UTUMIE UJANA WAKO VIZURI

UTUMIE UJANA WAKO VIZURI


Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.


BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno hai la MUNGU.
Ujana ni Umri kuanzia miaka 18 hadi miaka 45. 
Ni muhimu sana kuutumia ujana wako vizuri na njia muhimu sana ya kuutumia ujana wako vizuri ni kumcha MUNGU wakati wa ujana.
Kama kuna ujana basi na kuna uzee pia hivyo Utumie Ujana Wako Vizuri.
Yohana 21:18 '' Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka.''

 Andiko hili linaonyesha jambo fulani kuhusu ujana na kuhusu uzee pia, kuna  madhara ya kuutumia ujana vibaya maana katika uzee unaweza kukosa mwelekeo mzuri.
Ukiwa kijana unakuwa na nguvu za kwenda popote na kufanya chochote lakini ukiwa mzee utategemea zaidi matokeo ya kile ulichokifanya katika ujana wako.
Kama ujana wako uliutumia vizuri kwa MUNGU hakika uzee wako utakuwa mzuri kama bado ukibaki katika tumaini la wokovu wa KRISTO.
Utumie Ujana Wako Kwa YESU.
 Fanya Kazi Ya MUNGU Leo Ili Siku Ya Kupeleka Hesabu Uwe Kamili. 
Obadia 1:15 ''Kwa maana hiyo siku ya BWANA i karibu juu ya mataifa yote; kama ulivyotenda, ndivyo utakavyotendwa; malipo yako yatakurudia juu ya kichwa chako mwenyewe.'' 
 
Siku ya mwisho ni siku ya kutoa hesabu ya yale uliyoyafanya duniani.
Sijui wewe ujana wako unautumiaje!
Nguvu zako ulizonazo sasa unazitumia katika nini?
Mimi nakushauri sana uutumie Ujana Wako Kwa YESU Ili Uuweke Uzee Wako Pazuri. 
Utumie Ujana Wako Katika Maisha Matakatifu.
 Utumie Ujana Wako Kumcha MUNGU. 

Yoshua 24:14 ''Basi sasa mcheni BWANA, mkamtumikie kwa unyofu wa moyo na kwa kweli; na kuiweka mbali miungu ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, na huko Misri; mkamtumikie yeye BWANA.'' 
Kijana kwa sababu ana nguvu basi ni rahisi sana kuleta m,abadiliko mazuri katika familia yake au ukoo wake au taifa lake, Kama kijana huyo atajitambua.
Katika mambo yote vijana ndio hutumiwa kwa sababu tu wana nguvu. Ukiona maandamano na fujo jua tu kwamba wahusika ni vijana.
Ukiona kanisa linastawi jua tu kwamba vijana wanajitambua na wanatimiza jukumu lao.
Wazee hawawezi kutembea mwendo mrefu wakihubiri lakini vijana wanaweza.
Ndugu, Utumie Ujana Wako Kwa Faida Na Sio Hasara.
 Utumie Ujana Wako Kuenenda Kwa ROHO Bila Kutazamia Tamaa Za Mwili. 
Wagalatia 5:16 '' Basi nasema, Enendeni kwa ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.''
  
Fahari Yako Kijana Ni Nguvu Zako Tu Na Sio Vinginevyo Hivyo Nakuomba Sana Uutumie Ujana Wako Kwa BWANA YESU. 
Wewe ni kijana kwa sababu tu una nguvu na unaweza kutenda mambo mengi yanayohitaji nguvu.
 
Mithali 20:29 ''Fahari ya vijana ni nguvu zao, Na uzuri wa wazee ni kichwa chenye mvi.'' 
 
Utumie Ujana Wako Kujifunza Neno La MUNGU Na Kulitii. 
Utumie Ujana Wako Kumzalia MUNGU Matunda Kwa Utumishi Wako. 
Utumie Ujana Wako Kwa Kutafuta Amani Na Watu Wote.
Waebrania 12:14 '' Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona BWANA asipokuwa nao; '' 
 
 Utumie Ujana Wako Kuwaheshimu Baba Na Mama Yako Ile Upate Kuishi Miaka Mingi Na Heri Duniani.
Mathayo 19:19 '' Waheshimu baba yako na mama yako, na, Mpende jirani yako kama nafsi yako.''
  
 Utumie Ujana Wako Kuwa Na Moyo Safi Maana Ni Wenye Moyo Safi Tu Ndio Watamuona MUNGU.
Mathayo 5:8 '' Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona MUNGU.''
Jifunze Kumsikia MUNGU Katika Ujana Wako.
Umejifunza Sana Kumsikia shetani Kupitia Dhambi Ulizofanya Lakini Leo Jifunze Kumsikia Na Kumsikiliza MUNGU Na Kumtii.
 Tangu kuwekwa Misingi ya Ulimwengu hakuna na wala haitatokea Mtu awaye yote kujutia ndani ya nafsi alipochukua maamuzi upande wa kumtumikia MUNGU.

 Wewe Mteule ni mtu wa muhimu sana katika nyumba ya MUNGU, ishi tu maisha matakatifu na kumtumikia KRISTO.
 Wana Wa MUNGU Ni Wale Ambao Wameokoka Wameacha Dhambi Zote.
Utumie ujana wako kwa kuokoka na kuishi maisha matakatifu.
Kumcha MUNGU huongeza umri wa kuishi.
Mithali 10:27 ''Kumcha Bwana kwaongeza siku za mtu; Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa.'' 
Japokuwa uzee huishia katika kifo lakini wanaokufa wengi zaidi wakati huu ni vijana na sio wazee, kwa sababu tu hawamchi MUNGU na hawana hofu ya MUNGU ndani yao.
Ukisikia majambazi wameuawa jua tu ni vijana.
Magonjwa mabaya ya kuambukizwa kupitia uasherati yanawapata zaidi vijana na wengi hufa kwa sababu ya kutokumcha MUNGU kwao.
Ni muhimu sana wewe kuutumia ujana wako kwa BWANA YESU na sio kwa shetani.
Kijana hakuna haja ya kuwa muongo na tapeli.
Hakuna haja ya kuwa mwasherati  na kahaba.
Hakuna haja ya kuwa mwizi na kibaka.
Hakuna haja ya kuwa kutumia nguvu zako kwa shetani. 
 ''Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo, Na yeye asingiziaye ni mpumbavu.-Mithali 10:18''

Kama hukujua kumcha MUNGU ndio maana ulianguka dhambini basi geuka leo na anza na BWANA YESU.
Tengeneza maisha yako kwa YESU leo.
Anza kuishi maisha matakatifu kuanzia leo.  
Heri ukianguka dhambini amka na kuendelea mbele kuliko kuanguka na kulala kabisa.
Ukianguka mara moja kwenye dhambi amka kutoka kwenye dhambi na endelea mbele na KRISTO kuliko kuanguka na kuendelea na shetani moja kwa moja.
Usione fasheni pia kuanguka na kusimama bali jitahidi wakati huu ukianguka simama na usikubali kuanguka tena dhambini.

 Neno la MUNGU linaweza kumbadilisha mtu wa MUNGU mapema sana kama mtu huyo akilitii Neno hilo la MUNGU aliye hai.
Mimi sijui kama wewe ndugu ni mmoja wa wanaolitii Neno la MUNGU au ni mmoja wa wale wanaolipuuzia Neno.

Kumbukumbu 10:12 '' Na sasa, Israeli, BWANA, MUNGU wako, anataka nini kwako, ila umche BWANA, MUNGU wako, na kwenda katika njia zake zote, na kumpenda, na kumtumikia BWANA, MUNGU wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote; ''
Wewe ndio mwisraeli wa leo na MUNGU anataka umche yeye kwa moyo wako wote na umtumikie yeye kwa moyo wako wote.
Japokua shetani anakufuata muda wote lakini wewe mtafute KRISTO tu muda wote na huyo shetani atakuja kushangaa tu wewe uko uzima wa milele tayari.
Pia tambua kwamba Mwili huu hautaingia katika uzima wa milele hivyo ndugu usipende sana kuutii mwili maana mwili wako wakati mwingine unaweza kuwa ndio chanzo cha kuikosa mbingu kama utautii.


Unaweza kusema utajitakasa kesho lakini kesho usifike.
Unaweza kusema utaokoka mwaka ujao lakini wewe mwaka ujao usifike.
Kuokoka ni leo ndugu yangu.
Kuacha dhambi ni leo ndugu yangu.
Kuna baraka katika kumcha MUNGU BABA na hakuna anayeweza akajificha mbele za MUNGU.

Mithali 20:27 '' Pumzi ya mwanadamu ni taa ya BWANA; Hupeleleza yote yaliyomo ndani yake.''
 Jitahidi sana usiwe fedheha kwa kanisa.
Mwanakanisa anapoanguka dhambini anajiabisha yeye na analiabisha na kanisa zima pia. Ole wake Anayeliabisha kanisa la MUNGU.

Kama unautumia ujana wako kwa BWANA YESU Usilie wala usifadhaike, Mtetezi wako YESU anaishi leo na atakushindia hakika.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Post a Comment

0 Comments