VITA VYA KIROHO
: ROHO ZITAWALAZO MAENEO
Katika makala hii tutaangalia mafundisho yanayohusiana na kile
wanachokiita “Roho za Kimaeneo”. Kulingana na mafundisho hayo, wanadai kuna
roho chafu maalum ambazo zinatawala jamii, vijiji, miji, jiji au hata nchi
nzima. Hiyo ina maana kwamba, roho hizo zinatawala katika eneo zima kulingana
na jiografia ya eneo lenyewe; na hivyo huitwa “Roho za Maeneo”. Inaendelea
kufundishwa zaidi kwamba eti hizi roho za maeneo zanao uwezo na mamlaka ya
kuwabana watu katika giza, vifungo na dhambi kulingana na jiografia ya eneo lao.
Kimsingi, zaidi ya hilo, hawa wanaohamasisha mafundisho hayo, wanatuambia
kwamba hizi roho za maeneo zinao uwezo wa kushikilia jamii ndogo au miji kiasi
kwamba Injili peke yake haiwezi kufaa, kupata kuingia wala kupendwa au
kuenea katika eneo hilo hadi hapo hizi roho za kimaeneo zitakapotambulikana
na kisha zikafungwa, zikazidiwa nguvu pamoja na kukemewa kwa njia ya
maombi. Wanafundisha kwamba watu hawawezi kumjia Bwana, wakaokolewa na
kukombolewa kutoka katika dhambi, giza, pamoja na vifungo mbalimbali, kwa idadi
kubwa mpaka kwanza hapo tutakapotambua na kisha kuzifunga na kukemea
nguvu za roho hizo za kimaeneo. Hivyo ndivyo wanavyosema na kuwafundisha watu.
Hiki
ndicho kidokezo cha mafundisho yao kwa lugha rahisi kadiri iwezekanavyo, na
nina hakika kwamba utakubali kuwa ikiwa mafundisho haya ni ya kweli, basi ni ya
umuhimu mkubwa. Kuenea kwa Injili pamoja na kuokolewa kwa watu kunategemea
ufahamu na matumizi ya mafundisho haya, ikiwa mafundisho hayo ni ya kweli!
Jambo hili haliwezi kuwa swala la jinsi mtu aonavyo au tafsiri ya kibinafsi,
kwa sababu litaathiri ufahamu wetu kuhusiana na jinsi Injili ilivyo, pamoja na
lile alilolifanya Yesu pale Kalvari.
Kama
ilivyo katika zile makala nyingine zilizopita, napenda kwanza niangalie
yale ambayo Maandiko yanavyosema na kufundisha. Kwa hivyo, kwa muda huu,
hatutaangalia Maandiko ambayo watu wanadhani wamepata kuyaona mambo hayo
yakifundishwa. Jambo hili ni la msingi na lenye uzito mkubwa kiasi kwamba
hatuwezi kuyaachia kwenye ubunifu au hisia za kibinadamu tu. Tunachotafuta ni
maandiko ambayo mambo haya yanafundishwa dhahiri na kutajwa bayana.
Mambo
haya yanafundishwa wapi ndani ya Agano Jipya?
Kwa
jibu la urahisi na la ujumla kuhusiana na habari hiyo hapo juu ni – “Hakuna
popote!” Hatuyapati mahala popote katika Agano jipya, mafundisho haya yahusuyo
kutambua na kuzifunga roho za kieneo!
Yesu
hakutumia au kufundisha mbinu hii.
Hakuna
mahali popote
tunaposoma kuwa Yesu aliibainisha roho iliyokuwa ikitawala eneo, kijiji au mji,
na kisha akaifunga na kuikemea kabla hajaanza kuhubiri na kufanya miujiza
mahali hapo.
Hakuna
mahali popote ambapo
Yesu aliwafundisha mitume wake au mtu mwingine yeyote kwamba Neno la Mungu
linaweza kuwa na nguvu na mafanikio katika eneo fulani ikiwa kwanza
utaibainisha roho ya lile eneo na kuifunga na kuzishinda nguvu zake kwa njia ya
maombi. Kamwe hatusomi popote Yesu akiitumia au kuifundisha mbinu hii.
Mitume
hawakutumia au kufundisha mbinu hii.
Hakuna
mahali popote pale
katika Injili au kwenye Matendo ya Mitume ambapo tunasoma habari za mitume au
mtu mwingine yoyote yule akitumia mbinu za jinsi hiyo katika kuineza Injili.
Mtume Paulo alitembelea miji mingi sana ambamo kulikuwa na zinaa ya kutisha,
mambo ya kimwili, uchawi pamoja na dhambi. Hakuna popote pale ambapo tunasoma
juu yake akizitambua kwanza roho hizo katika miji hiyo ili aone ni aina gani ya
roho za kimaeneo zinazotawala katika miji, wala hatusomi mahala popote pale na
kuona akiomba juu ya roho za aina hiyo ili kwamba kazi ya Injili ipate kustawi.
Hakuna
mahali popote pale
ndani ya maandishi yao kwa makanisa au kwa watu binafsi, ambapo mitume hawa
wamepata kutaja tu mbinu za jinsi hiyo, licha ya kuzifundisha. Yapo mahusia
mbalimbali kwa ajili ya kuomba katika Agano Jipya. Lakini hakuna mahali
popote pale ambapo mitume wanaelekeza kuwa roho za kimaeneo zina uwezo juu
ya watu katika baadhi ya maeneo na kwamba watu hawana budi kuomba dhidi ya roho
hizo na kuzivunja nguvu zake, ili kwamba Injili ipate kustawi na ili wanawake
na wanaume wapate kuokolewa.
Hayapo
mafundisho ya jinsi hiyo ndani ya Agano Jipya. Kwa msingi huu pekee, tunaweza,
kwa usalama kabisa, kuyakataa mafundisho ya jinsi hii.
Lakini
sasa, mtindo wa jinsi hii haufudishwi kwenye Agano la Kale wala hatuna hata
mfano mmoja katika Agano la Kale, unaoelezea juu ya mtu yeyote anayezitambua
roho za kimaeneo na kufunga nguvu zake kabla kazi ya Bwana haijakamilishwa
ipasavyo. Kwa
kweli, waandishi hao wa kisasa wanarejea katika maandishi fulani fulani ya
Agano la Kale, na tutakwenda kuangalia maandishi hayo baadaye, lakini hata
hivyo, hakuna hata andiko moja linalounga mkono mtindo huo na mbinu zao
zinazoenezwa na waandishi hao.
Jukumu
la Uongo
Wanawezaje walimu hawa wa siku hizi kusema, “Lazima
uzitumie mbinu hizi ili kuhakikisha mafanikio ya uInjilisti katika ulimwengu”, wakati
ambapo maandiko hayatushauri kufanya hivyo? Wanaweka jukumu juu ya
watu we Mungu wakati ambapo maandiko hayaweki jukumu la jinsi hiyo. Kwa
maneno mengine, wao huongezea maneno yao juu ya Neno la Mungu – na
wakizitumia mamlaka zao juu ya watu wa Mungu, mamlaka ambazo hazitokani na Mungu.
Hili ni jambo la hatari sana. Ni jambo moja kusema kuwa, kwa sababu maandiko
hayawazuii kuzitumia mbinu hizo, kwa hivyo wao wanajisikia uhuru kuzitumia.
(Hata hivyo, hoja hii si ya msingi, kwa sababu mafundisho yao yanagusa kweli za
msingi za Injili na ufanisi katika kuenezwa kwake, hivyo wanapaswa kuonyesha
kwa uhakika mambo hayo yanafundishwa wapi katika maandiko, kabla hawajafundisha
na kuzitumia kanuni hizo). Lakini kwa kweli wanafundisha kanuni zao za lazima
kwa ajili ya kueneza Injili. Huo ni udanganyifu na unaweza kuwapelekea watu wa
Mungu, kutumbukia katika kuchanganyikiwa, vifungo pamoja na hatari iwapo
watapokea na kuyafuata mafundisho ya jinsi hii.
Ikiwa
mbinu hizi za kuzitambua na kuzifunga roho za kimaeneo ni za lazima kwa ajili
ya kuleta mafanikio ya uenezaji wa Injili, kwa nini basi Yesu pamoja na
mitume wake hawakufundisha wala kutufunulia mambo hayo? Tunaelezwa na hawa
walimu wa kisasa kwamba maombezi dhidi ya mamlaka na uweza juu ya maeneo ya
kijiografia, yanahitajika sana kabla Injili haijapenya katika maeneo
hayo. Je, mitume walikuwa ni wajinga juu ya mbinu hizo? Au labda walishindwa
kutufunulia kile kilicho cha lazima kwa ajili ya uenezi wa Injili, na kwa ajili
ya wokovu wa nafsi za watu? Je kanisa litakuwa limeondolewa ukweli huu wa lazima
kwa muda wa miaka 2000? Hapana! Kanisa halijanyimwa ukweli huu wa lazima, na
bado Injili imeendelea kuenea muda wote huo kwa karne zote hizo, kama Yesu
alivyosema Injili haina budi kuenea, hata bila kanisa kufundisha au
kuzitumia mbinu hizo ambazo hawa walimu wa kisasa wamezibuni. Kutokea muda wa
Matendo ya Mitume hadi kufikia siku hii ya leo, kumekuwepo na uamsho, maelfu ya
watu wamerejea kwa Bwana kwa idadi kubwa, nao wameokolewa kutokana na dhambi,
giza na vifungo vya shetani pasipo hata kujulikana kwa mbinu hizo,
kufundishwa wala kuzitumia!
Kutamani
“matokeo” kupita kiasi.
Lakini
moja ya kusudio lao kuu hawa wahubiri na walimu wa kisasa ni kuona “matokeo”.
Mmoja wa viongozi wa kanisa ambaye anaamini katika kutumia kanuni hizo
amesikika akisema kuwa iwapo kanisa lake halitaongezeka kutoka washirika 1000
hadi kufikia washiriki 2000 ndani ya miaka miwili, basi hapo itakuwa ni
kutokana na kushindwa kwao katika kujaribu kwa makini kufanya hivyo. Kwa maneno
mengine, iwapo tutazitumia mbinu halisi basi tutegemee kanisani washirika
kuongezeka mara mbili zaidi ndani ya miaka miwili! Watu hawa wanalifanya kanisa
kuwa kana kwamba ni aina fulani ya biashara ambapo tunapaswa kuzitafuta kanuni
bora zaidi ili kutoa matokeo na kufikia malengo. Hata makanisa mengi kwa sasa
yameanza kutoa “maelezo ya umisheni” pamoja na malengo yao kwa ajili ya
mafanikio yao. Mtindo wa aina hii kwa kazi ya Mungu, umeazimwa moja kwa moja
kutoka kwa ulimwengu wa kibiashara. Hii yote inamdhalilisha Yesu Kristo ambaye
ndiye kichwa cha kanisa lake ambaye ndiye aliyetuonyesha kwa neno lake jinsi
itupasavyo kujishughulisha wenyewe. Mmoja wao amesema kwa uwazi kabisa kwamba
wanavutiwa zaidi na yale “yanayofanya kazi” ( yaani, yanayoleta mafanikio au
matokeo ) kuliko “yale yaliyo ya kweli”. Kwa hiyo basi, tayari wameanza kujenga
msingi wa udanganyifu wao. Katika kujiondoa kwao kutoka katika miongozo iliyo
sahihi ya Neno la Mungu, wao wamekuwa wakijiweka wazi kwa udanganyifu wa
shetani; kadiri wanavyoendelea na kuzitumia mbinu na kanuni zinazoweza
kuwaletea matokeo ya haraka na yenye kuvutia.
Yesu
anaomba kwa Baba akisema “Neno lako ni kweli”, Yohana17:17. Sasa kama watu wa
Mungu, sote tunatamani na kuomba kwamba Injili iweze kufikia na kuokoa nafsi za
watu wengi watuzungukao na ulimwenguni kote. Lakini watu wa Mungu, maombi yetu,
kazi zetu, pamoja na mafundisho yetu lazima yawe kulingana na neno la Mungu,
ambako ndiyo kweli. Hamu yetu ya “kuona matokeo” isituongoze kuelekea kwenye
kuikataa au kujitenga na Neno la Mungu kama lilivyofunuliwa katika maandiko; au
kuanzisha mbinu zetu wenyewe au mtindo wa fikra kwa ajili tu ya kujipatia kile
kinachoonekana kuwa ni “matokeo” ya haraka. Mengi ya mafundisho hayo ya kisasa
yanasukumwa na mawazo ya “mafanikio” yakikusudia kutafuta kitu fulani
“kinachofanya kazi” na hiyo ni “Mafanikio”. Hawa walimu wa kisasa wanaendelea
kubuni mawazo mapya pamoja na mitindo ya kufundisha. Hakuna hata mmoja
anayeweza kujihoji mwenyewe kuwa inakuwaje kila baada ya miaka michache kunahitajika
“mitindo” mipya, katika mtazamo wa Kitheolojia – hii ni upepo mpya wa imani!
Wala hakuna hata mmoja anayeweza kuuliza, kulitokea nini na ule upepo wa imani
uliopita? Au kutambua kwamba kanisa halihitaji mtindo mpya katika mafundisho
yake ya Imani isipokuwa ni marejeo kwa yale ambayo tayari yamefunuliwa vizuri
katika maandiko. Ikiwa tutakuwa waaminifu, tutapaswa kuungama kwamba,
mafundisho hayo mengi ambayo yanaendeshwa na wazo la mafanikio ni matokeo
yanayotujia moja kwa moja kutoka kwenye mila za kibiashara za Marekani (U.S.A);
mahala ambako kila kitu kinategemea malengo, matokeo pamoja na mafanikio. Na
Wakristo zaidi sana huko Marekani wameazima akili hizo au wamechukua mtazamo na
silka kutoka kwa ulimwengu na wameuingiza kanisani, umewapelekea kwenye ubunifu
wa mafundisho na matendo ya kutatanisha.( Bila shaka, mimi sisemi kwamba, wazo
la roho za kimaeneo linakuja kutoka kwenye desturi za kibiashara, lakini huu msukumo
kwa ajili ya mafanikio – ambao umewapelekea Wakristo hawa kutumbukia katika
ubunifu na udanganyifu).
Mwandishi
na mwalimu ambaye ni mmoja wa waenezaji wakuu wa mafundisho haya anaelezea juu
ya jambo ambalo nimeligusia hapo juu, kuhusiana na kukosekana kwa maandiko
yanayounga mkono mafundisho haya. Katika utangulizi wa kitabu chake alichokiandika
yeye mwenyewe kiitwacho “Territorial Spirits” (“Roho za Kimaeneo”; Sovereign
World Ltd. Ó1991 C.P.Wagner), amesema kuwa, amewahi kutazama kwenye vitabu 100
huko kwenye seminari ya theolojia ambavyo vimezungumzia kuhusiana na somo la
malaika na mapepo, ili aweze kugundua mafundisho yahusuyo roho za kimaeneo.
Anaendelea kueleza kuwa, siku za leo ipo haja kubwa sana ya kufanya utafiti kwa
ajili ya somo hilo. Lakini kwa nini tufanye utafiti? Je utafiti wa kwenye
Biblia hautoshi? Je hatuna Biblia? Neno la Mungu halitoshi kutuelekeza
kuhusiana na jambo kama hili la msingi? Kwa dhahiri kabisa sivyo hivyo, kwa
kuwa yeye hawaaliki watu wafanye utafiti katika Biblia. Ijapokuwa kwa hakika
anajaribu kutafuta ushahidi kwa ajili ya mafundisho hayo kwenye maandiko, kama
tutakavyoweza kuona hapo baadaye, yeye anaenda sehemu nyingine ili kuona iwapo
anaweza kupata uthibitisho kwa ajili ya ubunifu huu wa kigeni. Lakini
anatuambia kwamba ni vitabu vitano tu kati ya 100 vilivyotaja
kuhusiana na somo hilo la roho za kimaeneo, na kati ya hivyo vitabu vitano, ni vitatu
tu ambavyo angalau vinasema chochote kinachoweza kusaidia. Lakini hakuna
chochote kati ya vitabu hivyo ambacho kilistahili kujumuishwa katika kitabu
chake. Hii haishangazi kwa vile mafundisho hayo hayamo pia katika Biblia – na
mpaka sasa hakuna hata mmoja ambaye amebuni au kuyatumia kwa jinsi hiyo, kwa
kadri nifahamuvyo. Kwa hiyo, katika kitabu chake hicho anajumuisha michango
kutoka hasa kwa waandishi wa siku za leo ambao wanaoeneza mawazo ya jinsi hiyo.
Wagner alikuwa anafanya utafiti juu ya kanuni za ukuaji wa kanisa na maombi,
alipowafikia viongozi wa kanisa fulani ambao walikuwa wakifanya aina hii ya
maombezi dhidi ya roho za kimaeneo. Hapo, ilimpelekea kuingia ndani zaidi ya
mafunzo yake juu ya somo hili. Kama tulivyokwisha kuona katika makala nyingine
iliyopita, watu hao wanapofanya utafiti wao hawaanzi kwa kusoma Biblia,
isipokuwa wao huanza kwa kutegemea uzoefu wao wenyewe na “mafunuo ya kiroho”
wanayoyapokea. Ndipo hutafuta maandiko ambayo huyalazimisha au kuyafanya
yaunge mkono “mafunuo” waliyopokea. Nasi tutatazama maandiko hayo hapo baadaye.
Lakini napaswa kusema kuwa, hata hao viongozi wa makanisa – ambao waliiamini
imani hiyo ya kigeni, hawakubaliani wao kwa wao kuhusiana na mafundisho haya, na
namna ambayo yanapaswa kutumiwa. Kwa vile hayaungwi mkono na maandiko ya Neno
la Mungu, basi haishangazi kuona kwamba mmoja wa waenezaji wa mawazo haya
ameamua kusema kwamba kwa kuwa Mungu ni mwenye enzi, basi anafunua mbinu
mpya na bora kwa ajili ya uInjilisti wa ulimwengu mzima. Wanachomaanisha ni
kwamba Mungu anaufunua kwao ufunuo huu usiopatikana katika Biblia,
na hivyo wanajihesabia wenyewe mamlaka ya kitume! Yote hii inaonyesha jinsi
wanavyoiacha imani, kwa vile wanayainua mafununuo yao na uzoefu wao juu ya neno
la Mungu.
Hebu
sasa tuyatazame kwa karibu yale yanayofundishwa na waandishi hawa wa kisasa
kuhusu vita vya kiroho.
0 Comments