SEMINA YA KUPANDA NA KUVUNA 2017



SADAKA INAYOMFANYA MUNGU AKUKUMBUKE
*NA MWL MWAKASEGE*
>>Katika kujifunza somo hili nataka tuangalie point kama tano hivi.
*1 KUNA SADAKA UNAYOWEZA KUMPA MUNGU NA IKAWA UKUMBUSHO MBELE ZAKE ILI AWE ANAITUMIA KUKUMBUKA*
_’’Matendo ya mitume 10:1-4, 31 Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima. Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. akasema, Kornelio, kuomba kwako kumesikiwa, na sadaka zako zinakumbukwa mbele za Mungu’’_
>>Hii si sadaka kama zilivyonyingine maana Mungu huwa anaitumia kukumbuka.
*2 KUNA VITABU VILIVYOKO MBINGUNI AMBAKO KUNA ANDIKWA VITU AMBAVYO MUNGU ANATAKA VIWE KUMBUKUMBU KWA AJILI YAKE NA KWA AJILI YAKO*
_’’Malaki 3:16 Ndipo wale waliomcha Bwana waliposemezana wao kwa wao. Naye Bwana akasikiliza, akasikia; na *kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake*, kwa ajili ya hao waliomcha Bwana, na kulitafakari jina lake’’_
>>Mbinguni kuna Vitabu vya ukumbusho zinakoandikwa kumbukumbu mbali mbali, Ngoja nikuoneshe kwenye maandiko
*a) Kitabu cha uzima cha wenye uhalali wa kukaa na Bwana milele*
_’’Ufunuo 3:5 Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake *katika kitabu cha uzima*, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake’’_
*b) Kitabu kilichofungwa kwa mihuri (seal)*
_’’Ufunuo 5:1 Kisha nikaona katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi* kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa muhuri saba*’’._
>>Yesu ndiye aliye na uwezo wa kukifungua na kufungua hiyo mihuri saba. Na baada ya kufunguliwa kuliandikwa matukio na nyakati yaliyo katika nyakati.
*c) Kitabu cha hukumu*
_’’Ufunuo 20:12 Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na *vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao*’’_
_’’Daniel 7:10 Mto kama wa moto ukatoka ukapita mbele zake; maelfu elfu wakamtumikia, na elfu kumi mara elfu kumi wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na *vitabu vikafunuliwa*’’._
*d) Kitabu cha mashtaka yanayopelekwa na mshitaki ibilisi*
_’’Wakolosai 2:14 akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani;’’_
*e) Kitabu wanachopewa watumishi*
“_Ufunuo wa Yohana 10:1-10, 8 Na sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena, ikisema, Enenda, ukakitwae kile kitabu kilichofunguliwa katika mkono wa yule malaika, aliyesimama juu ya bahari nag juu ya nchi.9 Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali. 10 Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mkono wa malaika yule, nikakila; nacho kikawa kitamu kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu.”_
 katika agano la kale walitumia neno gombo na walikuwa wanaitwa chuo au gombo la chuo. Mfano Kitabu cha Isaya kiliitwa chuo cha nabii Isaya. Utumishi kitabu ambacho Mungu kawapa watumishi ili waweze kwenda kama kilivyoagiza. _”Yohana 1:8 8 Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana”_
*f) Kitabu cha ukumbusho*
_”Waebrania 9:18-22 Kwa hiyo hata lile la kwanza halikuanzwa pasipo damu. Maana kila amri ilipokwisha kunenwa na Musa kwa hao watu wote, kama ilivyoamuru sheria, aliitwaa damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji na sufu nyekundu na hisopo, akakinyunyizia kitabu chenyewe, na watu wote, akisema, Hii ni damu ya agano mliloamriwa na Mungu. Na ile hema nayo na vyombo vyote vya ibada alivinyunyizia damu vivyo hivyo. Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo._
 Jinsi Musa alivyokuwa anaweka wakfu vitu vya hema. Na maandiko yanasema kilichokuwa kinafanyika kwenye hema kilikuwa ni kivuli cha mambo ya ulimwengu wa roho yaliyo halisi.
 Vitu vyote ndani ya hema vilikuwa vinatakaswa kwa damu na Musa alikuwa anasema hii ni damu ya agano , Pia katika agano jipya tunaona _”Basi, Mungu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji Mkuu wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu Yesu, Waebrania 13 : 20”_
 Vitabu vilivyoko mbinguni aliye na uhalali wa kuvifungua ni Yesu ili na sisi tupate uhalali wa kuvifungua tunahitaji damu ya Yesu. kufuta hati za mashtaka tunahitaji damu ya Yesu, uzima wa milele unahitaji damu ya Yesu ili kufuta dhambi zako. Pia katika utumishi napo ili utumike vema unahitaji kunyenyekea chini ya damu ya agano.
  *Yesu alijitoa kuwa sadaka ili iwe ukumbusho wa agano Jipya*
*3 SADAKA YAKO INAPOINGIZWA KATIKA KITABU CHA KUMBUKUMBU CHA MUNGU NA MUNGU ANAITUMIAJE*
_”Malaki 3:16’18 16 Ndipo wale waliomcha Bwana waliposemezana wao kwa wao. Naye Bwana akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao waliomcha Bwana, na kulitafakari jina lake. *17 Nao watakuwa wangu, asema Bwana wa majeshi, katika siku ile niifanyayo; naam, watakuwa hazina yangu hasa; nami nitawaachilia, kama vile mtu amwachiliavyo mwanawe mwenyewe amtumikiaye* 18 Ndipo mtakaporudi, nanyi mtapambanua kati ya wenye haki na waovu, na kati ya yeye amtumikiaye Mungu na yeye asiyemtumikia.
_Malaki 4:1-3 “1 Kwa maana, angalieni, siku ile inakuja, inawaka kama tanuru; na watu wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa majeshi; hata haitawaachia shina wala tawi. 2 Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mbawa zake; nanyi mtatoka nje, na kucheza-cheza kama ndama wa mazizini. 3 Nanyi mtawakanyaga waovu; maana watakuwa majivu chini ya nyayo za miguu yenu; katika siku ile niifanyayo, asema Bwana wa majeshi.”_
 angalia kwa makini hapo mstari wa 17, utajifunza kitu kikubwa sana . Anaposema nitaifanya siku, lakini tukienda kwenye Mwanzo tunaona siku ziliumbwa sasa anaposema *ataifanya siku ina maana ni siku ambayo haikuwepo na ni tofauti na zile siku za kawaida na hii siku ni maalumu kwa ajili ya kukusaidia ili usiangamie. Tunakwenda sawa sawa..
 Sasa anaposema siku ile inakuja ina maana sio siku nzuri (hapa nazungumzia siku ya kwenye Malaki 4:1-3). Na hiyo siku ni ya kuteketeza au siku ya uharibifu sasa hii ni tofauti na ile siku ya kwenye Malaki 3:16-18. Ndio maana ukitoa sadaka yako Mungu anaiweka kwenye kitabu cha kumbukumbu kwa ajili ya kukutengenezea siku ili kuja kukutoa au kukuokoa na katika siku ya uharibifu. Na ile Mungu kukuandalia siku ina maana anakuja kukutembelea yaani anapanga special .. ziara maalumu kwa ajili yako .
*4 SADAKA HIYO YA UKUMBUSHO INAMFANYA MUNGU AKUKUMBUKE WEWE NA JAMAA YAKO NA RAFIKI ZAKO KWA SABABU YA SADAKA YAKO ULIYOITOA*
_”Matendo ya Mitume 10:23-24 23 Akawakaribisha wawe wageni wake. Hata siku ya pili, Petro akaondoka akatoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu waliokaa Yafa wakafuatana naye. 24 Siku ya pili yake wakaingia Kaisaria. Na Kornelio alikuwa akiwangojea, hali amekusanya jamaa zake na rafiki zake.”_
 Siku ile ambayo Malaika anaenda kumtembelea Kornelio na kumwambia Yale yampasayo kufanya alikuwa na marafiki zake yaani walipewa VIP treatment kwa sababu ya sadaka za Kornelio zilizokuwa zimewekwa kwenye kitabu cha kumbu kumbu cha Mungu. Wayahudi walikuwa wanashangaa sana kuwa imekuaje sasa hili jambo, lakini Yesu ndiye mwenye control ya vitabu ni Yesu ambaye aliangalia kwenye vitabu vya kumbukumbu mbinguni na kuona inatakiwa Kornelio apewe maelekezo juu ya juu ya mambo yampasayo kufanya.
>>Sadaka za aina hii huwa zinatoa VIP treatment ya Mungu kuja kukupa instructions kwa watu wake _Mwanzo 19:29 Ikawa Mungu alipoiharibu miji ya Bondeni, *Mungu akamkumbuka Ibrahimu, akamtoa Lutu katika maangamizi alipoiangamiza miji hiyo aliyokaa Lutu*._
>>Lutu alipona kutokana na sadaka alizokuwa anatoa Ibrahimu kwa Mungu, haijalishi wako Sodoma na Gomora lakini Mungu alimkumbuka kwa sababu ya Ibrahimu, hii neema sana kukumbukwa na Mungu kwa ajili ya sadaka ya mtu mmoja.
>>Pia kwa ajili hiyo maandiko yanasema _*’’Kumbukumbu la Torati 2:9Bwana akaniambia, usiwasumbue Wamoabi, wala usishindane nao katika mapigano; kwa kuwa sitakupa katika nchi yake kuimiliki; kwa sababu Ari nimewapa wana wa Lutu kuimiliki’’*_
>> Umeona hata wana wa Israel hawakuweza kupigana na wana wa Lutu, Mungu aliendelea kuwakumbuka kwa ajili ya ile sadaka aliyotoa Ibrahimu, na wanakumbukwa mpaka leo. Tunakwenda sawa sawa.
_Kutoka 2:24-25 Mungu akasikia kuugua kwao, *Mungu akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu na Isaka na Yakobo*. Mungu akawaona wana wa Israeli, na Mungu akawaangalia._
Hapa tunaona namna Mungu alivyowakumbuka wana wa Israel, kwa sababu si ya kilio chao bali ni kwa sababu aliangalia agano alilofanya na Ibrahimu na agano alilifanya kwa njia ya sadaka na ndio maana maandiko yanasema _*Zaburi 50:5 Nikusanyieni wacha Mungu wangu Waliofanya agano nami kwa dhabihu*_
Sasa katika kiingerea wamesema Sacrife yaani sadaka na sadaka ilitolewa angalia Mwanzo 15:8-19 Akasema, Ee Bwana MUNGU, nipateje kujua ya kwamba nitairithi? Akamwambia, *Unipatie ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa*. Akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akaweka kila kipande kuelekea mwenzake, ila ndege hakuwapasua. Hata tai walipotua juu ya mizoga Abramu akawafukuza. Na jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia. Bwana akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali mengi. Lakini wewe utakwenda kwa baba zako kwa amani, utazikwa katika uzee mwema. Na kizazi cha nne kitarudi hapa, maana haujatimia uovu wa Waamori bado. Ikawa, jua lilipokuchwa likawa giza, tazama, tanuru ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama. *Siku ile Bwana akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati*,
Umeona hapo uhusiano wa sadaka na agano, ndio maana pale katika Kutoka Biblia inasema Mungu alilikumbuka agano na agano ndilo hilo nililokuonesha hapo juu. Na ndio maana katika matendo ya mitume tunaona Mungu akimtuma malaika na kuwambia Kornelio aende kwa Petro yaani kupata instructions. Na kwa wana wa Israel Mungu alimtuma Musa, maandiko yanasema _Kutoka 6:2-5 Kisha Mungu akasema na Musa, akamwambia, Mimi ni YEHOVA; nami nilimtokea Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kama Mungu Mwenyezi, bali kwa jina langu YEHOVA sikujulikana kwao._
>>Walitolewa Misri kwa sababu ya kumbukumbu na ndio maana siku ile walipojirahibu nafsi zao Musa alisema _Kutoka 32:13-14 Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, Nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu nao watairithi milele_ ndio maana Mungu aliacha, kwa sababu ile sadaka aliyoitoa Ibrahimu katika lile agano ilikuwa inambana Mungu kwa sababu aliahidi kufanya kuwapeleka Kanani. Japo walikuwa wanaabudu ndama bado walipewa VIP treatment kwa sababu ile sadaka ya Mzee Ibrahimu na Mungu aliendelea kuwakumbuka.
>>Japo shetani alimtengenezea Yusufu mashtaka ya uongo na kutupwa jela na kusahauliwa kwa miaka miwili jela lakini Mungu alihakikisha Farao anaota ndoto na ile ndoto Yusufu aliitafsiri na baadae alitolewa jela na akawa huru na kuwa waziri mkuu. Leo ni siku yako ya wewe Mungu kukumbuka saa ikifika hamna mtu wa kukuzuia na ataikumbuka sadaya yako na atawavusha na ndugu zako.. ooh haleluyaa haleluyaaa.
>> Hata Paulo alipo okoka na alikuwa hakubaliwi na wanafunzi, Mungu alimuinua Anania na alipomwekea mikono na Kumwacha Paulo alijua kuwa atakubalika kwa wanafunzi, lakini haikuwa hivyo, na bado Mungu alimwinulia Barnaba wa kumtambulisha kwa wanafunzi hadi alikubalika maandiko yanasema na walipoona neema niliyopewa walinipa mkono wa shirika, na wewe leo ni siku yako kupitia sadaka yako unayoitoa Mungu atakukumbuka na kukuinulia watu mbele yako ili kukuvusha kwa hiyo usikate tamaa.
_*’’Mwanzo 30:22-24 Lea akasema, Mungu amenipa mahari njema, sasa mume wangu atakaa nami, kwa kuwa nimemzalia wana sita. Akamwita jina lake Zabuloni. baadaye akazaa binti, akamwita jina lake Dina. Mungu akamkumbuka Raheli; Mungu akamsikia, akamfungua tumbo’’*_
>>Lea alipozaa mtoto alijua ndiyo nafasi kupendwa na Mungu alimpomkumbuka Raheli, haikuwa mimba ya kawaida maana ndiyo mimba iliyombeba Yusufu na Yusufu alikuwa kabeba kitu kikubwa sana. Pia ukisoma katika kitabu cha Samweli utakutana na habari za Hana, na utaona namna Hanna alivyotoa sadaka ya nadhiri ya kumtoa Samweli kama mtumishi wa Mungu na Mungu alimwezesha kumpata mtoto.
>>Ukijua kilichoko ndani ya Sadaka, nakwambia utamtafuta Mungu kwa spidi sana maana sadaka ya Ibrahimu ilimfanya Mungu akumbuke kizazi chake kilichokuwa Misri kwa miaka 400. Na Mungu alikitoa kizazi cha Ibrahimu utumwani.
*5 Unatoaje sadaka iwe ukumbusho mbele za Mungu*
>>Kuna tofauti gani kati ya sadaka unayoitoa kuwa ukumbusho kwa Mungu au Sadaka ya Hazina.
Sadaka ya ukumbusho inamfanya Mungu kakuumbia siku maalumu ya kuja kukutoa kwenye shida
*i) Toa sadaka kwa imani ili Mungu asikusahau siku ya uhitaji wako mkubwa na aingilie kati*
_Waebrania 11:1,31 Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana., Kwa imani Rahabu, yule kahaba, hakuangamia pamoja na hao walioasi; kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi kwa amani._
Toa sadaka yako kwa Imani, maana hiyo sadaka itakusaidia sana kuvuka katika magumu utakayokutana nayo au kukutoa kwenye hali hiyo, sadaka aliyoitoa (Ya kuwakaribisha wapelelezi) Rahabu ilikuwa msaada sana kwake
Ukisoma _Yoshua 2:9-13 akawaambia wale wanaume, Mimi najua ya kuwa Bwana amewapa ninyi nchi hii, na ya kuwa hofu imetuangukia mbele yenu, na ya kuwa wenyeji wote wa nchi wanayeyuka mbele yenu. Maana tumesikia jinsi Bwana alivyoyakausha maji ya bahari ya Shamu mbele yenu, hapo mlipotoka Misri, tena mambo hayo mliyowatendea wafalme wawili wa Waamori waliokuwa huko ng’ambo ya Yordani, yaani, Sihoni na Ogu, mliowaangamiza kabisa. Na mara tuliposikia hayo mioyo yetu iliyeyuka, wala haukusalia ujasiri wo wote katika mtu awaye yote, kwa sababu yenu; kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu, katika mbingu juu na katika nchi chini. *Basi sasa, nawasihi, niapieni kwa Bwana, kwa kuwa nimewatendea ihisani, ya kwamba ninyi nanyi mtaitendea ihisani nyumba ya baba yangu; tena nipeni alama ya uaminifu*; ya kwamba mtawaponya hai baba yangu na mama yangu, na ndugu zangu wanaume na wanawake, na vitu vyote walivyo navyo, na kutuokoa roho zetu na kufa._
>>Kilichokuwa ndani ya Rahabu ni imani na ndio maana aliamini kuwa watu hawa walipoingia kwake na yeye alisema ndio sehemu yenyewe ya kutokea na aling’ang’ana na aliomba Mungu amtoe kwenye ile hali ya ukahaba aliyokuwa nayo. Na ndio maana maandiko yanasema kuwa Yoshua aliwaambia kuwa watakapofika katika ile nchi ya Yeriko wasije wakamsahau Rahabu, na walipomchukua Rahabu tunaona wakimuweka nje ya matuo maana walikuwa hawaamini kabisa kuwa anaweza changamana nao, lakini baadae tunaona akija kuingia katika ukoo wa Yesu.
*ii)Unganisha sadaka hiyo na maombi*
_Isaya 43:26 Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako._ eleza mambo yako unapokuwa unapeleka sadaka yako kwa Mungu.
*iii) Kuna maombi yanayowekwa kwenye kumbukumbu za Mungu juu mbinguni*
>>Mungu alimwambia Kornelio kuwa sadaka na sala zako zimefika Mbinguni, na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.
Mwaka 1985 nilikuwa naombea nchi kuwa Mungu atuinulie watumishi wazawa, na nakumbuka ilikuwa siku moja (saa za kazi) kule Arusha nilienda kwa mchungaji wa Anglican, na niliomba ufunguo wa kanisa na nilienda madhabahuni na niliomba Mungu naomba tuinulie watumishi wazawa kama ulivyofanya kwa nchi zingine. Na utakapowanuia naomba usinisahau na *kweli Mungu hajanisahau mpaka leo kanikumbuka* na kipindi kingine nilikuwa naamka usiku kuomba na bendera ya Tanzania na ndipo Mungu alinifundisha kutoa sadaka kila msimu, kila msimu mpya ukianza huwa natoa sadaka, ili Mungu anisaidie.
>>Hii siku haikuwepo kabisa na Mungu kaifanya maalumu kabisa, Mzee Mmanyi anajua kitu naongea. Lakini Mungu kaifanya maalumu siku ya leo hapa Diamond jubilee.
*iii) Unganisha na wimbo wa kumtukuza Mungu*
>>Hesabu 10:10,9 _Tena katika siku ya furaha yenu, na katika sikukuu zenu zilizoamriwa, na katika kuandama miezi kwenu, *mtapiga hizo tarumbeta juu ya sadaka zenu za kuteketezwa, na juu ya dhabihu za sadaka zenu za amani; nazo zitakuwa kwenu ni ukumbusho mbele za Mungu wenu; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu*_.
_Tena hapo mtakapokwenda kupiga vita katika nchi yenu, kupigana na adui awaoneaye ninyi, ndipo mtakapopiga sauti ya kugutusha kwa tarumbeta; nanyi mtakumbukwa mbele za Bwana, Mungu wenu, nanyi mtaokolewa na adui zenu_.
>>Kama unatoa sadaka na kuna hali ndani unasikia kuimba endelea na huo wimbo usiache endelea nao na imba, na siku umepata shida utaona huo wimbo ukikurudia na utashangaa msaada wa Mungu ukikujia. Na Mungu atakukumbuka na kukusaidia. Mwaka huu kule Arusha kwenye semina dada mmoja alikuja kushuhudia ambavyo Mungu alimsaidia kupata mtoto baada ya kukosa mtoto kwa miaka 9. Na kampa jina lake Christopher kwa sababu siku moja nilienda wanapofanya kazi na nilikuwa nimemsindikiza mke wangu. Nilipokuwa kwenye gari binti alikuja na akanieleza kuwa baba nina shida ya mtoto sijapata kwa miaka 9 sasa. Na nilimuuliza unataka mtoto wa aina gani akainiambia wa kiume na nilimuombea nikiwa kwenye gari, baada ya muda akapata mimba na sasa kajifungua mtoto wa kiume kama tulivyoomba.
*iv) Unapokula chakula cha Bwana, na unganisha na moambi ili jambo lako liwe ukumbusho mbele za Mungu*
>>Yesu alisema fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu, haijalishi unapita mazingira gani siku ya leo Mungu akukumbuke na akusaidie na unapota sadaka hakikisha unaomba na tamka nano.
*Mungu akubariki sana kwa kusoma somo hili, na liweke kwenye matendo hakikisha unatoa sadaka yako kwa Mungu na hakika Mungu atakukumbuka, Kasome biblia na angalia sadaka moja ya Ibrahimu aliyoitoa inadumu mpaka leo, na wewe fanya hivyo Mungu atakumbuka kizazi chako. Bwana akubariki na uwe na mwaka mwema 2017 ukafanyike Baraka sana kwako na hakika ukamuone Mungu akikusaidia na kukuvusha*.
Kupanda Kanda hii ya somo hili piga namba hii 0754249590 au 0754766517
Ubarikiwe sana na kila la kheri.
      

Post a Comment

0 Comments