MCHUNGAJI KIONGOZI JOSEPHAT GWAJIMA
Basi vizazi vyote tangu
Ibrahimu hata Daudi ni vizazi kumi na vinne; na tangu Daudi hata ule uhamisho
wa Babeli ni vizazi kumi na vinne; na tangu ule uhamisho wa Babeli hata Kristo
ni vizazi kumi na vinne.” Mathayo 1:17
“Yekonia alikuwa na umri wa
miaka kumi na minane alipoanza kutawala; akatawala miezi mitatu katika
Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani wa
Yerusalemu. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, mfano wa yote aliyoyafanya
baba yake. Wakati ule watumishi wa
Nebukadreza mfalme wa Babeli
wakakwea kwenda Yerusalemu, na mji ukahusuriwa. Na Nebukadreza, mfalme wa
Babeli, akaufikilia huo mji, hapo watumishi wake walipokuwa wakiuhusuru. Na
Yekonia, mfalme wa Yuda, akatoka akamwendea mfalme wa Babeli, yeye na mama yake,
na watumishi wake, na wakuu wa watu wake, na maakida wake; mfalme wa Babeli
akamchukua mateka katika mwaka wa nane wa kutawala kwake. Akatoa huko hazina
zote za nyumba ya Bwana, na hazina za nyumba ya mfalme, akavikata-kata vyombo
vyote vya dhahabu ambavyo Sulemani,
mfalme wa Israeli, alivifanya katika hekalu la Bwana, kama Bwana alivyosema. Akawachukua
mateka watu wa Yerusalemu wote pia, na wakuu wote, na mashujaa wote, watu elfu
kumi; na mafundi wote, na wafua chuma wote; hapana mtu aliyebaki, ila waliokuwa
wanyonge wa watu wa nchi.” 2Wafalme 24:8 – 14
Mfalme
wa Israel wakati ule alikuwa anaitwa Yekonia na alitawala miezi mitatu na
kumtenda Mungu dhambi, naye Mungu akaruhusu mfalme wa Babeli aende kwa mfalme
wa Israeli na kuitawala Israel. Kumbe katika utawala, mtawala haihitaji muda
mrefu sana ili kuharibu mambo; vivyo hivyo kwenye wokovu, mtu haihiitaji kuwa
kwenye wokovu muda mrefu ili amkosoe Mungu. Tunaona Mfalme Yekonia alitawala
miezi mitatu tu na kisha kumtenda Mungu dhambi. Pia tunaona Mungu alipoziona
dhambi za Yekonia akaliachia taifa adui la Babeli kulivamia taifa la Israel.
Unapokuwa dhambini Mungu ataruhusu adui zako wakupige na hakika watakushinda. Hakuna ushindi katika dhambi. Na Mfalme Yekonia alilitambua vema jambo hili.
Kwa
kutambua hilo, Yekonia akaamua kujisalimisha kwa mfalme Nebukadreza yeye pamoja
na mama yake, baraza lake la mawaziri, maakida pamoja na watu wengine muhimu
katika nchi wakiwemo matajiri wote. Pia, mfalme Nebukadreza alichukua vitu vya
thamani kutoka katika hekalu la Bwana ikiwa ni pamoja na sanduku la agano.
Akachukua majeshi, mafundi, wenye akili wote na wafua chuma ili wakaujenge
ufalme wa Babeli.
Mfalme
Yekonia alijisalimisha kwa kuwa alijua atashindwa vita kwa sababu ya hali yake
mbaya kiroho, yaani dhambi. Imeandikwa,
“Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama
vile roho yako ifanikiwavyo.” 3 Yohana 1:2
Hali yako ya kiroho ikiwa imefanikiwa, “ukiwa hauna
dhambi” mambo mengine ya mwilini yatafanikiwa vivyo hivyo. Mfalme wa Babeli
hapa ni alama ya shetani. Shetani huwa ana kawaida ya kuwachukua wale watu
wenye akili, uwezo na nguvu popote aingiapo na kuondoka nao. Yawezekana ni
katika nchi au hata familia. Hujawahi kusikia msibani watu wakisema, “ni heri
angekufa fulani na si huyu.” Kuna msemo kuwa watu wazuri huwa hawadumu. Kwa
nini? Shetani anajua kuwa watu wa namna hii ni hatari kwa ufalme wake ndio
maana anajitahidi kuwafanya mateka mapema wawe misukule au wadhaifu kwa namna
ambayo hawatakuwa tishio kwake tena.
“Kabla sijakuumba katika
tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii
wa mataifa.” Yeremia 1:5
Kabla hujazaliwa Mungu tayari
alikuwa na mpango na maisha yako kwamba utakapokuja duniani, uje kuujenga
ufalme wa Mungu. Hivyo akakuwekea uwezesho wa namna fulani ambayo leo tunauita
nyota ya mtu. Yaweza kuwa ni nyota katika biashara, masomo, utawala au nyota ya
kupendwa na kuubalika. Nyota yako ilipokuwa inashuka kuingia kwenye tumbo la
mama yako, shetani pia aliiona. Ndio maana kuna watu matatizo yao yalianza
tangu wakiwa tumboni. Shetani anajaribu kuharibu ule mpango wa Mungu juu ya
mtu. Lakini Mungu wetu ni Mungu aokoaye, ni pale tunapokuwa tumejitenga naye
kwa dhambi zetu ndipo tunapompa mwanya wa kutufanya mateka.
Imeandikwa,
“Mungu
ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”
Yohana4:24
Mungu ni roho na kilichozaliwa
na roho ni roho na huushinda ulimwengu. Tunamwita Mungu Baba kwasababu ya Roho
zetu. Sisi sio miili, bali ni roho zilizotoka juu mbinguni na kuvaa miili.
Biblia inasema atokaye juu yu juu ya yote hata mauti. Kama kuna kitu cha
kipuuzi na cha kijinga tena kisicho na thamani hapa duniani basi kitu hicho ni
mwili wa mwanadamu. Miili mingine ya wanyama kama kuku, ng’ombe, mbuzi
inapokufa inaweza kutunzwa na kutumika baadae kama chakula au manufaa mengine.
Lakini mwili wa mwanadamu unapokufa hauna thamani ni wa kutupa tu. Wanadamu
wamejiwekea utaratibu wa namna ya kuutupa mwili ambao wanauita mazishi. Lakini
ukweli ni kwamba wanachokuwa wanafanya ni kuutupa mwili husika. Roho zetu ndizo
zenye thamani maana hizo hazifi hata milele. Kama sio Yesu, mwili wako hauna
thamani kabisa. Paulo alijua hili ndio maana akasema, “Kwa maana si mimi
ninayeishi bali Kristo aliye ndani yangu, kufa ni faida na kuishi ni Kristo.
Imeandikwa,
“Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye
aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka
mautini kuingia uzimani.” Yohana 5:24
“Mimi
nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu,
kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu;
bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa
ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Kama vile
ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni.”
Yohana 17: 14
Mfalme Yekonia hakuwa mjinga
bali mtu mwenye hekima. Alipokubali kujisalimisha kwa Mfalme Nebukadreza
alikuwa akiwaza ni heri wapelekwe uhamishoni kuliko kuipoteza nchi kabisa. Japo
nchi ilibaki na watu wadhaifu tu, alikuwa anajua katika viuno vyake kulikuwa na
mtoto ambaye ndiye angewatoa uhamishoni hawa wana wa Israel waliopelekwa
uhamishoni.
“Na
baada ya ule uhamisho wa Babeli, Yekonia akamzaa Shealtieli; Shealtieli akamzaa
Zerubabeli; Zerubabeli akamzaa Abihudi; Abihudi akamzaa Eliakimu; Eliakimu
akamzaa Azori; Azori akamzaa Sadoki; Sadoki akamzaa Akimu; Akimu akamzaa
Eliudi; Eliudi akamzaa Eleazari; Eleazari akamzaa Matani; Matani akamzaa
Yakobo; Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa YESU aitwaye Kristo.”
Mathayo 1:12
Leo kanisa limehamishwa kwenye
ulimwengu wa kiroho kiasi cha kutoamini uweza na nguvu za Mungu. Tumehamishwa
kwenye miji ya kiroho ya uharibifu, tupo mashimoni. Lakini tumebweteka na
kuridhika kukaa huku uhamishoni. Tumelima mashamba na bustani, tumeoa na
kuolewa huku uhamishoni na pia tumezaa tukiwa uhamishoni. Ni wakati wa kutambua
kuwa pamoja na mashamba na bustani tulizotengeneza lakini tuko uhamishoni na
yatupasa kurudi kwenye asili yetu.
“Bwana
amekufanya kuhani badala ya Yehoyada, kuhani, ili mpate kuwa watumishi katika
nyumba ya Bwana, kwa kila mtu aliye na wazimu, na kwa kila mtu ajifanyaye kuwa
nabii, umtie katika mkatale na pingu. Mbona, basi, hukumkemea Yeremia wa
Anathothi, ajifanyaye kuwa nabii kwenu, ambaye
ametuma watu kwetu katika Babeli, kusema, Uhamisho huu ni wa siku nyingi;
jengeni nyumba, mkakae ndani yake; pandeni bustani, mkale matunda yake.”
Ezekieli 29: 26
Kwenye ulimwengu wa rohoni
kuna miji ya kiroho kabisa ambayo mtu ambaye ni roho anaweza kuchukuliwa na
kupelekwa huko. Miji hiyo ina nyumba, magari na kila kitu kama ilivyo kwenye
ulimwengu huu. Iko miji ya kiroho ya Mungu ambayo ina nuru kuu inayoangazwa na
Yesu mwenyewe.
“Msifadhaike
mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna
makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi
mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili
nilipo mimi, nanyi mwepo. Nami niendako mwaijua njia.” Yohana 14:1
“Na
ukuta wa mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na katika ile misingi majina
kumi na mawili ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo. 23 Na mji ule
hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na
taa yake ni Mwana-Kondoo.” Ufunuo 21: 14
“Nami sikuona hekalu ndani yake; kwa maana Bwana Mungu Mwenyezi na
Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake. Na mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza,
kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo. Na mataifa
watatembea katika nuru yake. Na wafalme wa nchi huleta utukufu wao ndani yake.”
Ufunuo 21:22-24
Pia,kuna miji ya kiroho ya
giza ambayo giza lake hutokana na giza la mtawala wake shetani. Miji hii
inaitwa miji ya uharibifu. Inaitwa miji ya uharibifu kwa sababu ndani yake
kunafanyika mambo ya uharibifu. Huko ndiko shetani huwaweka watu na mali za
watu alizoiba.
“Katika
siku hiyo itakuwako miji mitano katika nchi ya Misri itumiayo lugha ya Kanaani,
na kumwapia Bwana wa majeshi; mji mmoja utaitwa Mji wa uharibifu.” Isaya 19:18
“Macho
yangu yamechoka kwa machozi, Mtima wangu umetaabika; Ini langu linamiminwa juu
ya nchi Kwa uharibifu wa binti ya watu wangu; Kwa sababu watoto wachanga na
wanyonyao, Huzimia katika mitaa ya mji. Wao huwauliza mama zao, Zi wapi nafaka
na divai? Hapo wazimiapo kama waliojeruhiwa Katika mitaa ya mji, Hapo
walipomiminika nafsi zao Vifuani mwa mama zao.” Maombolezo2:11-12
Katika miji hii shetani na
mawakala wake hufanya kazi za giza pamoja na kuchukua watu walio imara, wenye
akili, wenye nguvu, wenye uelewa mkubwa wanaong’ara na kuwapeleka kwenye miji
yake ya kiroho iliyoko kuzimu. Huko watu hawa humtumikia yeye kwa namna
mbalimbali katika kuujenga utawala wake wa kuzimu.
Sio mpango wa Mungu watu wake
wakae uhamishoni. Ndio maana hata kipindi kile, baada ya muda mrefu wa kukaa
uhamishoni Babeli, Mungu alimuinua Mfalme Koreshi akawaruhusu wana wa Israeli
kurudi kwenye nchi yao. Naye mfalme Koreshi aliandika waraka kwa wafalme
wengine katika njia ambayo wana wa Israeli wangeitumia kupita ili wawaruhusu
kupita. Mungu anainua mfalme Koreshi kwa kanisa katika wakati huu na waraka pia
umekwishaandikwa na Bwana Yesu mwenyewe. Ni wakati sasa watu wa Mungu tuhame
kutoka uhamishoni katika ulimwengu wa Roho na kurudi kwenye asili yetu chini ya
kiongozi wetu Yesu Kristo. Ni kweli tumejenga, tumelima uhamishoni lakini
hatuna budi kuacha yote na kuirudia ile asili yetu.
MAOMBI
Kwa mamlaka ya jina la Yesu
Kristo, ninarudi kwenye mtazamo wangu wa asili niliowekewa na Mungu. Kwa jina
la Yesu ninarudi kutoka uhamishoni, ninawafyeka wale wote mnaonizuia nisirudi
kwa jina la Yesu. Ninatoka uhamishoni kwa jina la Yesu, ninahama kwenye
uhamisho wa kiroho kwa jina la Yesu; wale wote mlionipandikizia fikra na
mitazamo ya kishetani ninawateketeza kwa moto wa Mungu. Kwa jina la Yesu
ninaangusha milima yote iliyo mbele yangu, wachawi wote mlionizuia uhamishoni
ninawateketeza kwa moto wa Mungu, ninawaangusha kwa jina la Yesu. Kwa damu ya
mwanakondoo, nawasha moto kwenye miji yenu, natoka narudi kwenye asili yangu ya
rohoni kwa jina la Yesu Kristo. Ninafungua njia ya kupita kutoka kwenye utumwa
kwa jina la Yesu Kristo, ninarudi nyumbani. Ninahama kwenye ulimwengu wa roho
kutoka utumwani, narudi uzimani kwa jina la Yesu; ninahama kutoka mautini
narudi uzimani kwa jina la Yesu, ninahama kutoka kwenye kushindwa narudi kwenye
kushinda kwa jina la Yesu, nahama kutoka kwenye kufeli, kuhuzunika, kuogopa,
ninarudi kwenye asili ya ujasiri, nguvu, uweza, uimara, utajiri, mafanikio kwa
damu ya mwanakondoo. Kila anayenizuia ninamsambaratisha kwa jina la Yesu
Kristo. Wote mnaonizuia nisihame kwenye vifungo vyenu ninawafyeka kwa jina la
Yesu. Ninarudi kwenye asili yangu ya kumiliki kutiisha na kutawala kwa jina la
Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai. Amen!
0 Comments