‘Siri ya
Mafanikio’
Maana ya ‘motivational speaker’ ni msemaji ambaye anawatia moyo
watu na kuwahamasisha wafikie malengo au makusudi yao kupitia kubadilisha
mtazamo wao. Wanawachochea watu watengeneze malengo (goli) kwa ajili ya maisha
yao ya baadaye. Wanafundisha sana juu ya ‘mafanikio’ na wanadai kuwasaidia watu
kuboresha na kufanikiwa katika maisha yao.
Usemi au fikra ‘motivational speaker’ inatoka wapi? Inatokana na
nia na roho ya kizazi hiki ambao hawamjui Mungu. Nyendo au mafundisho haya
yalianza miongoni kwa wasioamini hasa kama miaka 60 iliyopita. Msingi wa
mafundisho haya ni ifuatayo: huhitaji mtu mwingine; huhitaji Mungu au dini;
wewe mwenyewe kama binadamu tayari unao uwezo ndani yako kubadilisha maisha
yako na kutimiza ndoto zako zote na kutekeleza malengo yako yote! Wasemaji hao
wanaahidi watu watafanikiwa katika kila eneo la maisha yao – INATEGEMEA NA
MTAZAMO NA FIKRA ZAO TU! Ni lazima kubadilisha mtazamo wako tu! Kama ukibadilisha
mtazamo wako na fikra zako, yote yatawezekana kwako! Kwa maneno hayo wasemaji
hao (motivational speakers) wanachochea hisia za watu ili waamini waweze
kutekeleza malengo yao! Wanahubiri maisha ya kujitegemea kabisa! Kwa msingi,
wanahubiri wewe ni mungu! Mamilioni wa wasioamini wamefuata ‘injili’ hiyo.
Wasemaji hao wanaandika ‘Self-help’ vitabu, yaani, ‘Jisaidie
Mwenyewe’ vitabu, kama ‘The power of Positive Thinking’, ‘10 Steps to Success’,
‘Achieve Your Goals’, ‘Change your Destiny by Changing your Attitude.’ (‘Nguvu
ya Mtazamo Bora’, ‘Hatua Kumi Kufanikiwa’, ‘Tekeleza Malengo Yako’, ‘Badilisha
Maisha Yako Kupitia Kubadilisha Mtazamo Wako’ nkd.)
Bila aibu yo yote, wahubiri wa kikristo siku hizi wanatumia maneno
haya haya na lugha hiyo hiyo! Ndiyo, wanatumia mistari ya Biblia ambayo
wanadhani inatetea mafundisho yao, lakini kwa kufanya hivyo wanaharibu maana ya
mistari hiyo tu, kwa sababu kimsingi katika mafundisho ya ‘mafanikio’ lengo
lako linapewa kipaumbele cha kwanza na siyo neno la Mungu wala mapenzi ya
Mungu. HILO NI KOSA LA KIMSINGI YA MAFUNDISHO YAO. Ni wazi ni lazima kupanga
mambo kwa ajili ya maisha yetu. Hiyo siyo tatizo. Lakini neno la Mungu na
mapenzi Yake yanapasa yapewe kipaumbele cha kwanza katika yote tunayoyapanga.
Wahubiri hao wanaigia wasemaji wale wasioamini (motivational speakers) kabisa
na kupitia mafundisho hayo wanataka kuwavuta vijana wengi sana, na wanafanya
hivyo! Hasa vijana wa kikristo huvutwa na mafundisho hayo na wanategwa na
udanganyifu huo kwa sababu yanaahidi mafanikio na matekelezo ya malengo (goli)
yao! Tatizo ni lipi basi? Ya kwanza, watu wengi wanaoyafuata mafundisho hayo hawatafanikiwa
kwa sababu mafundisho hayo siyo ya kibiblia. Wanadanganywa tu. Ya pili, kwa
nini wengi wanadanganywa kwa urahisi? Kwa sababu mafundisho hayo yanachochea
mioyoni mwa watu hamu na hata uchoyo kwa mambo ya nje ambayo
yangewapendeza haijalishi kama ni mapenzi ya Mungu au sivyo. Wanasema,
zifuate hatua hizi tu, na utafanikiwa.
Kwenye somo hili nataka kuweka wazi kwamba katika Biblia hakuna
‘motivational speakers’ – hata mmoja! Aidha, Biblia haitumii lugha ya
motivational speakers, haitumii ‘filosofia’ ya watu hao. Mapenzi ya Mungu
huyapewa kipaumbele cha kwanza katika Biblia.
Yesu Kristo hakuwa ‘motivational speaker’!
Tunasoma kwenye Biblia, “…mtu mmoja alimwambia, ‘Nitakufuata ko
kote utakakokwenda.’” Lakini Bwana Yesu hakujibu, ‘Oh! Nafurahi unapenda
kunifuata. Hongera! Kumbe, unavyo vipaji vizuri nami nitakutumia na
utafanikiwa!’ Bwana Yesu akamjibu kwa namna hiyo, “Mbweha wana pango, na ndege
wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake.”
(Luka 9:57,58). Je, unafikiri jibu hili la Yesu lilimpendeza yule aliyejitolea?
Je, maneno haya yalimtia moyo? Kwa maneno haya Bwana Yesu alitaka kumuamsha mtu
huyo aelewe kwa dhati maana ya ‘kumfuata Yesu’! Mtu anaweza kuwa na hamu
kumfuata Yesu bila kuelewa maana yake, bila ‘kuhesabu gharama’! Labda mtu huyo
aliamini Injili ni Injili ya ‘baraka’, yaani, labda akasema moyoni kwake, ‘Ahh,
Mungu atanisaidia sasa, atanibariki, ataniokoa kutoka katika mazingira yangu
mabaya na atayafanya maisha yangu yawe nzuri na atanisaidia kufanikiwa!’ Jibu
la Yesu liliuzima moto wa hamu ya namna hiyo; liliizima hamu yenye tabia ya
kibinadamu kujifaidia! Hapana! Injili sio jambo la kujiendeleza mimi mwenyewe,
kujifurahisha matelekezo ya malengo yangu, kuboresha ‘uwezo’ wangu,
kujitajirisha!
Labda yule aliyetaka kujitolea kumfuata Yesu alifikiri, “Kumbe,
ninavyo vipaji, ninao uwezo mzuri ambazo Mungu angeweza kuzitumia kujenga
mfalme wake duniani!” Au hudhani hivyo? Lakini nilisoma kwenye Facebook mtu
fulani (mkristo?) aliyeweka post ifuatayo kwenye group ya kikristo fulani,
“Mungu anautumaini uwezo wako, basi wewe pia unaweza kufanya vile vile.” Na
watu wengi (wakristo?) waligonga ‘like’! Tunaongea, tunaandika kama Biblia
haipo! Watu hawajali neno la Mungu kabisa! Paulo alitanganza, “Sisi wenyewe
tulikuwa na hukumu ya mauti katika nafsi zetu ili TUSIJITUMAINIE NAFSI ZETU,
bali TUMTUMAINI MUNGU.” (2 Wakor.1:9), na tena, “Maana sisi tu tohara, tumwabuduo
Mungu kwa Roho, na kuona fahari juu ya Kristo Yesu, wala hatuutumainii mwili
(yaani, uwezo wangu mwenyewe).” (Wafil. 3:3).
Wengi wanatangaza, ‘Usikate tamaa! Usikate tamaa! Utafanikiwa.
Ujitumainie nafsi yako! (have confidence in yourself!). Amini katika uwezo wako
na vipawa vyako (believe in your capabilities and gifts!). Songa mbele tu!
Mungu atakusaida kufanikiwa!’ Hayo siyo lugha ya neno la Mungu; hayo siyo
mafundisho ya maandiko. Na kwa nini wanasema mara nyingi ‘kufanikiwa’? Ina
maana ya namna gani? Kufanikiwa katika biashara au kazi yangu? Kwa nini
hawatumii lugha ya Biblia? Kwa nini watu hawa hawaandiki ‘Amini Yesu naye
atakusaidia kushinda dhambi’ au ‘Usikate tamaa! Songa mbele na utaona Mungu ni
Mwaminifu!’ Kwa nini wengi wanapenda na wanapendelea kutumia lugha ya
‘mafanikio’? Kwa nini wanasistiza mambo ya nje tu na siyo mambo ya kiroho?
Katika muktadha huo, Bwana Yesu hakutumia lugha hiyo wala mitume Wake.
Bwana Yesu hatafuti watu ‘wajitoleao’ (volunteers). Anatafuta watu
ambao watatubu kwa ndani sana, kujikana wenyewe na kuchukua msalaba wao na
kutafuta kwanza Ufalme wa Mungu na haki Yake. Mungu anatazamia sisi tuyatafute
mapenzi Yake tu, na siyo kuyajenga mapenzi yetu mweyewe kadiri tunavyopenda,
kadiri ya ‘uwezo’ wetu.
“Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, ‘Nitakufuata; lakini, nipe
ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu.’ (Luka 9:61). ‘Nitakufuata
…lakini kwanza…’. Hamna ‘lakini kwanza’, hamna ‘lakini’. Yesu ni Mwana wa
Mungu! Huwezi kubadili na Mungu. Yesu hakufa kustarehesha maisha yetu! “Yesu
akamwambia, ‘Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa
ufalme wa Mungu.’” (Luka 9:62).
Unatafuta nini?
Yesu “Akamwambia mwingine, ‘Nifuate’.” Haijalishi unalotaka
kufanya au unalopanga. Yesu hakufa kustarehesha maisha yetu au kutimiza
mitazamo yetu, alikufa ili tutimize mapenzi Yake ndani yetu kupitia yetu.
“Akasema, Bwana, nipe ruhusa kwanza niende nikamzike baba yangu.” Lakini Bwana
Yesu hajali mipango yetu, “Akamwambia Waache wafu wawazike wafu wao; bali wewe enenda
ukautangaze ufalme wa Mungu.” (Luka 9:59,60). Neno la Mungu linakuja kwetu kama
neno lenye “nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena
lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani
yake; tena li jepesi KUYATAMBUA MAWAZO NA MAKUSUDI YA MOYO” (Waebr.4:12).
Unaona? Watu wengi wanaweza kuwa watu wajitoleao (volunteers) ambao wanafikiri
uwezo wao, au vipaji vyao, au ‘maono’ yao, au hata hamu yao kumfuata Yesu
zinafaa kwa ajili ya kujenga Mfalme wa Mungu duniani, lakini Bwana Yesu
anachunguza na kugundua makasudi ya kiini ya mioyo yetu! Kama ilivyoandikwa,
“Kalibu ni kwa fedha na tanuru kwa dhahabu, bali BWANA huujaribu moyo.”
(Mithali 17:3). Neno la Bwana linafanya kazi ndani ya mioyo na maisha yetu kama
kalibu na tanuru kutofautishiana kati ya maneno na hamu yetu (na yale
tunayoyadai), na makusudi yetu kweli kweli!
Unaona? Mtu mmoja anasema, ‘Nitakufuata ko kote utakakokwenda.’
Lakini Yesu alimlazimisha atafakari juu ya gharama ya kumfuata Yeye! Hamu ya kufanya
kitu haitoshi! “Kutii ni bora zaidi kuliko dhabihu.” (1 Sam.15:22). Mtu
mwingine alikuwa anajishughulisha na jambo fulani lakini neno la Mungu lilikuja
kwake kukatiza mawazo na maisha yake! Tunapokuja kwake Bwana Yesu, Yeye hajali
mtazamo wangu, au makasudi yangu kwa maisha yangu, au malengo yangu – mambo
hayo yote ya kwangu binafsi siyo muhimu kwa ufalme Wake. Msalaba wa Kristo
uliyasulibisha mambo haya yote ya binafsi. Sina haki kuwa na makasudi yangu
mwenyewe, ndoto zangu za binafsi, kutaka kutekeleza matakwa yangu! Jukumu langu
ni “kutoa mwili wangu uwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu.”
(Warumi 12:1). Kutoka katika dhabihu hiyo (mahali ambapo sitafuti mapenzi
yangu) Mungu ataifufua mapenzi Yake kwa maisha yangu. Ni hatari kwa maisha ya
kiroho ukitegemea hamu au uwezo wako kufanya kitu! Bwana anatazamia utii wetu
na imani yetu na Yeye atatutia nguvu tufanye mapenzi yake.
NAOMBA UNIELEWE VIZURI. Hapo naongea juu ya wahubiri watumiao
mafundisho ya wasioamini (wakati wanadai ni ya kikristo) kuwachochea waumini
watufute ‘mafanikio’ badala ya kufundisha neno la Mungu ili kuwapa waumini
ufahamu juu ya mapenzi ya Mungu kwa maisha yao. SISEMI huwezi kuchagua upendalo
kujifunza juu ya elimu yako. Sisemi ni kosa kuchagua kazi upendayo kufanya!
Mambo haya yote ni maisha tu, ni mambo ya kawaida tu – ila kwa wakristo ni
jambo la kawaida pia kutafuta mapenzi ya Mungu katika mambo hayo yote kwa
sababu ni LENGO letu kumpendeza YEYE katika mambo yote, liwe kubwa, liwe ndogo.
Watu wengi walimfuata Yesu. Je, unafikiri Yeye alikuwa
‘motivational speaker’? Imeandikwa, “Makutano mengi walipokuwa wakifuatana
naye.” Na Yesu alifanyaje? Neno la Mungu linatuambia, “aligeuka, akawaambia,
‘Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na
wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi
kuwa mwanafunzi wangu.” (Luka 14:25,26).
Je, unataka kumfuata?
Je, maneno haya ya Mwana wa Mungu yanakuvuta, yanakuhamasisha
(motivate you) umfuate? Au maneno ya Yesu ni changamoto kwako ambayo
yanakusababisha utafakari na kuchunguza makusudi yako kweli kweli na
kuitafakari gharama ya kumfuata Yesu? Wapi Bwana Yesu anatumia maneno
yafuatayo, “Njoo! Nifuate mimi na utafanikiwa!”, au, “Usikate tamaa. Tengeneza
mtazamo wako tu na utafanikiwa”? Hayatumii maneno haya. Badala yake anaendelea
kuwaambia watu, “Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu,
hawezi kuwa mwanafunzi wangu.” (Luka 14:27). Inawezekana kabisa watu wengi
walimfuata Yesu kwa ajili ya ‘baraka’ na kwa ajili ya miujiza aliyoifanya – na
kama wewe ukifanya hivyo, unakosa sana! Kama ukifanya hivyo, mwishoni utakata
tamaa, au utachukizwa au hata malengo yako ya binafsi yatakukwaza! Kwa maneno
hayo hapo juu, Bwana Yesu alitaka kuweka wazi kabisa ili watu waelewe haitoshi
kabisa kumfuata kwa sababu ya ‘baraka’ au ya miujiza au ya ‘mafanikio.’ Ni
jambo la kuhuzunisha sana wahubiri wengi siku hizi wanatumia – kwa kusudi –
ahadi ya ‘mafanikio’ kuwavuta watu kwa huduma zao na makanisa yao. Wanafundisha
kana kwamba ipo ‘siri’ ya mafanikio, na sasa, eti, ili ufanikiwe katika maisha
yako lazima ufuate mafundisho yao – badala ya kusoma neno la Mungu tu, badala
kuamini neno la Mungu tu, badala ya kulitii neno la Mungu ambalo limeandikwa
kwa wazi katika maandiko. Je, neno la Mungu halitoshi kwao?
Changamoto ya mistari hiyo ya hapo juu ni wazi. Lakini kama
ukimfuata Yesu, aliahidi ‘tutakuwa na uzima, kisha tuwe nao tele’ (Yoh.10:10),
na mambo mengi zaidi. Lakini lengo langu lilikuwa kuonyesha kupitia mistari
hapo juu kuwa Yesu hakuwa motivational speaker.
Tafadhali unielewe vizuri. Udanganyifu wa ‘motivational speakers’
ni kama ifuatayo: wanaichochea kwa maneno yao hamu ya ‘nafsi yako mwenyewe’
upate unalotaka, au ufanikiwe au uwe kitu – na wanaahidi mambo haya yote wakati
wakidai ni ‘mapenzi ya Mungu’ kwa ya maisha yako! ‘Utafanikiwa! Songa mbele tu!
Usikate tamaa! Badilisha fikra zako tu! Utafanikiwa!’ Motivational speakers
wanahubiri mambo yale ambayo watu na hata wakristo wengi wanapenda kuyasikia
kwa sababu hawahubiri msalaba wa Kristo na kujikana, bali wanahubiri njia
kutekeleza makusudi yako mwenyewe ya binafsi, na namna ya kufanikiwa au
kutajirika. Kwa hiyo msingi wa mafundisho haya siyo kuyafuata mapenzi ya Mungu
bali ‘tekeleze malengo yako mwenyewe, ujipendeze nafsi yako mwenyewe.’
Nijalie nijikatize kutoa maelezo zaidi kidogo juu ya lengo la somo
hili: Ni WAZI katika maisha yetu ni lazima tutafakari na kupanga mambo
juu ya mahitaji yetu, juu ya elimu, kazi au biashara zetu. Ni wazi tunapaswa
tusiwe wavivu bali “kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho
zenu; mkimtumikia Bwana” (Warumi 12:11). Hiyo ni jambo la kawaida ya maisha!
Siyo kosa! Msingi na mzigo wa ujumbe huo ni tuyatafute na kuyafuata mapenzi ya
Mungu KATIKA YOTE TUNAYOYAFANYA, na siyo kuyafuata mafundisho (ya wasioamini)
juu ya ‘mafanikio’ ambayo yanatupelekea mahali pa kuacha neno la Mungu na
badala yake kujenga maisha yetu juu ya mawazo ya wasioamini ambao wanatuchochea
tuifuate ‘ndoto’ yetu bila kujali neno wala mapenzi ya Mungu.
Tunapaswa kumfuata na kumwamini Yule aliyesema, “utafuteni ufalme
wa Mungu, na hayo mtaongezewa….Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa
zote. Msiogope basi… Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri
ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu… Umtumaini Bwana
ukatende mema, ….nawe utajifurahisha kwa Bwana, naye atakupa haja za moyo
wako…. Umkabidhi Bwana njia yako, pia umtumaini, naye atafanya….Mtumaini Bwana
kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako
zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni
pako… Shikeni basi maneno ya Agano hili myafanye, ili mfanikiwe katika yote
mfanyayo.” (Matt.12:7,31,31; Wafilipi 4:19; Zaburi 37:3-5; Mithali 3:5-7;
Kumbuk. 29:9).
Zaidi ya hayo, neno la Mungu linalsema, “Basi, ndugu zangu,
nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu IWE DHABIHU ILIYO HAI,
takatifu, ya kumpendeza MUNGU, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe
NAMNA YA DUNIA HII; bali mgeuzwe kwa KUFANYWA UPYA NIA ZENU, mpate kujua HAKIKA
mapenzi ya MUNGU yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” (Warumi 12:1,2).
Sasa, yeye (mtume Paulo) aliyesema, “Na Mungu wangu atawajazeni
kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo
Yesu,” alisema PIA, “Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni FAIDA KUBWA. Kwa
maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na
chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini hao watakao kuwa na mali
HUANGUKA KATIKA MAJARIBU na TANZI, na TAMAA NYINGI ZISIZO NA MAANA, zenye
kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la
mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo
wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi. Bali wewe, mtu wa Mungu,
UYAKIMBIE MAMBO HAYO; UKAFUATE haki, utauwa, imani, upendo, saburi, upole.” (1
Tim.6:6-11). Sasa je, unadhani mtume Paulo alikosa aliposema maneno hayo kwake
Timotheo? Jibu, moyoni mwako tu. Je, unadhani mtume Paulo kwa maneno yake
anawazuia waumini wasiboreshe maisha yao? Jibu moyoni mwako. Je, unadhani,
mtume Paulo anataka waumini wabaki hali ya unyonge? Je, Paulo alikosa au
hakukosa kwa maneno yake kwake Timotheo? Jibu moyoni mwako – na kama unajibu
‘hakukosa’, unapaswa kutengeneza mtazamo wako, fikra zako na moyo wako uzifanye
sawa na Paulo.
Kama tukiongea juu ya maisha yetu, na maisha yetu ya baadaye, kwa
nini kwa kiwango kikubwa sana walimu wa ‘mafanikio’ hawanukulu mistari hiyo ya
hapo juu katika mafundisho yao?
Wao wanaofundisha ‘mafanikio’ KWA UJUMLA ni nani? Kwa uzoefu wangu
wanaishi mjini, siyo kikijini. Kwa ujumla (siyo wote) ni watu wenye elimu, hata
elimu ya juu. Kwa ujumla ni watu wanaoishi katika mazingira ambapo FURSA ya
kuboresha maisha yao ni zaidi sana kuliko vijijini! Kwa ujumla, sio ‘siri ya
mafanikio’ ambayo inawasaidia kuboresha maisha yao, ni fursa ambayo mazingira
na familia yao inawatoa! Naongea kwa ujumla. Sisemi kuwa mvivu ni sawa. Hapana,
hata kidogo! Lakini wapo wengi vijijini ambao wanayo bidii, na hamu na akili kuboresha
maisha yao kadiri wewe unavyokuwa nayo! Nilikutana nao. Lakini fursa ya
kuborehsa maisha yao inakosa kwa kiwango kubwa kuliko mjini. Nashangaa sana wao
wenye elimu (hata ya chuo kikuu) mjini HAWAELEWI JAMBO HILI LA MSINGI la
maisha. Ningeweza kuthibisha ninayoyasema. Wewe unayefuata mafundisho ya ‘siri
ya mafanikio’, njoo pamoja nami. Nitakupelekea kijiji mmoja. Kaa pale kwa mwezi
moja, au mwezi sita, au miaka sita. Utachoshwa. Hutafanikiwa. Mafundisho yako
hayatabadilsha wala kuyagusa maisha ya waumini kwa sababu tayari wengi – hasa
vijana – wanayo hamu na bidii na akili kuboresha maisha yao lakini wanakosa
fursa kutokana na mazingira yao. SIYO jambo la kutokuchukua fursa waliyo nayo.
Hapana. Inatokana na upungufu wa fursa. USIWALAUMU ndugu zako (kupitia ujinga
wako) kwa kusema wao ni wavivu, au hawana hamu wala bidii kuboresha maisha yao,
au lazima wabadili mtazamo wao. Ni wazi huwajui. SISEMI maisha ya mtu fulani
hayawezi kubadilika au lazima abaki yale yale. Hapana. Sisemi hakuna awezaye
kuboresha maisha yake, ila mafundisho yako ya ‘mafanikio’ na ‘kubadili mtazamo
wako tu’ kwao, hayatawasaidia – unadhihirisha ujinga wako tu juu ya maisha yao
na juu ya Biblia!
Ni rahisi. Tunalo neno la Mungu. Wapi katika Agano Jipya mitume
waliandika juu ya maskini, ‘badili mtazamo wako tu na utafanikiwa’.
(Wanafundisha dhidi ya uvivu na sisi sote tunakubaliana na hiyo). Wapi? SISEMI
hali ya mtu fulani haiwezi kubadilika (naomba usinisingize), lakini toa mstari
mmoja kwenye Agano Jipya ambao unasema yale yale unavyosema, yaani, ‘badili
mtazamo wako tu na utafanikiwa, utajitoa kutoka katika umaskini.’ Toe tu. Jibu
ni rahisi – hamna hata mstari mmoja wala mafundisho ya namna hiyo katika Agano
Jipya na kimsingi katika Biblia nzima.
Kwa nini nimeandika somo hili? Kwa sababu kimsingi mafundisho ya
‘mafanikio’ yanawaongoza watu ‘kuanguka katika majaribu na tanzi na tamaa
nyingi zisizo na maana ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu.’ Basi,
mambo hayo ni muhumu sana kwa ajili yetu! Najua watu wale wanadai wanataka
kuwasaidia waumini kuboresha maisha yao – lakini huwezi kuwasaidia kwa
kutokujali neno la Mungu. Katika mafundisho yote ni afadhali kulitumia neno la
Mungu kwa ajili ya maisha ya waumini.
Tuendeleeni sasa na mafundisho. Wengine wanafundisha ni lazima
kujipenda mwenyewe kabla ya hujafanikiwa! Hayo ni mafundisho na saikoloji ya
wasioamini. Na wahubiri wanapotosha neno la Mungu kwa kunukulu mistari kama
Mtt.22:39, “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” Sasa, maneno hayo
yanamaanisha? Ina maana ninajipenda mimi mwenyewe, ninajibusu, ninajitazama
mwenyewe katika kioo nikisema, “Mimi ni bora, mimi ni mtu wa ajabu! Jinsi
ninavyonipenda!” Hasha! Biblia inafafanua Biblia. Mungu apewe sifa! Kama
tunasoma Warumi 13:9 na Wagalatia 5:14, tunaona “Mpende jirani yako kama nafsi
yako” ina maana USIWATENDEE WATU VIBAYA kwa sababu siyo tabia ya mtu
kujitendea vibaya! Hiyo ni maana ya ‘kupenda nafsi yako.’ Kwa mfano, ukijisikia
kiuu, utakunywa maji, chai au soda! Ni tabia ya mtu kujitunza na kujilinda
mwenyewe. Kwa hiyo katika Warumi 12:20 imeandikwa, “Lakini, Adui yako akiwa na
njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya
moto kichwani pake.” Mstari ule hapo juu unahusu MATENDO YETU kwao wengine!
Sasa, kwa nini wanafundisha ni lazima ‘kujipenda mwenyewe’? Kwa
sababu wanajua watu na hata waumini wanaweza kujisikia hawafai, na kujichukia
mwenyewe. Lakini njia ya kutoka katika hali ya hiyo siyo ‘kujipenda mwenyewe’!
Kujisikia wewe hufai ni kazi ya shetani moyoni mwako – njia ya kutoka katika
hali hiyo ni kuacha kutokuamini; usipokee uongo wa shetiani; ‘kuwa hodari
katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Kuvaa silaha zote za Mungu, mpate
kuweza KUZIPINGA HILA ZA SHETANI; kuitwaa NGAO YA IMANI, ambayo kwa hiyo
mtaweza kuizima MISHALE YOTE yenye moto ya yule mwovu; KULIAMINI pendo alilo
nalo Mungu kwetu sisi. Mwamini Mungu aliyesema, ‘Ni nani atakayewashitaki
wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia
adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa…naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena
ndiye anayetuombea.” Kwa maneno hayo na mengi mengi zaidi ya maandiko tunaweza
kuwatia moyo waumini! Sasa je, kwa nini wale wanaofundisha ‘mafanikio’ hawajali
neno la Mungu na badala yake hufundisha mambo matupu na ya udanganyifu kama
‘kujipenda mwenyewe’?
Ninayo raha moyoni mwangu siyo kwa sababu ‘ninajipenda mimi
mwenyewe’ (Hasha!), bali kwa sababu Mwokozi wangu alinipenda na alikufa kwa
ajili yangu; alinisamehe dhambi zangu zote; alinisafisha kwa ndani na aliweka
Roho yake ndani yangu kunifanya niwe mtoto Wake, ‘alinibariki kwa baraka zote
za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo’; na mambo mengi zaidi!
Na Yeye ni Yule anayenitia moyo wangu! Sitafuti ‘mafanikio’. Sitafuti kujipenda
mwenyewe (Hasha!). Siamini katika mimi mwenyewe (Hasha!). Siweki tumaini langu
kwa mimi mwenyewe (Hasha!). I don’t believe in myself – this is idolatry. I
don’t trust in myself – this is rebellion against God. Namwamini Mungu. Bwana
ndiye tumaini langu! Bwana asifiwe! Namtafuta Yeye ili nimjue Yeye!
Mpendwa msomaji, labda unafikiri ninakwenda kupita kiasi katika
ninalosema! Hapana. Mhubiri maarufu mmoja wa Tanzania aliwasisitiza waumini
waamue kubadilisha mtazamo wao kwa kusikia yale TU ambayo
yatajenga ubora wa maisha yao ya baadaye; akawasisitiza watamani
kusikiliza wale watu ambao wamefanikiwa, akidai ‘Imani chanzo chake ni
kusikia’. Aliwachochea waumini watengenze goli yao, goli ya achievement akiwauliza
wanataka kuwa nani, kufika wapi. Aidha, aliwaambia wachukue kalamu na daftari,
kuchora kila saa, mwundo wa serikali yao ya kampuni, namna ya wanataka
kuendesha biashara zao, na kuweka pembeni na kurudia tena na tena mpaka
wametekeleza lengo lao!
Huo ni mfano wa ‘motivational speaker’. Unapata mafundisho hayo
wapi kwenye Biblia? Hayapo. Ni injili ya kujipendeza, ya kujitegemea, kuboresha
maisha yako ya nje. Haya ni mafundisho ya saikolojia ya wasioamini wapendao
kuboresha maisha yao (bila Mungu) kwa kubadilisha mtazamo wao. Wamefundisha
vivyo hivyo (kwa miaka mingi) na wametumia maneno yale yale. Na mhubiri huyo
anatumia lugha yao asilimia 100 bila kujisikia aibu!
Inawezekana mhubiri huyo anafundisha neno la Mungu wakati
mwingine, lakini hapo anakosea sana. Kwa maneno yake hapo juu anawapeleka watu
mbali na neno la Mungu na anawasababisha kuacha njia na nia ya Yesu Kristo.
Alisema kwamba ‘Imani chanzo chake ni kusikia.’ Wazo hili peke lake siyo
kweli! Analighoshi neno la Mungu. Kujenga imani unahitaji ‘neno la
Mungu’. Biblia ianasema yafuatayo, “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na
KUSIKIA HUJA KWA NENO LA MUNGU.” (Warumi 10:17). Unaona? Aliondoa maneno ‘na
kusikia huja kwa neno la Mungu’. Na ndiyo kweli, yeye hahubiri neno la Mungu
hapo, badala yake anawalisha waumini na mawazo ya wasioamini na saikilogia ya
ulimwengu huo. Anachochea wakristo watengenze wenyewe goli yao. Wapi anataja
mapenzi ya Mungu? Wapi anasema ‘tujitoe miili yetu iwe dhabihu iliyo hai,
takatifu, ya kumpendeza Mungu.’ Wapi anasema, ‘tamani kusikiliza maneno ya
Mungu’ au ‘Ishi kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.’ Hamna! Badala
yake anachochea mioyo ya waumini wawe na nia ya kujipendeza wenyewe, kuweka
malengo ambayo yataboresha maisha, yaani, biashara zao. Kwa kufanya hivyo,
anapotosha neno la Mungu na anapotosha watu. “Unataka kuwa nani wewe?” Swali
hilo livutalo kiburi na kujitegemea tu! ‘Injili hiyo nyingine’ inataka
kunichochea kutengeneze goli yangu kwa kubuni namna gani mimi nataka nifike
mahali. Kumbe, sasa wewe ni bwana wa maisha yako!
Kama ukipenda kufanya semina ya uchumi na biashara, fanya semina
hiyo kwa kuitumia lugha inayohusu masomo hayo; usipelekee neno la Mungu katika
mafundisho yako ya ‘mafanikio’ kana kwamba yanakubaliana.
Najua, ni kweli, kila kazi au biashara inahitaji utaratibu wake na
mpango wake, lakini hilo ni jambo la kawaida tu! Na Mungu anaweza kuibariki
kazi yako na hata biashara yako – lakini siyo kwa njia ya kupotosha neno la
Mungu na kuchanganya neno la Mungu na mafundisho ya wale wapingao Mungu, siyo
kwa njia ya kuchochea kujipendeza, uchoyo na hata majivuno. Mafundisho ya neno
la Mungu ni tofauti kabisa,
“Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani
na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; WALAKINI HAMJUI
YATAKAYOKUWAKO KESHO. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa
kitambo, kisha hutoweka. Badala ya kusema, BWANA AKIPENDA, tutakuwa hai na
kufanya hivi au hivi.” (Yakobo 4:13-15).
Hamna ‘Bwana akipenda’ katika mafundisho ya mhubiri yule hapo juu,
hamna wazo la ‘mapenzi ya Mungu’. Badala yake waumini wanachochewa kutengeneza
malengo ya kuboresha maisha yao kana kwamba ni ‘mapenzi ya Mungu’, au hata
kutokujali mapenzi ya Mungu kabisa. Kwa nini ninaandika somo hili? Kwa sababu
inanihuzunisha sana kwamba vijana wengi wanadanganywa na ‘motivational
speakers’ wa namna hiyo. Wanasukumwa kutengneza malengo (goli) yao wenyewe na
wahubiri hao, lakini kwa wengi malengo yao hayatatekelezwa kwa sababu
mafundisho ya namna hiyo hayatokani na Biblia; wengine watawaambia wasikate
tamaa lakini mwishoni watakata tamaa kwa sababu haya yote ni mambo matupu, ni
upuuzi. Inawezekana wengine wataacha kumfuata Bwana. Na wahubiri hao wanachukua
wajibu kwa ajili ya hiyo. (Kati maelfu mengi inawezekana wengine watafaulu,
lakini watafaulu kwa sababu maisha ni maisha, siyo kwa sababu mafundisho hayo
yanatokana na Mungu – ni jambo la kawaida tu kwamba kwa juhudi na uwezo wetu
tunawezekana kufaulu.)
Yesu alifanya muujiza. Aliwalisha waume elfu tano kutokana na
mikate mitano na samaki wawili. Ndipo tunasoma, “Kisha Yesu, hali akitambua ya
kuwa walitaka kuja kumshika ILI WAMFANYE MFALME, akajitenga, akaenda tena
mlimani yeye peke yake.” (Yoh.6:15). Kwa nini Bwana Yesu alijitenga? Inaonekana
kuwa nafasi ya ajabu awe mfalme juu ya watu! Hapana! Watu wale walitaka
kumfanya Yesu mfalme KWA AJILI YA FAIDA YAO TU ili wapate baraka za kimwili au
za nje tu! KWA SABABU YA HIYO, waumini wengi wa siku hizi wanapenda sana
‘motivational speakers’! Vivyo hivyo kama wayahudi walipenda kumfanya Yesu
mfalme wao! Msingi ni kujipendeza na siyo kujikana! Labda walisema, “Kumbe!
Anafanya muujiza! Hatutahitaji cho chote tena! Yeye atatubariki kupita kiasi na
sisi tutafanikiwa tu! ATABADILISHA MAZINGIRA YETU! Ataondoa maadui zetu Warumi!
Ataboresha maisha yetu! Biashara yetu itafanikiwa, na yote tulilolitaka,
yametimizwa! Twende tumfanye mfalme!” Je, na wewe unataka mwokozi wa namna hiyo
awe mfalme wako? Kama ni hivyo, huwezi kumfuata Mwokozi Yesu Kristo! Huwezi
kuwa mwanafunzi Wake – humjui. Yesu alikataa kabisa kuwa mfalme juu ya msingi
wa kujipendeza kwa watu! Alijitenga na akaenda mlimani peke Yake. Je, utamfuata
pale, pale jangwani, mlimani, pale ambapo hakuna cho chote ila Yesu tu na
msalaba wake? Je, Yesu Mwenyewe tu anatosha kwako? Tunaimba, “Wewe tu ndiwe
utoshaye.” Je, ni kweli kwako kila siku? Unataka nini? Unatafuta nini?
Bwana Yesu, Yeye aliye na macho yake kama mwali wa moto, huangalia
na kuchunguza makasudi (motives) yetu kweli kweli yaliyofichwa ndani sana ya
mioyo yetu! Yesu siyo ‘motivational speaker’. Watu wanaweza kusema hivi na
hivi, wanaweza kuwa na hamu kwa ajili hivi na hivi, hata kumfuata Yeye, lakini
Yesu anachunguza makusudi kweli kweli ya mioyo yetu! Yesu alisema, “Amin, amin,
nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna
uzima ndani yenu.” (Yoh.6:53). Baada ya kusema haya, imeandikwa, “Kwa ajili ya
hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma.” (Yoh.6:66). Wanafunzi
hawa walikwazwa na mafundisho ya Yesu; walisema, “Neno hili ni gumu, ni nani
awezaye kulisikia?” (Yoh.6:60). Labda walifikiri kupitia mafundisho ya Yesu
hawatafanikiwa kuwavuta watu! Labda waliondoka kumtafuta mhubiri mwingine
atakayefundisha mambo yale ambayo watu wanapenda kusikia na awezaye kufanikiwa
kujenga ‘mega-church’! Je, Bwana Yesu alijaribu kuwashawishi warudi? Hapana.
Yesu hakupaza sauti kuwatia moyo kwa kusema, ‘Rudini kwangu tu! Nitayaeleza
yote! Hata nitawajulisha siri ya mafanikio!’ Badala yake, Bwana Yesu aliwauliza
mitume waliobaki, “Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka?” Unaona? Maneno ya Yesu
yanaingia mioyo yetu moja kwa moja kuuliza, “Unataka nini?” Yesu hatafuti
kuwakusanya watu kujenga ‘umaarufu’ wake! Kwa maneno yake na kazi yake katika
maisha yetu, Yesu Kristo anachunguza chunguza mioyo yetu mpaka makasudi yetu ya
kiini kabisa yamefunuliwa. Wale watu ambao wanatengeneza ‘goli’ lao la binafsi
kutokana na mafundisho ya ‘motivational speakers’ wanatayarisha njia ambayo
inaweza kuwakwaza, na mwishoni, kuwasabibisha warudi nyuma!
Kwa nini wasemaji/wahubiri hao hawawalishi waumini kwa neno la
Mungu? Imeandikwa, “Njia zote za mwanadamu huonekana sawa kwake, bali BWANA
huupima moyo.” Na tena, “Njia zote za mtu huonekana safi machoni pake mwenyewe,
BALI MAKUSUDI HUPIMWA NA BWANA.” (Mithali 21:2; 16:2). Hili ni kosa kubwa la
wahubiri hao, yaani, wanawachochea waumini kutengeneza njia zao ambazo
huonekana sawa machoni pao mwenyewe! Na wanaendelea kukosa zaidi kwa kudai
‘mbinu’ hiyo inaitwa ‘imani’ au ‘maono’! Lakini siyo imani, siyo ‘maono’, siyo
mbinu– ni mchezo wa mawazo tu, ni mchezo wa saikolojia. Wahubiri hao
wanawasukuma watu kucheza na mawazo yao tu. Kama wakitaka kuongelea maisha yetu
ya baadaye, kwa nini hawatumii neno la Mungu,
“MTUMAINI BWANA kwa moyo wako wote wala USIZITEGEMEE AKILI ZAKO
MWENYEWE; katika njia zako zote MKIRI YEYE, naye ATAYANYOOSHA MAPITO
YAKO. Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe, mche BWANA ukajiepushe na
uovu.” (Mithali 3:5-7).
Unaona? Neno la Mungu linakuongoza kumtegemea Mungu kabisa, siyo
mitazamo yako, au hata ‘maono’ yako ya binafsi kwa maisha yako ya baadaye!
Huhitaji ‘kukiri maono’ yako kila wiki, au kila mwezi, au kila mwaka ili
yatimizwe! Huhitaji kutoa jasho kwa sababu unajaribu jaribu kuamini Mungu
atatekeleza maono yako au malengo yako! Neno la Mungu linaondoa mzigo huo huo,
yaani, “Nitatengenza goli langu…nitaamini, sitakata tamaa…nitakiri goli yangu,
sitashindwa…nitashika maono yangu mpaka yatimizwe, sitakata tamaa, sitakata
tamaa, sitakata tama…” Lakini mwishoni wengi wanakata tamaa! Kinyume chake
Mungu anakuongoza uingie katika raha Yake na pumziko Lake! Bwana asifiwe! Ni
Habari Njema – siyo jasho la akili zetu! Ujumbe wa kutia moyo ni huo – Mtumaini
Bwana kwa moyo wako wote; mkiri Yeye katika njia zako zote! Hiyo ni njia ya
imani. Hiyo ni njia rahisi mno! Hiyo ni njia ya baraka bila shaka! Tukijitoa
Kwake na kuwa sikilivu, Yeye ni mwaminifu na ataipima mioyo yetu na makusudi
yetu, na Yeye Mwenyewe atayanyoosha mapito yetu! Lakini hiyo haimaanishi njia
Yake kwa ajili ya maisha yako ni sawa na ile uliyoitaka wewe! Kama Bwana Yesu
alimwambia Petro, “Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na
kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine
atakufunga na kukuchukua usikotaka.” Lakini kama tukimpenda Mungu kuliko
malengo yetu, kama tukiyatafuta mapenzi Yake na siyo ya kwetu, haitakuwa ngumu
– itakuwa baraka kubwa tu! Kama Bwana wetu alisema, “Njoni kwangu, ninyi nyote
msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami NITAWAPUMZISHA.Jitieni nira yangu,
MJIFUNZE KWANGU; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi MTAPATA
RAHA nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”
(Mathayo 11:28-30).
Bwana Yesu hakuhubiri ‘injili ya baraka’, yaani, uje kwangu nami
nitaboresha na kustarehesha maisha yako na utafanikiwa katika kila kitu! Yule
mwanamke Msamaria alitaka Yesu amrahisishie na kustarehesha maisha yake
akisema, “Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, WALA NISIJE HAPA KUTEKA.” Yule
mwanamke hakuelewa maneno ya Yesu Kristo. Msamaria alifikiri juu ya mambo ya
kimwili tu. Alitaka karama ya Mungu kwa ajili ya faida yake mwenyewe tu. Bwana
Yesu hakufa msalabani kubadilisha au kuboresha mazingira yako, bali
kukubadilisha wewe kwa ndani sana kabisa haijalishi mazingira ulipo! Kama vile
Paulo alivyosema, “nimejifunza kuwa radhi na hali yo yote niliyo nayo.” Na
wewe? Je, motivational speakers wanakufundisha uwe radhi na hali yo yote uliyo
nayo? Au unaweza kuwa radhi tu kama malengo yako yakifanikiwa? Wewe unataka
nini?
Bwana Yesu alipowajulisha mitume wake kwamba atakufa kwa udhaifu,
Petro alimchukua Yesu na akamkemea! Kumbe! Jambo la ajabu! Mwanaadamu anamkemea
Mungu! Petro hakuweza kuvumilia kamwe wazo la udhaifu, kutokufanikiwa – “Mwana
wa Mungu atakufa msalabani! Haiwezekani!” Yesu akamwambia Petro, “Nenda nyuma
yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana HUYAWAZI YALIYO YA MUNGU, BALI YA WANADAMU.”
Maneno mazito sana! ‘Motivational speakers’ (wale wanaowasukuma wasikilaji wao
kutengeneza malengo yao ya maisha ya baadaye) hufanya vivyo hivyo, yaani, kwa
msingi hawayawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu – na wanajaribu ‘kumtumia’
Yesu kutimiza malengo yao wenyewe, vile vile Petro alivyotaka Yesu ajenge
mfalme Wake duniani sawasawa na njia na malengo yake! Yesu aliendelea kuwaambia
Petro na wanafunzi wake wote,
“Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike
msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu ATAKAYE KUIOKOA NAFSI YAKE, ATAIPOTEZA; na
mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona. Kwani atafaidiwa nini
mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini
badala ya nafsi yake?” (Math.16:23-26). Bwana Yesu alikufa msalabani kutusamehe
dhambi zetu na kutuweka huru mbali na dhambi, kwa hiyo, “alikufa kwa ajili ya
wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya NAFSI ZAO WENYEWE, bali KWA
AJILI YAKE YEYE aliyekufa akafufuka kwa ajili yao.” (2 Wakor.5:15). Hilo ni
kusudi la Mungu kwa ajili yako na yangu.
Na je. mtume Paulo alikuwa ‘motivational spealer’? Sidhani, hata
kidogo. Nia ya Paulo na makasudi yake yalikuwa ya namna gani? Paulo alisema,
“Niliazimu nisijue neno lo lote kwenu ILA YESU KRISTO, NAYE
AMESULIBIWA.”
Bwana asifiwe sana! Tunahitaji wahubiri wa namna hao siku hizi!
Anaendelea,
“Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima
yenye KUSHAWISHI AKILI ZA WATU, bali kwa dalili za Roho na za nguvu, ILI IMANI
YENU ISIWE KATIKA HEKIMA YA WANADAMU, bali katika nguvu za Mungu.” (1
Wakor.2:2-5).
Lazima ilimhuzunisha Paulo kuandika maneno hayo, “..sina mtu
mwingine (kama Timotheo) mwenye NIA MOJA nami, atakayeiangalia hali yenu KWELI
KWELI. Maana WOTE WANATAFUTA VYAO WENYEWE, sivyo vya Kristo Yesu.” (Wafilipi
2:20,21). Kama ilivyokuwa siku za Paulo, ni vivyo hivyo siku hizi – wahubiri
wengi ‘wanatafuta vyao wenyewe, sivyo vya Kristo Yesu’. Kwa maisha yake ya
kiroho Paulo anatangaza, “…NATENDA NENO MOJA TU; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia
yaliyo mbele; nakaza mwendo, NIIFIKILIE MEDE YA THAWABU YA MWITO MKUU WA MUNGU
KATIKA KRISTO YESU. Basi sisi tulio wakamilifu na TUWAZE HAYO.” (Wafilipi
3:13-15). Je, lengo lako na lengo langu, ni lile lile? Anasema, ‘tuwaze hayo.’
Jinsi ‘utakavyofanikiwa’ bila kuwa na nia ya Paulo, bila ‘kuwaza hayo’?
Hili ni neno la Mungu. SASA najisikia huru kukutia moyo, mpendwa
msomaji, kufuata nia na makasudi ya Paulo. SASA unaweza kwa usalama kabisa
kutengeneza lengo lako! Kwa Paulo, kumjua Yesu kulikuwa ya thamani na muhimu
zaidi kuliko yote nyingine, “nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya
uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake
nimepata hasara ya mambo yote NIKIYAHESABU KUWA KAMA MAVI ili nipate Kristo.” (Wafilipi
3:8). Je, tunaweza kusema yale yale, yaani, tunayahesabu yote kuwa kama mavi
ili tupate Kristo? Je, hiyo ni nia yetu, mtazamo wetu, lengo letu? Hiyo
haimaanishi mambo yote yenewe si kitu; inamaanisha mambo yote nyingine
yanaonekana kama mavi kwangu KUYALINGANISHA NA KUMJUA YESU! Unaweza kusema
hayo?
Tena Paulo anasema, “Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa;
katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona
njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye
nguvu.” Je, na sisi tunaweza mambo yote katika Yeye atutiaye nguvu? Au tunaweza
kumsifu Mungu wakati malengo yetu ya binafsi yanapotimizwa tu au tunapofanikiwa
tu?
Kama tunataka kutengenza mwelekeo wetu au nia yetu, tunalo neno
jema kabisa,
“Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia
ndani ya Kristo Yesu, ambaye …alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa
namna ya mtumwa, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya
msalaba.”
Kwa hiyo Paulo alisema, “Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo,
na kufa ni faida.” (Wafilipi 1:21).
Badala ya kuongea sana juu ya ‘lengo lako, kusudi lako duniani’,
naamini ni muhimu zaidi sana kabisa kuliza, ‘Lengo la Mungu kwa ajili
yangu ni nini?’ Lengo la uwepo wetu duniani ni nini? Jibu ni rahisi na wazi.
Siyo siri. Toka mwanzo Mungu alitudhihirisha, “Mungu akasema, Na TUMFANYE MTU
KWA MFANO WETU, KWA SURA YETU.” (Mwanzo 1:26). Na kupitia kifo na ufufuo wa
Mwanwe, Mungu amelitekeleza LENGO LAKE, yaani, ili tuzaliwe toka juu, kuzaliwa
na Mungu! Ili Yesu Kristo aishi ndani yetu, tuyadhihirishe maisha Yake duniani!
(2 Wakor.2:15’ 4:10). “Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu
asili WAFANANISHWE NA MFANO WA MWANA WAKE, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza
miongoni mwa ndugu wengi.” (Warumi 8:29). Lengo la Mungu ni kuwa na watoto kwa
mfano Wake, waliozaliwa na Roho Yake. Kwa nini ‘ametukirimia ahadi kubwa mno na
za thamani’? Lengo la Mungu ni nini? Ni wazi – ‘ili kwamba kwa hizo TUPATE KUWA
WASHIRIKA WA TABIA YA UUNGU.’ (2 Petro 1:4). Kwa ajili ya lengo lipi Mwana wa
Mungu alikuja? Ni wazi, ‘Kwa KUSUDI HILI Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili
azivunje kazi za Ibilisi’ ndani yako na ndani yangu! Mungu apewe sifa! Ujasiri
wetu katika siku ya hukumu ni nini? Tumefanikiwa? Hapana. “Katika hili pendo
limekamilishwa kwetu, ili tuwe na ujasiri katika siku ya hukumu; kwa kuwa, kama
yeye alivyo, ndivyo tulivyo na sisi ulimwenguni humu.” (1 Yoh.4:17). Je,
ulitaka kujua lengo lako hapo ulimwenguni?
Huo ni mwito mkuu. Hilo ni kusudi kuu la Mungu. Ndiyo, kuna elimu,
na kazi, na biashara, na familia, na nyumba, na mwito, nkd, lakini mambo hayo
yote yatapata nafasi yake kwa wakati wake kama tukijenga maisha yetu juu ya
mwamba, Yesu Kristo.
Mungu ameshaitayarisha njia kwa ajili yako na mimi. ‘Maana tu kazi
yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali
Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.’ (Waefeso 2:10). Jambo la ajabu!
Paulo anatangaza, ‘Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi
pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa KWA
KUSUDI LAKE.’ (Warumi 8:28). Je, ninajishughulisha na kulitimiza lengo langu?
Paulo anasema, “UTIMIZENI WOKOVU wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.” Paulo
anaendelea kutuambia kwa nini tunapaswa kufanya hivyo, “Kwa maana ndiye MUNGU
ATENDAYE KAZI NDANI YENU, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa KULITIMIZA KUSUDI
LAKE jema.” (Wafilipi 2:12,13). Unaona? Tayari Mungu anatenda kazi yake ndani
yako kulitimiza kusudi LAKE! Ni afadhali kujishughulisha na kulijua kusudi lake
kwa maisha yako kuliko kujaribu kutengeneza kusudi au lengo lako.
Kusudi la maisha ya milele ni nini? Ni wazi,
“Na uzima wa milele NDIO HUU, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa
kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.” (Yoh.17:3).
Kwa hiyo, “Bwana asema hivi, Mwenye hekima asijisifu kwa sababu ya
hekima yake, wala mwenye nguvu asijisifu kwa sababu ya nguvu zake, wala tajiri
asijisifu kwa sababu ya utajiri wake; bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii,
ya kwamba ANANIFAHAMU MIMI, NA KUNIJUA, ya kuwa mimi ni Bwana.” (Yeremia
9:23,24).
0 Comments