mafundisho yenye makosa, yanayowaongoza watu katika uzoefu udanganyao.



Hatari za Mafundisho ya Kisasa – mafundisho yenye makosa, yanayowaongoza watu katika uzoefu udanganyao.

Wanasema kuwa aina hii ya “mapambano ya kiroho” ni muhimu kwa ajili ya mafanikio ya Injili. Pasipo shaka yoyote huo ni udanganyifu. Lakini tena wanatuambia kuwa kutakuwa na “majeruhi” miongoni mwa Wakristo, kwa sababu Wakristo wengi “hawana silaha zifaazo” kwa ajili ya aina hii ya mapambano au hawajafahamu “jinsi ya kupigana” aina hii ya vita! Lakini wazo la kuwa mtu anajishughulisha na vita vya kweli vya kiroho inaweza kumletea matokeo ya roho chafu kukushambulia na kuharibu maisha ya familia yake ni mafundisho yasiyo na maana na yasiyo ya Kibiblia. Hii ni zaidi ya aina fulani ya mafundisho ya ulozi ambayo yanaweza tu kuwaletea watu hofu katika mioyo yao. Hata kama chanzo cha majanga ambayo tunaelewa yanawaangukia wakristo, yanaweza kuwa ni kutokana na kujihusisha kwao na aina hii ya vita vya kiroho ambavyo sio vya Kibiblia, hii ni hoja ya kuijadili kama nilivyokwisha sema. Na sasa ningependa kufanya mambo mawili ya muhimu.

Kwanza, kwa vyovyote vile aina zote za matatizo hutokea katika maisha yetu ikiwa tutakuwa hatuishi kulingana na neno la Mungu. Katika Efeso 4:11-14, Mtume Paulo anaongea kuhusu huduma zitolewazo na Mungu kwa kanisa ili kwamba wote tupate kupokea kukua katika Kristo. Tunapaswa kukua na kuwa wenye nguvu katika ufahamu wa Kristo na tusibaki kama watoto wadogo au kama watu wa mwilini ambao huchukuliwa na kila aina ya upepo wa imani wakitazamia “jambo jipya” linalofuata – ili kutushitusha sisi na hivyo kutufanya shabaha ya hila na udanganyifu wa wanadamu.

Kumewahi kutokea uzao mwingi wenye hatari ya “upepo wa imani” au makosa yenye hatari kwa kadiri ya miaka mingi sasa. Makosa haya yawezekana yanaanzia au yanapata msaada wenye nguvu kutoka kwa waamini wa Amerika. Mafundisho hayo hayana msingi wowote wa neno la Mungu isipokuwa ni matokeo ya kufikiri kwa watu wenyewe na mafunuo ya pekee. Hali kadhalika na uzoefu wao binafsi ambao hauna ulinganifu wa kweli wa kimaandiko. Imani hizo zinahamasishwa na baadhi ya majina yanayo julikana vema, wengi wao ni viongozi wa mashirika yenye nafasi nzuri ya fedha nyingi ambazo ndizo zinazo wasaidia sana kusambaza ujumbe wao. Mengine hupeperushwa na upepo huu wa imani, pasipo hata kufikiria yale ambayo Biblia inasema au kufundisha. Na mradi wanakataa kuongozwa na neno la Mungu, haishangazi kwa hiyo kuona kwamba matendo yao pia huwa ni ya kimwili, Rumi 1:21-24. Ikiwa tutajiondoa kutoka kwenye neno la Mungu ndipo tutakuwa tunajiondoa pia kutoka katika maisha matakatifu yaliyo takasika. Yesu alisema, “watakase kwa kweli.” Yoh 17:17. Maisha ya watu hayajajengwa juu ya mwamba wa Yesu Kristo; juu ya mwamba wa kulitii neno la Mungu. Kwa hiyo si jambo kubwa la kushangaza kuona watu wengi wakipitia katika maisha ya taabu – katika nyakati hizi kunaonekana kuenea kwingi kwa watu kuondoka kutoka katika neno la Mungu ambavyo inaleta matokeo katika hali ya maisha kuwa ni ya kimwili na yasiyo imara kwa wakristo, ikiwafanya watu kuanguka katika aina fulani ya dhambi na shida na kuchomana wao kwa wao na kupitia kwenye huzuni nyingi. Katika mtiririko wa habari hii ni rahisi kwa waandishi hawa kusema kuwa watu wanapambana na matatizo katika maisha yao “kwa sababu” ya kujihusisha kwao katika aina hii ya vita vya kiroho, kwa sababu wapo wengi wenye matatizo tayari, lakini chanzo halisi cha matatizo yao kwa hakika yaweza ikawa ipo sehemu fulani.

Watu hawa hawaingii katika mapambano ya kiroho kabisa, bali wanaingia kwenye ulimwengu wa maroho unaotofautiana kabisa – pale wanapokuwa katika kudanganywa na kutokana na hilo huwajia “Injili nyingine”, “Yesu mwingine” na “roho mwingine”. Wanazitengeneza nguvu za “maroho ya kibinadamu” na kufanyika kuwa ni shabaha ya maroho yadanganyayo, ambayo ndiyo yanayowashawishi kuona kuwa wanajishughulisha na vita vya kiroho na kwamba watu wengi wanaendelea kudanganywa kunyang’anywa ufahamu wa kweli wa Mungu ambao umo ndani ya Kristo. Ndiyo naweza kuhisia kwamba mtu yeyote anayeifuata elimu ya mtindo huu na kuamini huku katika uzoefu unaofanana, lazima watajitumbukiza katika matatizo makubwa. Wanalivunja neno la Mungu, na wanalivunja ndani ya milki isiyo halali.

Inaweza ikatusaidia tukitazama katika 2Kor.11:1-15 ili kutusaidia kuelewa jinsi gani mambo haya yanavyoweza kuwa. (Tafadhali angalia katika makala ya kwanza ambamo hali ya kanisa la wakorintho pamoja na misingi ya udanganyifu wao ilivyoangaliwa). Katika kanisa la Korintho wengi wa watu wa Mungu huko walikuwa wanaenenda kimwili. Walipenda kupata “uwezo na utukufu”. Na hiyo hali ya kimwili pamoja na hayo matamanio ya kimwili ya kupata uwezo na vyeo ili wasababishia kupotelea mbali na mafundisho ya Kristo. Kung’ang’ania  kudumu katika mwenendo na tabia hizo kuliwaletea kuonekana wazi na kuwafanya wawe ni kafara ya udanganyifu wa shetani – ni udanganyifu wa kutisha! Tunaambiwa kuwa shetani mwenyewe hujigeuza katika sura ya “malaika wa nuru”, ule mstari wa 14. Ninaamini kwamba baadhi ya uzoefu wa watu hawa unapaswa ueleweke katika habari hii. Katika mstari wa 13 anaongea kuhusu “mitume wa uongo, wafanyakazi wenye hila, wakijibadilisha wenyewe kuwa mitume wa Kristo”. Katika mstari ule wa 4 anatueleza kwamba hata watu wa Mungu wanaweza kuongozwa na udanganyifu huu katika kumpokea Kristo “mwingine”, roho “mwingine” na Injili “nyingine”. Hatujaelezwa, kuwa mambo yanaweza kuwaje, lakini yanaweza kutokea iwapo mtu analiacha neno la Mungu, hilo limewekwa wazi sana kwetu. Na iwapo hilo liliweza kuwatokea wale ambao mtume Paulo mwenyewe aliwashuhudia na kuokoka ambao pia walikuwa katika hesabu ya kuongozwa na kuangaliwa kwa karibu na mafundisho yake; hivyo tusifikiri kuwa mambo haya basi hayawezekaniki nyakati za leo! Na hiyo ndiyo sababu inayoelekea kuandikwa kwa makala hii, kwa sababu mafundisho hata ya kisasa yanatuletea hila za shetani ili kuzichafua fikira za watakatifu kutokana na unyofu uliomo katika kristo – msitari wa 3. Katika Yeremia 5:30,31, tunakuta kufanana kunako shangaza juu ya yale anayoyasema mtume Paulo kwenye 2 Kor.11:13-20. Manabii wa uongo wakiwadanganya watu wa Mungu, viongozi wao wakiwatawala kwa nguvu, na bado watu wa Mungu wakiyapenda hayo yote! Mungu anaisema juu manabii kwenye Yeremia 14:14, “ndipo Bwana akaniambia, hao manabii wanatabiri uongo kwa jina langu mimi, mimi sikuwatuma, wala sikuwaamuru , wala sikusema nao; wanawapeni unabii wa maono ya uongo na uaguzi na neno la ubatili na hadaa ya mioyo yao“. Mambo kama haya yamewai kutokea na hata leo yanatokea pia.

Ijapokuwa yanawezekana kuwa mambo katika habari hii ambayo si rahisi kueleweka, inaonyesha wazi kuwa mtu yeyote asiye na haki anaweza akawasiliana na ulimwengu wa maroho, lakini umaarufu wake kwa watu wa Mungu ni kuwachafua iwapo angepata nafasi ya kufanya hivyo. Nimenukuu habari hapo juu ili kuonyesha kuwa watu wanaweza kuwasililana kimakosa na maroho, hata wakristo wanaweza kufanya hivyo. Ijapokuwa bila shaka sio habari yote hiyo ambayo inaweza kuwahusu waandishi hawa wa kisasa, bado kwa namna fulani, ninafikiri wameiharifu mipaka halali kama ilivyoonyeshwa katika 2 Kor.11:1-15.

Nilikuwa nasoma kitabu kimoja ambacho kimezungukia kasoro zote nilizo zitazama katika makala hizi tatu. Nilipokuwa nikisoma, niliamini kuwa mwandishi huyo amehalifu na ametumbukia katika udanganyifu. Kisha nikasoma kuwa mwandishi wa kitabu hicho yeye mwenyewe alikuwa analifahamu hilo. Yeye ni mwenye historia ya nyuma ya Kimarekani ya asili, naye anashuhudia kuwa, akiwa kama mkristo, bado mambo ya siri zake za hapo kale (au pengine tungeweza kusema kwamba unajimu au uchawi) ule uwezo wake wa kinajimu alioupata kutokana na desturi au mila za kihindi, ungeweza kujitokeza tena ndani yake na angeweza kufanya mambo yenye fumbo za kiunajimu (akiendesha ndani ya ulimwengu wa roho) ambao kwa uaminifu kabisa anakiri wazi kuwa hiyo haikuwa karama ya Roho Mtakatifu. (Ninaamini kuwa mambo kama hayo yanaweza kutokea na yanatokea siku za leo). Lakini ndipo anaendelea kusema kuwa alimwomba Bwana ili aondoshe na kuangamiza kabisa uwezo huo aliokuwa nao hapo kale. Hilo ni jambo jema. Lakini tena anaendelea kusema kwamba Roho Mtakatifu alishuka chini na kufikia kwenye ujuzi huo wa zamani na akawasafisha ili kuwatumia kwa ukamilifu zaidi! Hilo sio jambo jema! Na kadiri mtu anavyosoma kitabu, mtu huyo anaona kuwa huo ni ushuhuda wa uwezo wake wa mambo yake ya “kiunajimu” ya hapo kale yakimpeleka kwenye udanganyifu wa mambo ya uzoefu wa maroho ya kigeni ambayo hayatokani na Mungu. Wamebuni mafundisho mapya na uzoefu ambao wao wanauita “Baraza la Bwana” ambapo unaitwa mbele ya uwepo wa Bwana kwa ajili ya aina fulani ya mazungumzo. Sio uchaguzi wako. Mwandishi wa kitabu hicho wakati fualni alijisikia “ameitwa” kwenye uwepo wa Mungu pamoja na mtu mwingine, ambako Bwana aliwauliza iwapo Mungu sasa anaweza kuihukumu dunia hii. Na eti kwa sababu ya maombezi yao, ulimwengu uliachiliwa kutokana na hukumu ya dunia nzima kwa wakati ule, hii ni kulingana na watu hawa wawili wote kwa pamoja walivyoona na kuskia katika maono yao! Katika aliamini kuwa yeye mmoja na rafiki zake wanane walikuwa wakiitwa kwenye baraza la Bwana, lakini sasa yeye alishangaa kuona kuwa imekuwaje watu wote tisa waweze kusikia kitu kile kile na kuyaona maono yale yale (yanayofanana) kwa wakati mmoja. Hata hivyo alijisikia kuwa anapaswa “kutii na” wakaondoka pamoja, naye anasimulia jinsi ambavyo wote walivyoona kitu kile kile “katika roho” na kusikia kitu kile kile – sauti na maono ambayo wote kwa pamoja walipata kuyajua! Huo ndio upuuzi wa makutaniko ya mizimu, unajimu na ulozi! Hakuna hata moja kati ya hayo inayotokana na Mungu. Halifanani na chochote katika maandiko ya neno la Mungu. Wamefanya makosa ya nje hatari sana na wamedanganywa vibaya na hali hiyo italeta madhara mabaya. Kwa hakika huu ni “moto wa kigeni”! Yeye anasimulia maono hayo kwa kirefu katika kitabu chake lakini bado ni ya tabia ya kigeni na wala hayaleti sura yoyote ile ya kibiblia au hayana misingi yoyote ile ya Kimungu ndani yake. Ni kutokana na wanaume na wanawake wa jinsi hii ndio wanao leta mafundisho ya aina hii. Kama ilivyo kuwa kule Korintho nyakati za Mtume Paulo, ndivyo inavyotokea nyakati za leo pia. Watu wamejazwa maono yao wenyewe, wakimleta roho mwingine, Yesu mwingine, Injili nyingine. Wao wanaamini, kwa kadiri mnavyojua kuwa kwa kufanya hivyo wanakuwa wakimtumikia Mungu, lakini kwa ujumla kwa huzuni kubwa wamekosea.

Mambo haya yote huwaletea huzuni watu wengi wa leo kadiri wanavyo ona udanganyifu wa aina hii na kuchanganyikiwa kunako sababisha maumivu ya moyo, pamoja na matengano ikiwasababisha watu wa Mungu kukosea na kuwaondoa kutoka katika kweli na kuwaingiza kwenye vifungo Inaonyesha kuwa nyakati hizi shetani anajitahidi kufanya kila awezalo kudanganya ikibidi hata wateule. Je, anatumia njia gani kujaribu kufanikisha jambo hili? Kwa mujibu wa Yesu Kristo. Wakristo wa uongo (hii inamaana kuwa, ni wale wenye upako wa uongo) na watatokea manabii wa uongo nao watatoa ishara kubwa na maajabu. Ishara, maajabu manabii wa uongo na upako wa uongo ni vitu ambavyo shetani atatafuta kudanganya ikiwezekana hata wateule Mt. 24:24. Ikiwa mtu yeyote anaweza kutoa aina yoyote ya ishara na maajabu, au wanajifanya wenyewe kuwa ni mitume wenye nguvu au manabii, hapo ndipo wengi wa watu wa Mungu huonekana kuwa tayari kupokea mafundisho yoyote yale yanayoambatana nao! Hizo ndizo nyakati tunazoishi.

Kwa hiyo, ikiwa watu wanapata matatizo katika maisha yao, sababu kuu ni kwamba wamechagua kuishi pasipo imani na kutokuwa na utii wa neno la Mungu. Na nyakati za leo ni yote mawili hufanyika; yaani mafundisho ya uongo na uzoefu wa uongo ndiyo yanayowapeleka watu wa Mungu kuwa mbali na kweli na kuishi kwa ile kweli; sio kule kujiingiza katika mapambano ya maandiko kiroho ambako ndiko kunako sababisha matatizo, isipokuwa ni mafundisho yaliyokosewa ya aina hii ya vita vya kiroho, hiyo ndiyo chanzo cha mchanganyiko mkubwa, udanganyifu pamoja na matatizo.

Fungu la Maandiko Wanayoyatumia

Sasa tutaangalia aina ya aya ambazo waandishi hawa hupenda kuzilinganisha ili wapate kuyahalalisha makosa yao. Moja kati ya zile kuu inapatikana katika Efeso 6 na tutaanza kwanza kuitazama sura hii, pamoja na kufikiria kwa kifupi juu ya vita vya kiroho ni nini hasa, kabla hatujaendelea kuangalia katika sura nyinginezo.

EFESO 6:10-20
Hii penginepo ni sura ya msingi mkuu na ambayo mara nyingi hunukuriwa vibaya, ambayo hutumiwa kuunga mkono mafundisho yao kuhusu roho zitawalazo katika nchi. Mara nyingi hutumiwa na hawa waandishi wa kisasa ili kuainisha mapambano ya kiroho kuwa yanahusika na kuomba dhidi ya, na kuzifunga mamlaka na uweza ambayo inahusisha na roho zile za kiinchi, hii ni kulingana na tafsiri yao. Kama tunavyoangalia katika sura hiyo tuliyoitaja hapa, tunaona kuwa sura nzima haihusiki na chochote juu ya mambo kama hayo (niliishughulikia kwa makini sura hii pia pale nilipokuwa nafikiria ju ya maombi katika Agano Jipya kwenye makala yangu ya kwanza). Katika mstari wa 10 na wa 11, mtume Paulo anatusihi tuwe hodari katika Bwana tukizivaa silaha zote za Mungu ili tupate kuzipinga hila za shetani. Kwa nini tunahitaji silaha za Mungu? Ni kwa sababu adui yetu ni wa kiroho na kushindana kwetu ni kwa kiroho. Ule mstari wa 12 unatuambia kwamba kushindana kwetu, au vita vyetu sisi, sio juu ya damu na nyama, bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho”, (katika hali hiyo hatuhitaji kufafanua majeshi hayo yote ya kiroho, isipokuwa ni bora kuendelea kufuata hoja za mtume Paulo hapa). Kwa sababu ya hilo, tunahitajika kukamilika kiroho. Peke yetu wenyewe tu, hatuwezi kuushinda upinzani huu wa kiroho na hila! Sasa, baada ya kuliweka hili wazi katika ule mstari wa 12 mtume Paulo anatusihi kufanya nini hapo? Je, yeye anasema kwamba, “kwa kuwa upinzani wetu ni wa kiroho, jichukulieni wenyewe silaha za Mungu ili kwamba unaweza kuomba dhidi ya mamlaka hizi na uweza na kuzifunga kwa jina la Bwana”? Je, hivyo ndivyo mtume Paulo anavyozielewa vita vya kiroho? Je, hii ndiyo njia ya kupata ushindi? Hapana! Hivyo siyo hoja yake kabisa!

Anatuambia katika ule mstari wa 13 kwamba tutwae silaha zote za Mungu, ili tupate kuweza kushindana siku ya uovu na tukisha yatimiza yote kusimama! Mtume Paulo anazungumza kuhusu silaha ambazo zitatuwezesha kuyashinda majaribu na vishawishi mbali mbali ambavyo majeshi ya kiroho ya uovu yanaweza kutuingizia, na hatimaye tuweze kushinda. Anazungumza kuhusu mwenendo wetu kiroho katika Bwana. Hivyo mtume Paulo anatutia moyo kwamba “tupate kusimama”, hiyo ina maana kumpinga shetani na kuyashinda vishawishi vyake katika maisha yetu ya kila siku. Ili kuyafanya hayo tunapaswa kuipata kweli ya Mungu, na kuvaa dirii ya haki (mstari wa 14). Kweli ya Mungu itashughulikia uongo wa shetani na pia itatuadilisha na kututia moyo. Kusimama katika haki tuipatayo katika Kristo kutaitunza mioyo yetu ikiwa imesafishwa na kulindwa. Ushuhuda wa Kristo unapaswa mara zote uwe hai ndani yetu ili kwamba tuwe tumejiandaa kuwashirikisha watu wengine Injili hii (mstari wa 15). Kisha katika ule mstari wa 16 mtume Paulo anatusihi, “zaidi ya yote, tuitwae ngao ya imani ambayo kwa hiyo itatuwezesha kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu”. Anachokiongelea hapa ni kujishughulisha na kukataa malaumu yote, uongo na mashauri ya shetani ambao anatutupia ili kutufanya tumtilie mashaka Mungu pamoja na upendo wake kwetu, ili kutufanya tujisikie wenye kuhukumiwa, tusio na maana; na pweke ili kutufanya tujisikie wasikitivu au tunao jihurumia. Tunapaswa kuyashughulikia hayo yote kwa kuiweka imani yetu na matumaini yetu kwa Mungu na katika yale aliyokwisha yasema. Wote huwa tunashawishiwa na kujaribiwa kama ilivyo katika mstari huu; sote tunajua yanafananaje mambo hayo. Lakini sasa hayo ndiyo mapambano yetu kiroho na tunapaswa kuchukua ngao ya imani na wala tusijiachie wenyewe kudhurika kwa uongo wa shetani na mashauri yake. Ni kweli kuwa katika hali hii wengi wetu huanguka. Hatusimami kama mtume Paulo anavyo tusihi, na hivo tunaupoteza ujasiri wetu, furaha na amani yetu katika Bwana. Tunaishia katika kujisikia kuhukumiwa na tusio na maana, tukishangaa iwapo ni kweli Mungu anatupenda na kutujali. Katika hali ya jinsi hii, kwa kweli hatuwezi kukua katika Bwana na bado kuna upungufu wa matunda juu ya Mungu. Sura hii inapiga moja kwa moja nyumbani katikati ya mwenendo wetu na vita vyetu kiroho.

Ukweli ambao mtume Paulo anauelezea hapa ni wa lazima kwa ajili ya mwenendo wetu kiroho na kimapambano. Ni wa maana na ni dhahiri. Wanakaa katika moyo wa maisha ya kiroho na ya ushindi. Hivyo ndivyo inavyohusika na vita vya kiroho. Sio kuanza kuikunja “mikono ya kiroho” na kupiga kelele na kumkemea shetani na maroho ya nchi. Pasipo maswali yoyote, ni vyepesi zaidi na inaashiria kimwili zaidi mtu kuomba dhidi ya roho mbaya katika maombi ya mikutano, kuliko ilivyo katika maisha ya kila siku katika imani, upendo na utii kwa Mungu kusimama katika silaha za Mungu; hi ya mwishoni inawakilisha vita vya kiroho kulingana na maandiko, lile la kwanza halina lolote!

Mtume Paulo anaendelea katika kutusihi tuchukue chepeo ya wokovu – ambayo itatunza na kulinda akili zetu katika kristo – na upanga wa roho, ambao ni neno la Mungu. Tukiwa tumevaa silaha zote za Mungu, Paulo anatusihi sasa kuomba (mstari wa 18). Haya, je sasa tunatakiwa kuomba dhidi ya mamlaka na uweza na kuzifunga? Sasa, kwa kuwa tumepata silaha za Mungu, tunapaswa kusimama dhidi ya roho zitawalazo maeneo na kufunga uweza wake? Hapana. Sio hivyo, kulingana na mtume Paulo. Lakini Je, hivyo si ndivyo silaha inavyotakiwa kuwa? Kutujaza nguvu katika maombi kuzifunga roho mbaya? Hapana; sio hivyo, kulingana na mtume Paulo. Mtume Paulo hataji kuomba dhidi ya maroho na kuzifunga. Anazungumza kuhusu “kuomba kwa sala zote, na maombi kila wakati katika roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote na kwa ajili yangu mimi…..”

Kwa hiyo kuenenda kiroho, na kuzishinda kwa mafanikio hila za shetani katika vita hivi vya kiroho katika maisha yetu ya kila siku, kunatuwezesha kuomba kwa ufasaha kwa ajili ya watakatifu. Kwa uwazi kabisa maombi ni sehemu muhimu ya mwenendo wetu kiroho mbele za Mungu, lakini tunawezaje kuomba kwa ufasaha pale tunapolitilia shaka pendo la Mungu na matunzo yake kwa ajili yetu, pale tunapojisikia kuhukumiwa watu tusio na maana, au tusiopendwa, pale tunapokuwa na uchungu, kutokusamehe na ugumu mioyoni mwetu; pale tunapokuwa katika kutokuamini! Kwa hiyo tunaweza kuona kuwa, mtume Paulo anatupatia amri sahihi katika sura hii – uhusiano wetu na Mungu, pamoja na mwenendo wetu mbele zake lazima uwe safi kabla hatujaweza kuwa wenye mafanikio kiroho katika maeneo mengine. Kwa hiyo vita vya kiroho vinahusika na kupinga vishawishi vya shetani na uongo wake katika mwenendo wetu wa siku kwa siku na Bwana – tukivaa silaha zote za Mungu. Hilo ndilo linatuwezesha kuomba kama itupasavyo kwa ajili ya watakatifu.

Sura hii yote ya mtume Paulo haiwakilishi mbinu fulani fulani au maagizo ya kuyashambulia na kufunga maroho mabaya kupitia maombi! Kwa urahisi tu anasema kwamba, kwa sababu adui yetu ni wa kiroho, kwa hiyo silaha zetu zinapaswa kuwa za kiroho, katika mapigano yanayotuhusu ili kupinga vishawishi, uongo na mashauri ya kutokuamini ambayo shetani atayapanda ndani ya mioyo yetu na maisha yetu. Kwa kweli, mbali ya mapepo kufukuzwa nje ya mtu mmoja mmoja, haupo mfano hata mmoja katika maandiko unao mwonyesha mtakatifu yeyote moja kwa moja akishambuliana na kuzifunga mamlaka zozote zile, uweza au roho zitawalazo maeneo, katika maombi. Maombi yote katika Biblia yanaelekezwa kwa Mungu.
Katika maombi watu wa Mungu wanakiri na kutukuza Uungu wa matoleo yake na wanatoa haja zao kulingana na mafunuo ya neema ya tabia ya uungu wake. Na maombi yao mengi ni kwa ajili ya watu wa Mungu. Kama inavyoonyeshwa na mtume Paulo katika sura hii.

Vita vya Kiroho Kulingana na Maandiko – kwa kifupi.

Hatutakwenda kuangalia kwa undani juu ya somo hili katika makala hii, lakini ningependa kutoa muhtasari wa ukweli huu wa lazima; huku tukifikiria juu ya Efeso sura ya 6.
Hebu tuanze mwanzoni kabisa; katika bustani ya Adeni mambo yote yalikuwa mema, lakini baadaye nyoka alikuja katika bustani. Je, hiyo ilikuwa ni kuvamiwa kwa nchi ya Mungu na mapepo? Je, haya yalikuwa ni mashambulizi ya ghafla na upenyezaji usiotakiwa ili kuharibu kusudi la Mungu? Kibinadamu, tunaweza kufikiri, kuwa ni jambo la kuhuzunisha kuona shetani kupewa nafasi katika bustani, wakati kila kitu kilikuwa salama na pengine tunashawishiwa kufikiri kuwa Adamu na Hawa wangeweza kufanya maendeleo iwapo kama isingekuwa huo upenyezaji wa shetani. Tunaweza kufikiri ingeweza kuwa ni vema kuitisha mkutano wa maombi na kuanza kumfunga na kumkemea shetani au kumtaka Mungu atumie uwezo wake kumfukuza shetani. Lakini pengine tunaweza kupata ufahamu mzuri zaidi na undani wake juu ya tukio hilo kwa kuyatazama maandiko mengine.

Kama tutaangalia katika kitabu cha kumbukumbu ya torati sura 8:2,3, Ayubu 1:6-12 na Mathayo 4:1, kwa uangalifu na moja baada ya nyingine, tunaona kuwa Mungu aliruhusu watu wake pamoja na mwanae pekee ili aweze kujaribiwa na kushawishiwa kwa kupitia mazingira na kwa mashauri ya shetani. Kusudi la Mungu ni kuona kuwa hakuna mtu hata mmoja awezaye kuumizwa, kuharibiwa au kuanguka katika dhambi bali waweze kupitia katika mazingira hayo yanayowajaribu na kuwapima. Na ilikuwa ni mazingira hayo ambayo ndiyo yangewataka kufanya uchaguzi! Kupitia mambo yote mawili lile linalohusu namna walivyofikiri na lile lihusulo jinsi walivyoweza kufanya. Na ilikuwa ni kupitia uchaguzi huu sahihi, kwa kuchagua kumwamini na kumtii Mungu ndiko kutakako wafanya wakue kiroho katika maumbile na katika kumfahamu Mungu. Majaribu na shida za jinsi hiyo kwa kweli ndizo zilizokuwa ni njia yao ya kukua katika neema na kumfahamu Mungu. Mungu hakuhitaji watu wake waanguke au watende dhambi. Hiyo ni kinyume cha tabia yake! Yeye alipenda kuwaleta katika ufahamu na sura yake yeye mwenyewe, kwa wao kuukataa uovu na kuchagua mema. Mistari inayofuatia inabeba ukweli huu tunao uangalia hapa Rumi 5:3-5; Heb.5:8,9,13,14; Yak.1:2-4; 1Pet.1:6-8.

Kusudi la Mungu la kumturuhusu shetani amjaribu Adamu na Hawa ilikuwa ni kuwawezesha kukua katika neema na haki ya Mungu wao, na katika upendo wao kwa yeye. Na walipokabiliana na mashauri ya shetani jibu la Adamu na Hawa halikuwa ni kuitisha mkutano wa maombi ili kumfukuza shetani nje ya Adeni; isipokuwa ni kuvaa silaha zote za Mungu na kuupinga uongo wa shetani na sio kuyaruhusu mashauri ya shetani yapate sehemu katika mioyo na akili zao! Hili la mwishoni linawakilisha vita vya kiroho; lakini lile lililo tangulia halihusiki na lolote. Kama wangaliweza kulifanya hilo la mwishoni, ndipo shetani  angewaachia Yakobo 4:7. Shetani alipomjia Hawa angepaswa kutumia upanga wa roho dhidi yake shetani kwa sababu alilijua neno la Mungu kwamba watakufa iwapo watakula mti wa ufahamu wa mema na mabaya. Lakini yeye hakuuchukua upanga wa kiroho dhidi ya uwongo wa shetani; hakuchukua ngao ya imani dhidi ya mashauri yake yanayoendelea. Mungu alikuwa ni mwema sana kwa Adamu na Hawa kwa kuwaumbia kila kitu kwa ajili yao naye kuwaumbia kwa mfano wake mwenyewe ili kwamba waweze kuwa na ushirika pamoja naye.

Yule nyoka alipomjia, Hawa angeweza kutumia upanga wa kiroho dhidi yake, kwa vile alilijua neno la Mungu kwamba wangekufa iwapo wangekula tunda lile. Lakini Hawa hakuushika upanga wa Roho wala ngao ya imani juu ya maongo ya Shetani. Alisahau ule wema wa Mungu kwao akiona tunda lile alilolitaka ili kujipendeza. Hivyo shetani anawadanganya na kuwaongoza kuelekea kwenye kiburi. Na hasipo dirii ya haki na chepeo ya wokovu kwa kule kumruhusu mawazo mabaya kuhusu Mungu yaweze kupandwa ndani ya moyo wake na akili zake. Mawazo mabaya ya kutokuamini ambayo shetani aliyapanda ndani ya moyo wake, ilimfanya Mungu aonekane kama ni mtu asiyetujali na kutupenda, kana kwamba anayekataza mambo mazuri yasitupate, kwamba aonekane ni mtu asiyetutakia mema ila mabaya. Mungu alikwisha waambia wasile mti ule kwa ajili ya manufaa yao wao wenyewe na wokovu wao. Yeye alipenda wawe kama yeye alivyo, lakini shetani aliwashauri kuwa Mungu alikuwa anawazuia kula tunda la mti ule, kwa sababu hakupenda mambo mema yawajie. Hakupenda wao wawe kama yeye alivyo! Ni kweli shetani ni baba wa uongo! Anaweza tu kuzungumza uongo, na kusudi lake ni kutokumheshimu Mungu na tabia yake ndani ya mioyo na akili za watu, ili kwamba watu hao wasiweze kuweka imani zao na matumaini yao kwa Mungu. Kwa hakika pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, naye asiyeamini amemfanya Mungu kuwa ni muongo, 1Yoh.5:10. Pasipo imani hatuwezi kuufaidi wokovu wa Mungu pamoja na neema yake ambao tumepewa kupitia Kristo. Jambo hili kwa hakika shetani analijua na hapo ndipo anapopazingatia na kuelekeza shughuli zake, ambayo ni kutufanya sisi tumtilie shaka Mungu!

Shetani huja kupanda hoja na mawazo yasiyo na faida ndani ya mioyo ya watu, ikiwa pamoja na watu wa Mungu. Kwa kutumia mashaauri yake yanayoendelea, yeye hutafuta kuziinua hoja zake hizo kinyume na ufahamu wa Mungu; na kuangamiza ile sura na ufahamu wa Mungu. Mashauri yake hayo yakudanganya yanaendelea kushikilia akili za watu wale wanaoyakubali. Ni “mambo ya juu” yanayopinga maarifa na utukufu wa Mungu, 2 Kor.4:4-5. Katika sura hii, ndani ya waraka wa Wakorinto wa pili, Mtume Paulo anaelezea ukweli unaofanana na ule ulioko katika Efeso 6, yaani, vita vyetu sio vya kimwili, lakini silaha zetu zina nguvu kupitia Mungu, na kuziangusha “kila ngome” za aina hii, hoja za udanganyifu ndani ya akili za watu, ambazo zinapinga ukweli na ufahamu wa Mungu. Sura hii haiwakilishi mbinu ya kuzifunga roho zitawalazo katika maeneo ambazo ziko mahala fulani huko angani, bali inakusudia kuonyesha silaha za ki-Mungu ambazo tunazo pale tunaposhughulika na hoja za udanganyifu za shetani! Ufumbuzi kwa Hawa, haikuwa ni kujaribu kumfunga shetani, isipokuwa ni kupinga na kukataa uwongo wake na ndipo angeweza kumkimbia, Yak. 4:7.

Majaribu ya jinsi hii yanaruhusiwa na Mungu. Kristo alipokuwa anabatizwa, mara moja akaongozwa na Roho Mtakatifu kwenda nyikani kujaribiwa na shetani, Mt. 4:1. Hayo yalikuwa ni maongozi ya ki-Mungu. Wala haikuwa ni kujipenyeza kwa mapepo! Hiyo ilikuwa ni msingi wa makusudi alioudhamiria Mungu; haikuwa ni ajali ya bahati mbaya ili kuiharibu kazi ya Mungu. Ilikuwa ni kupitia majaribu haya halisi, ndiyo yanayotufanya tuwe imara katika Mungu na kukua kiroho. Tunasoma katika Injili ya Luka kuwa Yesu alienda nyikani akiwa amejaa Roho. Na baadaye alirudi akiwa na nguvu za Roho (Luka 4:1-14), na hilo ndilo kusudi la Mungu kwetu. Lakini sasa Mungu anatutazamia tumchague, kumpenda na kumwamini yeye!  Ikiwa hatuwezi, ndipo majaribu yanafunua udhaifu, kujipendeza kwetu au matendo maovu katika mioyo yetu, Kumb.8:2,3. Sura hii yenye msingi katika kumbukumbu ya Torati inatuonyesha kwamba Mungu anayaruhusu majaribu ili kutufanya tuweze kujifunza kumtumaini yeye kuliko kitu kingine chochote kile. Hata mbele ya mahitaji mengi na masumbufu; neno lake ndilo lipaswalo kuwa la maana zaidi kwetu kuliko baraka zozote za muda zilizo nje. Upendo wetu na imani unapaswa uendelezwe na kutumbukia ndani zaidi nyakati kama hizo – na hivyo haitatusababishia sisi kukua katika maumbile kiroho tu – bali pia itamtukuza Mungu!

Hebu angalia jinsi Yesu anavyomshughulikia shetani pale nyikani. Yesu hakumpigia makelele shetani na kumfunga kwa kujaribu kumfuata yeye! Kwa hakika, yeye ameongozwa katika nyika ili aweze kujaribiwa na shetani. Na shetani mara zote huja na aina hiyo hiyo ya mashauri: “Mungu wako yuko wapi? Je, wewe ni mwana wake hasa? Una njaa na ni muhitaji. Je ni kweli anakujali wewe? Kwa nini hufanyi kitu kingine chochote kile sasa ili kutimiza hitaji lako? Fanya ili kujisaidia wewe mwenyewe! Fanya ili kujipanga mwenyewe. Ikiwa utajifurahisha mwenyewe, tazama utanufaikaje na jinsi gani ambavyo mambo yako yatakuwia rahisi!” Mambo kama hayo ndiyo tabia ya mashauri yake. Lakini Yesu alijibuje? Alijibu kwa upanga wa roho – kwa neno la Mungu. Naye ananukuru katika kumbukumbu la Torati 8:31 Israel wamekuwa wakitembea jangwani kwa miaka 40; na Yesu aliitumia siku moja nyikani kwa ajili ya kila mwaka wa miaka hiyo, akiwa anajaribiwa, kama vile na wao walivyojaribiwa. Lakini Yesu hakuhusika na “mahitaji” yake mwenyewe, wala hakuweza kumpatia muda wowote ule shetani kwa kuyasikiliza mashauri yake – Yesu yeye aliishi kwa neno la Mungu, akimheshimu na kumwabudu Mungu zaidi kuliko lolote lile lingine! Yesu alimpinga shetani na shetani akamwachia kwa muda.

Lakini Israel alishindwa kule jangwani. Wao hawakuishi kulingana na neno la Mungu pale walipokabiliana na shida na mahitaji. Hawakuchukua upanga wa imani bali waliruhusu shetani ajaze mioyo yao na akili zao kwa mashauri ya uongo kumhusu Mungu. Na hivyo mashauri hayo yakajenga ngome katika fikara zao nao wakampinga Mungu na kukufuru tabia yake. Asili ya vita vya kiroho vya shetani ni kuwaelekeza watu waingie katika hali ya akili na moyo ambapo watakuwa wakifikiri kama Israel walivyofikiri. Katika Kumb. 1:27, tunaambiwa kuwa kwa kweli Israel waliamini kuwa Mungu alikuwa amewachukia na kwamba amewaleta jangwani ili kuwaangamiza! Na hivyo ndivyo walivyoweza kufikiri hata baada ya kuona yale maajabu ya Mungu aliyowafanyia huko Misri na katika jangwa! Huo ndio udanganyifu wa dhambi na kutokuamini! Na hizo ndizo mbinu za shetani kutufunga sisi tufikirie mambo mabaya kuhusu Mungu na kuutilia shaka wema wake juu yetu. Ni kwa njia hiyo ndivyo shetani anavyo tafuta kutuleta au kutuweka nje ya neema ya Mungu, wokovu na urithi ambao ametuwekea. Tunaweza kutenda dhambi, lakini ikiwa tutajinyenyekeza wenyewe na kumtumainia Mungu kuutafuta msamaha wake, ndipo atatusamehe kulingana na neno lake. Lakini ikiwa mtu atautilia shaka wema wake na asili yake Mungu, mtu huzo atawezaje kupokea chochote toka kwa Mungu? Tunaelewa kuwa Israel alipoteza kutokana na kutokuamini. Lakini hawakuweza kumlaumu shetani kwa ajili ya hali ya mioyo yao. Mungu alikuwa anawategemea wamwamini na kumtii yeye. Majaribu hayo yaliweza tu kufunua hali ya mioyo yao. 

Ni kazi ya shetani kuwapata watu ili waweze kuamini mambo haya, lakini sisi tunahusika kama wana wa Mungu, ikiwa tutajiruhusu kushawishika katika kuamini mambo hayo! Hivyo ndivyo moja ya sababu kuu za kwa nini Paulo anaandika yale anayofanya katika Efeso 6.

Kama ilivyokuwa kwa Hawa katika bustani, na ilivyo kwa Israeli kule jangwani, na ilivyo kuwa kwa Yesu kule nyikani, ndivyo itakavyokuwa kwako wewe na mimi. Shetani hutujia ili kupanda mashaka ndani ya mioyo yetu dhidi ya Mungu. Dhambi hii ya kutoamini inavunja ushirika wetu na Mungu na inatuzuia kupokea mambo mema aliyo tuwekea Mungu, inapofusha mioyo yetu isione kweli na inampa nafasi shetani kutufanya mateka kwa aina zote au mwenendo mbaya. Hivyo tunapaswa kumpinga na kupigana vita vizuri vya imani, ambavyo kwa hiyo tumetunzwa salama na kukua na ambavyo kwa hiyo Mungu anaheshimika!

Mmoja wa wahamasishaji wakuu wa mafundisho hayo ya kisasa anashauri kuwa Yesu alishiriki katika “vita vya kiroho vya kiwango cha mbinu” (strategic – level spiritual warfare) ambapo alijaribiwa nyikani. Anasema kuwa, eti hayo majaribu aliyoyapata Yesu kule nyikani yanawakilisha kiwango cha juu cha mapambano ya kiroho na shetani, ambayo wachache wetu tu au hakuna hata mmoja awezaye kuyapata. Kwa vyovyote vile jambo kama hilo ni uwongo mtupu! Sote huwa tunapitia katika majaribu yanayofanana vile vile kama hayo, ndani ya maisha yetu! Shetani hatokezi kwetu kama aina fulani ya dudu baya lenye mapembe kutushurutisha kufanya makosa. Ingekuwa ni wazi! Tungeweza kuona kupitia mbinu hizo na kushituka! Shetani yeye hutumia hila. Huja katikati ya majaribu na shida; na kujaribu kupanda lile linaloonekana kama la “maana” au “mashauri yenye kusihi” na mawazo katika “akili” zetu. Lakini mashauri yote hayo yanalo lengo moja tu na yanatuongoza kuelekea katika aina moja ya hali ya akili – kutufanya tumtilie mashaka Mungu na tutende kwa kujitegemea! “Yuko wapi sasa Mungu wako? Je, ni kweli anakujali? Kwa nini basi huchagui njia nyepesi?” Haya ndiyo aina ya mawazo ambayo shetani anaweza kuyapandikiza ndani ya akili zetu. Nasi tunaweza kuona kutokana na mistari iliyotajwa hapo juu, kwamba iwapo tutakuwa tunaonyesha haja ya kutaka kutosheleza miili yetu au sisi wenyewe, kuliko kumpenda na kumtii Mungu, ndipo majaribu ya shetani yatatujia. Kwa vyovyote vile shetani hawezi kutujia na kutusimamisha juu ya jengo, wala hataweza kuja na “kutupatia” ulimwengu iwapo tutamwabudu yeye. Mazingira haya maalum kwa hakika ni ya kipekee kabisa kulinganisha na majaribu ya Yesu. Lakini lile ambalo sio la kipekee ni kwamba shetani anatujia na aina ile ile ya majaribu kwetu kila mmoja. Ikiwa shetani hatafanikwa kutupata tumtilie mashaka Mungu, ndipo anajaribu kutupata tutumbukie mbali zaidi katika yale tunayoyaamini ili kwamba tuweze kuwa na kiburi na tuishie katika kumjaribu Mungu – ambayo ndiyo yale ambayo shetani anajaribu kuyafanya kwa vyovyote vile, ili kumtia moyo Yesu aweze kurukia juu ya hekalu, au shetani atajaribu kutia moyo au kuweka katika akili zetu chanzo cha tendo fulani ambalo litatufurahisha, kufanya mambo yawe rahisi kwa ajili yetu, kutupatia faida au litutukuze sisi. Hii ndiyo ilikuwa tabia ya jaribu la mwisho la Yesu. Lakini maandiko yote yanatusihi kujikana wenyewe, kumpinga shetani na tujikabidhi wenyewe kwa Mungu na kuyaweka matumaini yetu kwake. Hivyo ndivyo alivyofanya Yesu, ambaye katika maeneo yote alijaribiwa kama tunavyojaribiwa sisi, (Heb. 4:15), na hivyo ndivyo itupasavyo na sisi kufanya. Hivyo ndivyo tunabyokua kiroho kiroho, na hivyo ndivyo tunavyoweza kuingia katika urithi ambao Mungu ameutayarisha kwa ajili yetu katika Kristo.

Tabia halisi ya vita vya kiroho kama ilivyo kuwa kwa Adamu na Hawa, kama ilivyo kuwa kwa Israel kule jangwani, kama ilivyo kuwa kwa Yesu kule nyikani na kama ilivyo kwako wewe na mimi, inatupasa kupinga na kukataa mashauri yote ya aina hii ili kusudi yasipate nafasi katika mioyo yetu. Na tunapaswa kufanya hivyo hasa tuwapo katikati ya majaribu, wakati wa shida na maumivu, tukiwa na juhudi katika imani ya Mungu pamoja na wema wake ambayo inalikumbatia neno lake. Na katika hili agano jipya sasa tumepewa nguvu ya kumpinga na kumshinda yule adui kwa roho na ule uzima wa Kristo uliomo ndani yetu.
Nimewahi kuhudhuria katika makanisa ambayo tumeweza kuomba dhidi ya shetani na kuzifunga roho chafu. Wakati fulani mtu mwingine angeweza kuomba, angeweza kumfunga shetani na kumtupa katika bahari au shimoni! Ninakiri ya kuwa niliweza kushangaa niliona ni jinsi gani shetani alivyoweza kutoka huko alikotupiwa baada ya kuwa tulikwisha “mfunga” katika mikutano ya maombi yetu! Nilijiuliza iwapo yale tuliyokuwa tukiyafanya yalikuwa ni mambo ya kiroho au la, na iwapo ilikuwa na ufanisi wa kweli mbali ya kutufanya sisi “tujisikie vizuri”. Na ilitufanya sisi tujisikie vizuri na “wenye ushindi” kule kupandisha sauti zetu na kupiga kelele na kuzifunga roho chafu – kwa vyovyote vile kulikuwa upande wa washindi! Ninaamini kuwa shetani na roho chafu na kwamba wapo kazini kupinga kazi ya Mungu ndani na kati ya watu, lakini kwa uaminifu kabisa siwezi kusema kuwa kwa kelele katika mikutano ya maombi yetu ambayo inakazia juu ya shetani na kuomba moja kwa moja dhidi yake, kuwa inaweza kuwa na ufanisi wowote ule wa kweli. Hapa sisemi kuwa haitupasi kuomba juu ya mazingira ambayo yanaonyesha kuwa shetani anaingilia, au haitupasi kupiga kelele katika maombi. Sisemi hivyo. Napenda tu kuwatia moiyo watu wa Bwana katika maombi, lakini iwapo tutaangalia katika maandiko kwa uaminifu, hatuwezi kupata kuiona aina hii ya uombaji kuwa ndio njia ya kumshinda adui. 

Niliwahi kujihusisha na aina hii ya maombi hapo zamani, na bado sijabadili kuamini kwangu juu ya Mungu au shetani, lakini ninatakiwa kukabiliana na yale ambayo kwa kweli maandiko yanaonyesha na kufundisha, kuhusiana na kuomba pamoja na vita vya kiroho. Vile vile nilipaswa kukabiliana na ukweli kwamba, mbali ya kutufanya tujisikie wazuri, hatukuweza kwa hakika kuelewa au kusikia ushahidi wowote kwamba kumfunga shetani kwetu au roho chafu kuliweza kuleta ufanisi wowote ule. Katika hayo yote kuhusika kwangu ni kwamba tunajaribiwa na Ibilisi mwenyewe kutuingiza katika kiburi. Mbinu moja wapo ya shetani, pale aliposhindwa kumpata Yesu ili ajifurahishe mwenyewe na kuyabadili mawe yawe mkate, ilikuwa ni kumshawishi Yesu zaidi ya njia nyingine. Kwa kuwa Yesu alikuwa akiishi kwa neno la Mungu, shetani angejaribu kutumia hilo ili kumpeleka Yesu katika kiburi. Shetani alimpandisha Yesu juu ya hekalu, akanukuu maandiko kutoka katika kitabu cha Zaburi kuhusu malaika wakimwangalia Yesu ili kwamba asiweze kudhurika. Na tena akasema ikiwa yeye ni mwana wa Mungu basi ajidhihirishe kwa kuruka kutoka juu ya hekalu! Yesu hakufanya hivyo, akanukuu maandiko “usimjaribu bwana Mungu wako”, Kumb. 6:16. Katika majaribu hayo tunaona kwamba shetani ananukuu maandiko lakini anafanya hivyo ili tu aweze kumpata Yesu ili afanyemambo kipekee pasipo Mungu. Yesu hakuhitaji kufanya mbinu maalum kwa ajili ya shetani ili kuhakikisha kuwa yeye ni mwana wa Mungu.Yesu anaishi tu katika kumtukuza na kumpendeza Baba yake!

Lakini hivyo ndivyo ambavyo shetani atajaribu kututendea kutujaza akili zetu na mambo ya hakika yaliyo na ukweli fulani wa kimaanddiko, lakini yote hayo ni ili kutufanya tuende mbali zaidi na yale ambayo Mungu ametuamuru ili atusababishie maumivu au hasara kwa namna fulani. Hivyo watu wanaweza kufikiri, “sawa, sisi ni wana wa Mungu naye ametupatia uwezo kumshinda shetani! Basi hebu tuombe dhidi yake na kuzifunga nguvu zake!” Lakini mtazamo wa aina hii sio wa kibiblia. Ni majivuno. Na inaenda mbali zaidi ya yale ambayo Mungu ametuagiza kuliko kumshinda shetani, inalenga uangalifu wetu tuutupie kwa shetani na hivyo kutufanya tumtukuze yeye na kumhesabia yeye kuwa ni maarufu na mwenye uwezo kuliko ile aliyonayo kwa hakika au inayompasa! Hii kwa kweli inapora utukufu wa Mungu na uweza wake katikati yetu! Bwana Yesu alisema kuwa – walipo wawili au watatu wamekusanyika pamoja kwa jina langu; yeye atakuwa katikati yao. Hakusema kuwa – pale wawili au watatu wamekusanyika pamoja kwa jina lake, shetani atakuwa hapo na kwa hiyo kanisa litahitajika kuomba na kuzifunga na kukemea roho chafu kutoka katika kusanyiko lao! Lakini ikiwa tutafanya aina hii ya mambo nje ya aina fulani za desturi zetu tulizo nazo, hapo tutakuwa tukidhirisha kutokuamini katika Mungu na katika neno lake na tutakuwa tunamwabudu shetani kwa yale matendo ya ushirikina ambayo tunayaita ni vita vya kiroho! Ninalifahamu kanisa fulani katika mji ninaoishi, ambako mchungaji wa hapo aliwachukua watu ili kuombea jengo lote la kanisa – kuzifukuza roho chafu ambazo alisema ndizo zilizokuwa zinaishi katika jingo lile na zinapinga kazi ya Mungu sehemu hiyo! Jambo hili ni aina ya kutokuamini na ushirikina, tunaweza kutumbukia humo kwa mafundisho haya ya kisasa!

Vita vya kiroho inatuhusisha kusimama huku tukiwa tumeshika silaha ya imani katika Mungu pamoja na neno lake kinyume na uongo wote, mashutumu na majaribu ya shetani. Hiyo ndiyo inayoelezwa katika Efeso 6 yote. Haihusiki na kuvaa aina fulani ya silaha za kiroho ili kwamba tuweze kupigana mieleka moja kwa moja na aina fulani ya roho chafu au ya kieneo, tukipiga kelele na kukemea katika maombi. Kuhusiana na kupiga kelele na kukasirika kwa ajili ya shetani, ambayo imeenea sana kwa baadhi ya watu siku hizi, yapo maandiko fulani ambayo yanatuelekeza vizuri. Tumekwisha kuona tayari jinsi Yesu alivyoweza kumkabili shetani kule Nyikani. Hakuweza kupata joto na kukasirika kuhusiana na Ibiilisi, ampigie makelele kana kwamba hapaswi kuwepo pale. Pengine tunaona kushangazwa jinsi ambavyo Mungu alivyomwelezea yule shetani kule katika sura ya kwanza na ya pili ya kitabu cha Ayubu. Mungu anamruhusu Shetani aseme maneno yake na anaruhusu mabishano yake na matendo yake – lakini tu ni kulingana na kusudi lake mwenyewe. Mungu yu salama na mwenye uhakika katika haki yake ya umilele. Yeye anatawala katika haki, na kila mmoja kule mwishoni atahukumia kwa haki ya Mungu. Yeye pia ni mwenye mamlaka juu ya mambo ya wanadamu na yeye anayemruhusu shetani kuwajaribu watakatifu wake. Mungu hachanganyikiwi kuhusu shetani – hukumu yake ya mwisho ni yenye uhakika. Shetani anatupwa katika ziwa la moto. Mpaka hapo, shetani anachofanya ni kuzunguka huku na kule kama Simba angurumaye, naye anatafuta kunyang’anya, kuua na kuangamiza. Bado anawadanganya watu na kupinga kazi ya Mungu. Kwa wale wanao mwamini Krsito, nguvu za shetani zimevunjwa naye hana uwezo dhidi yao, ingawaje kama tulivyokwisha kuona. Mungu anamruhusu shetani hatua fulani, lakini yote hiyo ni kwa ajili ya kuwajaribu watu wake ili kwamba imani yao ipate kuwa kama dhahabu! Lakini katika mfano wa hapo juu si Kristo hapa duniani wala Mungu kule mbinguni aliyechemka kwa kumkaripia shetani. Amepewa nafasi na fursa kulingana na hekima yake Mungu mwenyewe na mamlaka zake, lakini kazi za shetani pia hukemewa na kuvunjwa pale anapoingilia kazi ya Mungu ya kuokoa roho kama tulivyokwisha kuona katika Matendo ya Mitume. Sasa ni Yuda anayeandika katika Agano Jipya anatupatia neno la kutuonya kuhusiana na jambo hili. Yuda 1:8-10. Hapa anatuambia kuwa hata malaika mkuu Mikaeli hakutoa mashutumu ya kukemea dhid ya shetani. Sisemi hapa kuwa shetani anayo nafasi maalumu na uwezo ambao yatupasa sisi kuogopa. Hapana! Hapana kabisa! Aliye ndani yetu ni mkuu kuliko yeye aliye nje ulimwenguni.

Lakini ninapenda tuone maandiko yanavyotufunulia kuhusiana na jambo hili na yanavyofundisha. Lengo langu katika kusema haya yote ni kuona kuwa, hatumpatii shetani nafasi kubwa na uwezo katika kufikiri kwetu na ndani ya maombi yetu kwa kumhesabia umaarufu ambao hastahili kuwa nao; au kwa kwenda mbali na maandiko kwa kujaribu kupigana naye na kumkemea au kupambana na roho zitawalazo maeneo (roho za kimaeneo) kama zinavyoitwa! Yuda hapa anaongelea kuhusu watu wanaoongea uovu juu ya mambo wasiyo yajua au wasiyoyaelewa. Na hivyo ndivyo sawa sawa na hawa waandishi wa kisasa na walimu wa kisasa wanavyofanya. Bila shaka roho chafu ni ushetani. Lakini sasa hawa waandishi wa kisasa wanaongea mambo kuhusu hao pasipo kuelewa wanasema nini hasa! Wanatutaka tukazie macho yetu kwa shetani na roho chafu, tukiwapatia uwezo na mamlaka juu ya miji ambayo kwa kulingana na maandiko hawanavyo! Kisha wanatutaka tujihusishe katika mapambano binafsi ya kirogho pamoja na maroho hayo na kukemea dhidi yao katika maombi! Mambo hayo yote yanaenda mbali zaidi na maandiko na pia yanaenda mbali zaidi na yale yote ambayo Mungu ametuagiza.

Sipendi nikupatie kanuni ya jinsi ya kuomba au kutokuomba katika mazingira maalum ambayo utakabiliana nayo mbali ya kuelekeza maandiko halisi na ukweli wa kiroho ambao unapaswa kutulinda katika kuomba kwetu. Pia sisemi kwamba hatuwezi kupiga kelele au kuomba kwa sauti kuu inapohatijika tunapofanya maombezi – inategemea na aina ya maombi. Ninaloandika ninaliandika juu ya kujaribiwa kwetu tupige kelele kwa hasira dhidi ya Shetani kupita kiasi na bila kujali mafundisho ya Biblia na mfano wa Yesu Kristo. Tunaweza kuhakikishiwa kuwa Kristo aliziangamiza kazi zote za shetani juu ya msalaba na kuharibu mamlaka na uweza pale msalabani. Hii inaweza kutufariji tunapoomba kwa Mungu kuhusu mazingira ambayo tunaamini kuwa shetani anapinga kazi ya Mungu, lakini pasipo kujishughulisha na mambo hayo yao yasiyo ya kibiblia ambayo yanahamasishwa na waandishi hawa wa kisasa!

Nimewahi kuwasikia, watu wakisema miaka mingi sasa, “namchukia shetani” hasa kama mtu ametenda dhambi vibaya au ameumia vibaya. Haya, haikusaidia chochote kumchukia shetani kwa ujumla haitoshi na wala sio hoja yenyewe. Hoja hapa ni kwamba iwapo mtu atajikana mwenyewe na kumpenda pamoja na kumtii Mungu. Ile kinachoweza kutusaidia zaidi katika maisha yetu kiroho ni iwapo tunazichukia dhambi na kuipenda haki (Heb 1:9), ikiwa tunamwamini na kumtii Mungu. Tunapaswa kumpinga shetani kwa moyo wetu wote na wala tusikubaliane na mashauri yake ya udanganyifu au matoleo yake ya kujaribu watu. Hii ndiyo njia kuelekea kwenye furaha, amani, na haki. Kutoka katika maandiko ningeweza kusema kuwa, ni jambo jema sana kutokujihusisha mwenyewe na hisia zozote zile kuelekea kwa shetani. Yesu kule nyikani hakupenyeza uso wake mbele kwa hasira yenye dharau na kuanza kumkemea shetani, akirusha ngumi yake hewani! Je tunapaswa kufanya hivyo? Lakini tunaona kuwa shetani hakuwa na uwezo wowowte juu yake, na Yesu alirudi toka nyikani akiwa amejaa nguvu za Roho – baada ya kuwa amepinga vishawishi vya shetani. Ikiwa unapenda kuchukia kitu chochte hapa duniani, basi uichukie dhambi na katika hali ya kuwa hupendi kufanya lolote lile navyo. Na kama tunawaona wengine wanatenda dhambi, basi hebu tumwombe Mungu ambaye ni tajiri wa rehema na neema 1Yoh 5:16. Hebu tumfuate Yesu ambaye alipenda haki na akachukia maasi (Ebr.1:9) ambaye alipinga na kukataa vishawishi vya shetani pasipo kukemea juu yake kwa hasira, na ambaye kama kuhani mkuu huchukua majina yetu mara kwa mara kifuani pake mbele za Mungu katika maombi! Kut 28:12, 29, Heb 7:25. Nasi tuzifuate nyayo zake, Efs. 6:18.

Post a Comment

0 Comments