashirikisha mipango
yote ili kuandaa harusi na makazi.
0 Comments