NGUVU ZA KUVUKIA
HATUA NYINGINE
“Hata Danieli,
alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani
mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili
Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za
Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo” (Danieli 6:10).
Maisha ni safari
ambamo kuna mambo mengi. Sio mara zote mambo yatakuwa mazuri na mepesi. Hata
kama unampenda Mungu sana na umeamua kuishi maisha ya kumpendeza siku zote,
kuna mapito imekupasa kupita. Uwe makini.
BWANA akijua hayo
alisema, “ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; Mimi nimeushinda
ulimwengu” (Yohana 16:33). Yeye alishinda, ndio maana amekuwa “hakimu wa haki”
kwa maana katika mambo YOTE naye alijaribiwa kama sisi, akashinda (Waebrania
2:17,18). Unapopita katika magumu, jua BWANA naye alipita. Unapokutana na
Ibilisi ana kwa ana, jua BWANA naye alikutana na Ibilisi ana kwa ana, tena
nyikani (Luka 4:1-13). Jipe moyo, utashinda.
Zingatia jambo
hili, kama BWANA alimwambia Petro, mwanafunzi wake ampendaye, “nenda nyuma
yangu Shetani” (Mathayo 16:23), kwa sababu ya kauli yake; yaani Petro alitumiwa
na Ibilisi wakati huo; imekupasa kujua kwamba, watu wengi walio KARIBU nawe
ndio WATAKAOTUMIWA na Ibilisi kukujaribu wewe. Kwa kupitia watu wako wa karibu,
utakutana na Ibilisi ana kwa ana! Lile NENO walilitamka masikioni mwako
litakujaribu. Je! Utasema UMESABABISHIWA na mtu kufanya ufanyayo? Hukujua
unajaribiwa?
Angalia jambo
hili, Danieli alipoPITA mahali pa kujaribiwa, kwa NENO la wale watu wake wa
karibu kazini [alipokuwa mkuu wa maliwali wa Babeli], hakupambana nao, aliomba
mara 3 kwa siku, kama ilivyokuwa destuiri yake. Sasa ona hapa, watu wengi
wanapenda kuwa WASHINDI kama Danieli, lakini hawapendi au hawafanyi kama
Danieli. Je! Nguvu za Danieli za kuvuka VIKWAZO vyake alipata wapi? Jifunze
maisha ya MAOMBI ya Danieli.
Jiulize sasa, Je!
Kiwango chako cha maombi ulicho nacho sasa kinaweza KUKUVUSHA unakopita? Je!
Kiwango “hicho” kinaweza kukuinua hatua zingine za mafanikio? Jipangie kwa
KUAMUA na KUDHAMIRIA kuongeza kiwango chako cha maombi; Mwombe Mungu akusaidie
katika nia hiyo. Nakuahidi kwamba haitakuwa rahisi, ila kadri unavyoweka nia na
kuanza kuchukua hatua, utaweza kuomba zaidi kuliko mwanzo, nawe utaona
utakavyovuka hatua zako kwa ushindi.
Huwezi kuona
mahali pameandikwa “Ibilisi akaja kumjaribu Danieli”, lakini nakwambia leo,
wale watu aliokutana nao ana kwa ana, kwa kupitia hao, Danieli alikutana ana
kwa ana na Ibilisi. Kwa bahati mbaya sana, Ibilisi amepita kwa mke/mume wako
hukujua; amepita kwa watoto wako hukujua; amepita kwa wafanyakazi wenzako
hukujua; nk. Sasa umebaki na LAWAMA na UCHUNGU na watu, hukujua Adui yako ni
MWEREVU kuliko wanyama wote wa walioumbwa! Ubebaki kusema, “kama sio mke/mume
wangu nisingefanya haya”, “Fulani ndio amesababisha hata nikawa hivi nilivyo”,
“kama sio fulani ningekuwa mbali kiroho”, nk.
UJINGA ukutoke kwa
jina la Yesu, utamtwika mwanadamu lawama hata lini na kumwacha Adui yako ali
akistarehe bila kuguswa? Utamfanyaje mwanadamu kuwajibika kwa makosa na dhambi
zako? Je! hukupaswa kusimama kwanza wewe ili kuwasaidia na wengine?
Shughulika na
adui; achana na watu. Hii ni sawa na kulaumu BOMBA kwa sababu hakuna maji.
Wengi wa hao unaowalaumu ni kama mabomba tu; aliyekugusa na kukujaribu ni
Ibilisi. Shughulika na Ibilisi; hiyo ndio siri ya ushindi wako. Na, Nguvu zako
utazipata katika maombi.
Frank P. Seth
0 Comments